Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba itaendelea kuikosa huduma ya nahodha wao John Bocco katika michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems kuamua kumuweka nje kwa ajili ya kupata muda wa kupona majeraha yake.
Bocco yuko nje ya kikosi cha Simba kwa wiki kadhaa baada ya kuumia kifundo cha mguu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakati timu hiyo ilipocheza na JS Saoura katika Dimba la Taifa, hivi karibuni.
Mshambuliaji huyo aliikosa mechi ya pili ya Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita ambapo klabu yake ilifungwa mabao 5-0 nchini DR Congo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mratibu wa Simba, Abass Ally amesema kuwa Bocco hatakuwa sehemu ya wachezaji ambao watashiriki michuano hiyo ya SportPesa ambayo ilianza jana Jumanne katika Uwanja wa Taifa jijini Dar.
“Bocco yeye hatakuwa kati ya wachezaji wetu ambao watashiriki michuano hii ya SportPesa baada ya kuumia hivi karibuni. Kocha ameamua kumpumzisha kwa ajili ya kupata muda wa kupona majeraha yake.
“Mazoezi aliyoyafanya leo (juzi Jumatatu) yalikuwa maalum kwa sababu alikuwa anaenda kutengeneza tangazo la hao SportPesa, ila hatacheza michuano hii,” alisema Abbas.
Wakati huohuo, Daktari wa Simba, Yassin Gembe amelieleza Championi Jumatano, kuwa hali ya beki wa kulia wa timu hiyo, Shomary Kapombe inatia matumaini ambapo kwa sasa amebakisha muda mchache kabla ya kuanza mazoezi mepesi.
“Kapombe anaendelea vizuri kabisa kwa sasa, amebakisha muda mchache kabla ya kuanza mazoezi madogomadogo ambayo atafanya kwa wiki kadhaa kabla ya kurudi rasmi uwanjani.
“Kuhusiana na Erasto Nyoni yeye tulisema atakaa kwa wiki tatu nje, tayari ameshamaliza wiki mbili bado moja ambayo akimaliza ataanza naye mazoezi mepesi kisha atajumuika na wenzake kwa ajili ya kurudi rasmi,” alisema Gembe.
Pia taarifa ya Simba imesema kuwa beki wake Asante Kwasi naye atakosa michuano hiyo kutokana na kwenda kwao Ghana kumuuguza mama yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment