November 18, 2018





Na Saleh Ally
KOCHA Mwinyi Zahera anapaswa kuambiwa kile ambacho hakiamini na kama akiweza anaweza akakifanyia kazi ili kuona kama haiwezekani.


Mtu kama Zahera anaweza akawa na mambo mawili ndani ya nafasi yake, lakini akaendelea kubaki yeye kwa kuwa kila mwanadamu si rahisi kusoma alichonacho ndani ya moyo wake.

Kocha huyu raia wa DR Congo, kwangu sitaungana na wale wanaosema si kocha mzuri, lakini lazima tukubali, uzuri unaweza kupungua kutokana na kutojua kosa au kosa la makusudi.



Nataka nianzie katika suala la mambo mawili ndani ya nafsi ya Zahera ambayo ni maslahi ya Yanga na maslahi yake binafsi.

Kama kocha lazima atakuwa navyo vyote kwa kuwa naye ni mwanadamu. Anataka Yanga ifanikiwe ili naye kimaslahi afanikiwe kwa kuwa yatakuwa ni mafanikio yake kwa maana ya maslahi binafsi.

Katika hayo mawili, lile la kufanikiwa kwa Yanga linapaswa kuwa juu kwanza na baada ya hapo binafsi na kutengeneza ubora wa uhalisia, lile la pili, linapaswa kuwa na nafasi ndogo kwa kuwa linabebwa na lile la kwanza.


Nilichoanza nacho nikitaka Zahera aambiwe ukweli ni kuhusiana na Amissi Tambwe ambaye alikuwa majeruhi na sasa amerudi uwanjani.


Wakati fulani Zahera aliwahi kusema Yanga inahitaji pointi tatu badala ya mabao mengi ya kufunga. Hakika ni sahihi kuanza kupiga hesabu za kutofungwa lakini muhimu sana suala la mabao mengi ya kufunga. Hili si geni na la kwanza kwa mpira wa hapa Tanzania. 
Tambwe bado ana nafasi ya kuikwamua Yanga hapa ilipofikia.


Raia huyo wa Burundi amekuwa kati ya washambulizi waliowafunga wengi midomo ya hisia kwamba yeye ni mshambuliaji wa kuvizia.
Idadi ya mabao aliyofunga inabaki kuonyesha ni mshambulizi mwenye uwezo wa kufunga tena na tena. Hata kama kiwango chake kitapungua, ataendelea kuwa msaada.


Mara ya mwisho Yanga ilipobeba ubingwa ikilingana pointi na Simba, Tambwe ndiye alikuwa shujaa akifunga mabao muhimu ya mwisho. Wakati huo alikuwa ametoka katika majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu na wakati anarudi, Yanga walikuwa wakilia mishahara. 




Mechi dhidi ya Prisons, Tambwe alifunga bao muhimu lililoiingiza Yanga rasmi kwenye foleni ya kuwa bingwa ikiwa na uhakika wa asilimia 90. Tena alionyesha namna alivyopambana na kuzima yale maneno ya mtaani kwamba huwa anavizia tu.


Msimu mmoja uliopita wa 2016-17, Tambwe alifunga mabao 11. Ulikuwa ni msimu ambao alikuwa na changamoto kubwa ya majeraha mfululizo.

Pamoja na mara nyingi kuwa nje ya uwanja na kurejea, akapanda haraka na kufikisha mabao hayo huku Simon Msuva akimaliza na mabao 14 na kuwa mfungaji bora akilingana na Abdulrahman Mussa.


Msimu uliopita ukawa wa Emmanuel Okwi ambaye aliisaidia Simba kurudi na kubeba ubingwa. Hii bado haipitishi kuonyesha Tambwe ameisha, kwa kuwa msimu huo alicheza mechi mbili tu kutokana na majeraha.

Mchezaji aliyefunga mabao 34 ndani ya misimu mitatu ya Ligi Kuu Bara pekee, huyu ni mtu hatari kwa kuwa kuna washambulizi wana misimu 10 hawajafikia idadi hiyo ya mabao.


Kujua Tambwe ameisha ni lazima kumpa nafasi ya kutosha ili kujihakikishia. Kuhakikisha hilo kwa kumpa dakika 10 tu za uwanjani haiwezi kuwa sawasawa.


Nilisema Zahera aambiwe kwa kuwa nilikuwa nina hofu ya maslahi binafsi. Kwamba kama inawezekana anajaribu kuendelea kumjengea hali ya kujiamini mshambulizi Heritier Makambo hata kama anafanya vibaya, basi aendelee kumjaribu.

Niliita maslahi binafsi labda kwa hisia kwamba Makambo aliletwa na Zahera, basi ndiyo lazima acheze. Kipa Klaus Kindoki ameonekana bado hayuko vizuri hata Zahera alipomjaribu mara nyingine, amekubali na leo tunaona nafasi ya kipa ilivyo vizuri kupitia Beno Kakolanya.


Maana yake anaweza kutoa nafasi kama hiyo kwa Tambwe na Makambo akaendelea kubaki benchi na kujifunza namna mkongwe huyo anavyofanya kazi yake na hapa ndiyo unaweza kusema ni maslahi ya Yanga.

Nafasi ya Makambo kujifunza bado ni kubwa sana na binafsi ninaamini ni mshambulizi mzuri lakini bado anayo ya kujifunza ambayo tayari Tambwe alishajifunza.


Maana yake, huu wakati unafaa kwa Makambo kukaa benchi na Tambwe apate muda wa kutosha ili kubadili gia ya Yanga katika ufungaji. 


Kama ndiyo atakuwa ameisha, muda wa kutosha kucheza, utadhihirisha hilo kama ambavyo Waingereza wanasema, “Time Will Tell.”


TAMBWE NA LIGI KUU KATIKA MISIMU MINNE:

2013-14
Tambwe                                  Simba    19           
Tchetche                                 Azam     13           
Mrisho Ngassa                    Yanga       13           
Elius Maguri                          Ruvu       13           
Hamis Kiiza                           Yanga      12

2014-15
Msuva                                  Yanga    17           
Tambwe                               Yanga    14            
Chidiebere                           Stand     11           
Okwi                                     Simba    10           
Kavumbagu                         Azam      10           

2015-16
Tambwe                  Yanga    21           
Kiiza                         Simba   19           
Ngoma              Yanga    17           
Maguri                    Stand     15           
Juma                 Prisons  15           

2016-17
Msuva                       Yanga    14                                               
Mussa                     Ruvu     14                                               
Yusuph                       Kagera  12                                               
Chirwa                        Yanga    12                                               
Kichuya                       Simba   12                                               
Tambwe                      Yanga   11


2 COMMENTS:

  1. Picha hiyo ya beki katili ya nini unatukumbusha? Mimi ni shabiki wa Simba lakini unyama ule aliofanyiwa Tambwe na beki huyo wa Ruvu, ilinifanya nimchukie huyo beki katili na kumuombea kwa Mungu kwa kitendo chake cha kinyama.

    ReplyDelete
  2. Nakubali saana TAMBWE anajua zaidi ya MAKAMBO kiufupi MAKAMBO hajui bora amuchezesha TAMBWE aachane na utaifa na maslah binafsi, huwez cheza na kiungo mwenye asist nyiingi alaf ubamagoli machache mno mbele ya mfumo wa 4:3:3 mda mwingingne 4:2:3:1 yeye akiwa foward tegemez alaf haonesh chochote

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic