KAMPUNI ya Multichoice Tanzania inayomiliki ving'amuzi vya DStv, imepata idhini ya kuonyesha michuano ya Kombe la SportPesa inayotarajiwa kufanyika Januari 22 mpaka 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Michuano hiyo ambayo inazishirikisha timu nane, nne kutoka Tanzania na nne za Kenya, itaonyeshwa mubashara na Chaneli ya Super Sport 9.
Timu shiriki kutoka Tanzania ni Simba, Yanga, Singida United na Mbao FC, huku zile za Kenya zikiwa ni Gor Mahia, AFC Leopards, Bandari na Kariobangi Sharks.
Mkurugenzi Mtendaji wa Multichoice Tanzania, Jacqueline Woiso, amesema huu ni muda muafaka kwa wateja wao kupata burudani ya michuano hiyo kupitia Super Sport na si sehemu nyingine.
"Tunayo furaha kubwa kuutangazia umma kwamba hamu yao kubwa ya kuishuhudia michuano hii mubashara sasa imepata jibu kwani DStv kupitia chaneli yetu ya Super Sport 9 ambayo ipo kwenye vifurushi vyote kuanzia kile cha chini kabisa."
Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, amesema: "Tangu kuanzishwa kwa michuano hii miaka mitatu iliyopita, imekuwa ikipendwa sana, hivyo tumeamua kushirikiana na DStv kuwawezesha wapenzi wa soka kuishuhudia michuano hii kwa mapana zaidi.
"Niwaombe tu wawakilishi wetu kutoka Tanzania kuandaa vikosi vyao kamili ili waweze kulibakisha kombe hapa nyumbani na kupata fursa ya kucheza na Everton hapahapa. Hatutaki watufanyie uhuni wa kutuletea vikosi dhaifu.
"Michuano hii ina heshima kubwa na ipo kwenye Kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania, Shirikisho la Soka la Kenya na Shirikisho la Soka Afrika, hivyo lazima iheshimiwe." alisema.
Kwa upande wa zawadi, bingwa wa michuano hiyo mbali na kucheza na Everton, pia atazawadiwa dola 30,000 (Sh 68,930,100), mshindi wa pili dola 10,000 (Sh 22,976,700), watatu dola 7,500 (Sh 17,232,500), wanne dola 5,000 (Sh 11,488,300) na zote zilizotinga robo fainali zitazawadiwa dola 2,500 (Sh 5,744,170).
Huu ni msimu wa tatu kwa michuano hiyo kufanyika ambapo mara mbili bingwa ni Gor Mahia ambayo ilipata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Everton ya England.
0 COMMENTS:
Post a Comment