January 15, 2019


KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya mwenyekiti wake, Malangwe Mchungahela, imetangaza kuwa, uchaguzi mdogo wa Klabu ya Yanga upo palepale.

Uchaguzi huo ambao ulisimamishwa kutokana na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kufungua kesi mahakamani kuupinga, sasa tarehe ya kufanyika kwake itajulikana baada ya siku saba zijazo kuanzia jana Jumatatu.

Akitangaza uamuzi huo, Mchungahela amesema: “Baada ya wanachama wale kufungua kesi mahakamani kupinga kufanyika kwa uchaguzi, tumegundua walikuwa wakihoji juu ya mambo makuu matatu, mosi ni kutaka kujua uhalali wa kadi za wanachama.

“Pili, kukataliwa kwa baadhi ya majina ya wanachama wa Yanga na tatu ni sintofahamu juu ya aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji ambapo ilisababisha baadhi yao kutowania nafasi.

“Kutokana na hayo yote, kama kamati tumeweza kukutana na wahusika wote hao na kukubaliana kwamba waondoe kesi hizo mahakamani na wamefanya hivyo.

“Hivyo basi, nipende kutangaza kuwa uchaguzi huu mdogo wa Yanga ambao ni wa kujaza nafasi za viongozi walioachwa wazi, tarehe yake itatangazwa baada ya siku saba zijazo kuanzia jana Jumatatu.

“Niwakumbushe tu kuwa, huu ni uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi, hivyo viongozi watakaoingia madarakani hawatakaa kwa zaidi ya miaka miwili. Baada ya hapo ndipo utafanyika uchaguzi mkuu.” alisema.

Ikumbukwe kuwa, uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Jumapili iliyopita, ulisimamishwa siku mbili kabla ya kufanyika kutokana na baadhi ya wanachama wa Yanga kutoka zaidi ya mikoa minne ya Tanzania kufungua kesi mahakamani kupinga kufanyika kwake.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic