December 26, 2018





NA SALEH ALLY
GUMZO sasa ni namna mabingwa wa soka Tanzania, Simba walivyofanikiwa kufuzu na kucheza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


Inakuwa timu ya tatu kufanya hivyo baada ya Yanga, halafu Simba mwaka 2003 na baadaye Simba imerudia kufanya hivyo na kwa pamoja tunakubaliana katika ukanda wa Afrika Mashariki, hatua hiyo imekuwa ngumu sana.


Imekuwa ngumu kiramani na kiuhalisia kwa kuwa si vibaya kusema mara zote timu ambazo zimekuwa zikifuzu katika hatua hiyo ni zile kutoka Ukanda wa Kaskazini mwa Afrika lakini pia zile za Magharibi mwa bara hili.


Afrika ya Kati, mfano Gabon, DR Congo, Congo ambalo ni maarufu kama Brazzaville nao wamekuwa na nafasi kubwa ya kuingia na kucheza katika hatua hiyo.


Kusini mwa Afrika pia wana nafasi yao na zaidi walikuwa ni Zambia na Afrika Kusini kutokana na ubora wao wa maendeleo na kifedha pia wamekuwa wakiingia mara kwa mara na kutengeneza ufalme mpya wa timu za nchi hiyo kuingia katika hatua hiyo.


Kurudi kwa Simba katika hatua hiyo kunasahaulisha mambo mengi sana ikiwemo ile miaka mitano ya Simba kuwa nje ya michuano ya kimataifa. Machungu, machozi na jasho ya mashabiki wa Simba ambao walipokonywa jina la “Wa Kimataifa.”


Sasa umekuwa ni wakati mwingine wa kuamini kwao ndiyo maana hakuna ubishi tena pale tulipowaona mashabiki wa Simba pekee wakiingia na kukaribia kuujaza uwanja wa taifa.


Hali ile ilikuwa ni ujumbe wa imani mpya lakini bado sote tunaona kwamba Simba imeitoa timu bora kutoka Zambia. Tena ile ambayo ilifanikiwa kupata ushindi kutoka kwao.

Kama timu ya Zambia inashinda kwao, lakini mechi inayofuata inashindwa kuulinda ushindi wake tena baada ya kuwa ilianza kufunga bao katika mechi ya pili. Hili si jambo dogo.


Angalia bao lililoivusha Simba, bao muhimu zikiwa zimebaki dakika mbili, kazi nzuri ya Shiza Kichuya aliyetokea benchi. Lakini kazi nzuri zaidi ya mmaliziaji, Cleotus Chama ambaye anafunga bao la “kideoni” huku akiwa na uhakika kabisa kwa kuwa wakati mpira unakimbilia kuvuka msitari, yeye alishaanza kukimbia kwenda kushangilia.


Simba hii, ndiyo ileile ya miaka mitano iliyopita. Kipindi Simba ilishindwa hata kubeba ubingwa wa Bara. Simba ambayo ilishindwa hata kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara?

Leo Simba inasonga kwenye hatua ya makundi katika hali ya kujiamini, kiwango bora na sahihi. Hakika hili ni jambo la aina yake, jambo ambalo linaweza kuwa dawa mpya kwa wale ambao walikuwa hawaamini timu za Tanzania zinaweza kusimama tena.


Tukubali, bao la Chama lilikuwa bora kuanzia utengenezwaji wake na hata umaliziaji. Maana yake kuna mambo makubwa yanaweza kufanywa na timu za Tanzania kama wachezaji watatengenezwa, kuhakikishiwa maslahi yao na kuelezwa kinachotakiwa.

Pamoja na hivyo, tukubali. Kuna timu zimewekeza lakini bado mambo si mazuri. Binafsi naona zinaweza kuwa zinakosa nguvu ya mashabiki. Mfano Azam FC imewekeza vizuri lakini inaweza kuwa na ugumu wa kufikia hatua hiyo kwa kuwa nguvu ya mashabiki ambayo huzaa presha na hamu kuu ya mafanikio hawana.


Mashabiki wa Simba waliokuwa uwanjani siku ya Jumapili, kwa mchezaji lazima utakuwa na hamu ya kuhakikisha wanatoka uwanjani wanafurahi. Utakuwa na hofu ya kuwakasirisha na kuwakatisha tamaa kwa kuwa utakuwa unajua walifika pale uwanjani kuwaunga mkono nyie.

Hivyo, presha yao inakuwa msaada na hasa kama itatumika vizuri. Ikitumika vibaya, mashabiki wanaweza kuwa “sumu” na kuwamaliza kabisa. Mambo yalikuwa mazuri kwa Simba maana mashabiki hao wakawa “maziwa.”


Kuna kila sababu sasa ya kujiamini kama dawa, kwamba Simba inaweza kufanya vema hata kama imeingia makundi na kukutana na timu vigongo. Hatua hiyo ilikuwa ni lazima iwe hivyo kwa kuwa ni hatua ya wanaojua, hatua ya wazoefu au waliofikia mbali.


Pamoja na hivyo, dawa iwaingie kwa namna Simba ilivyofika hapo kwamba hakuna kisichowezekana hasa kama utajipanga sahihi.


2 COMMENTS:

  1. Gumzo kwa leo ni MASHUJAA

    ReplyDelete
  2. Mpeleke Mashujaa akacheze na Nkana FC au Zamalek ya Egypty.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic