December 5, 2018







 Kesi ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania   (TFF), Jamal Malinzi na wenzake, Selack Mesaki ambaye   alikuwa Mhasibu wa TFF, imesikilizwa leo ambapo shahidi wa 9 alitoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu 
Mkazi Kisutu, Dar, na kupokewa na Hakimu  Mkazi, Wilbard Mashauri.


Malinzi anatuhumiwa na makosa 28, huku 23 kati ya hayo yakiwa ni kufoji risiti za kuwa anaidai TFF na kujipatia pesa zaidi ya dola laki 2 ambazo zinaonyesha zilianza kufojiwa tangu Novemba 2013 hadi Julai 2016.


Shahidi wa tisa, alifikisha vitabu vya  risiti vilivyotumiwa na Malinzi kwa ajili ya kutolewa fedha za mkopo kutoka kwake kwenda TFF, ambapo Wakili Mashauri alikubali ushahidi huo baada ya shahidi kuzitambua.


Miongoni mwa risiti hizo ni zenye namba 00831 ya Mei 9, 2016 ambayo inaonyesha kuwa kiasi cha dola 8000, namba 00832 ya Mei 9, 2016  inaonyesha alitoa dola laki saba, risiti namba, 00870 ya Mei 27, 2016 ambayo ilitoa kiasi cha shilingi milioni tano kwa ajili ya maandalizi ya timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17.


Risiti nyingine ni ile inayosomeka namba 00931 ya Juni 16, 2016 ambayo aliikopesha TFF dola 10,000, risiti  namba 00947 ya Agosti 2, 2016 iliyoonyesha kuwa Malinzi alitoa dola 1,000 kwa ajili ya kuwezesha safari ya Afrika Kusini ya Ayubu Nyenzi na Pelegrinius Rutayuga.


Aidha, ushahidi mwingine wa risiti uliotolewa ni namba 010137 ya Septemba 21, 2016 ambayo inaonyesha Malinzi ameikopesha TFF shilingi milioni 7, risiti namba 01042 ya Septemba 21, 2016 iliyotolewa shilingi milioni tatu ikitoka kwa Malinzi kwenda TFF ikiwa ni posho kwa ajili ya timu ya vijana chini ya miaka 17.


Pia kuna risiti namba 01071 ya Septemba 22, 2019 ambayo inaonyesha imetolewa dola elfu 15 kutoka kwa Malinzi ikiwa ni mkopo kwa ajili ya safari ya timu ya vijana chini ya miaka 17 kwa ajili ya kwenda Rwanda na Congo.


Baada ya kuwasilisha ushahidi huo, mawakili upande wa washtakiwa wakiongozwa na Richard Rweyongeza, walimuhoji shahidi huyo mambo mbalimbali kuhusiana na ushahidi huo, huku pia wakiomba siku nyingine mashahidi waweze kusikilizwa watatu na siyo mmoja ili kesi iende haraka.


Baada ya pande zote mbili kusikilizwa, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 18, mwaka huu.

Mbali nan Malizi, washtakiwa wengine ni aliyekuwa Katibu wa TFF, Nsiande Isawayo Mwanga, Meneja wa Ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na karani, Flora Rauya.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic