February 12, 2019





NA SALEH ALLY
UKIPATA nafasi ya kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kwa hapa nyumbani hasa inayojihusisha na michezo na hasa mchezo wa soka, utaona ishu ni Haji Sunday Manara.

Manara ni msemaji wa Simba, kijana wa Kitanzania mwenye maneno mengi kama ilivyo asili ya watu wa Pwani au Ufukwe wa Bahari ya Hindi. Hiyo ni jadi yao na imezoeleka, tofauti na wanaotokea Bara.

Msemaji huyo wa Simba amejichukulia umaarufu mkubwa, hii inatokana na ukubwa wa Simba lakini zaidi ni zile kauli zake za "shombo" dhidi ya watani wao Yanga. 

Kawaida, furaha na faraja ya watani hao wa jadi huwa ni kuuona upande mwingine ukitaabika au hauna furaha. Sijaelewa hii inaingiaje kwenye utani lakini inaonekana kuwa kwenye kipande cha jadi.

Gumzo nililoanza kulielezea ni kuhusiana na taarifa zilizotolewa awali kwamba Manara amepoteza kibarua chake na hasa baada ya mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mechi yao ya kesho dhidi ya Al Ahly.

Wengi waliamini kama ilivyo kawaida, Manara angezungumza akiwa ameweka mbwembe zake za kutosha kuhusiana na mechi hiyo. Mambo yakawa tofauti, safari hii ikawa ni Mo Dewji ambaye pamoja na kuhamasisha watu kujitokeza uwanjani pia alitaja hadi viingilio.

Baada ya hapo ikawa Manara hana kibarua na kadhalika. Huenda wengine wangefurahia kusikia hilo linakuwa sahihi lakini baadaye baadhi ya vingozi wa Simba walijitokeza na kutoa maelezo wakiweka msisitizo sivyo inavyozungumzwa.

Pamoja na hivyo, inaonekana mjadala umeendelea na zaidi hadi wale mashabiki wa Simba nao wamekuwa wakilizungumzia suala hilo wakijaribu kuchimba hapa na pale na kadhalika.



Wako wameeleza kwamba siku ya mkutano huo uliofanyika kwenye ofisi za Dewji, Manara alifika pale lakini akatakiwa kuondoka na ndio chanzo cha mjadala huo. Haya yote yanaweza kuwa yalitokea au la lakini umuhimu wake kwa kipindi hiki ni kipi hasa.

Simba wana mengi ya kufanya na hasa umuhimu wa mechi ya kesho. Wanawavaa Al Ahly kutoka Misri, hawa ni vigogo wa Afrika na tayari wameonyesha hilo baada ya kuwafunga Simba kwa mabao 5-0 nchini Misri. Je, Simba wamjadili Manara au wajipange na hili?

Simba wamejisahau, hawajui ugumu wa kinachowakabili mbele yao kesho! Au wako wanaosubiri mambo yaharibike kwa kuwa wana nafasi ya kulaumu basi waseme kwa kuweka msisitizo kwenye lawama zao.

Manara si muhimu kwa Simba ambayo inaliwakilisha taifa na Afrika Mashariki yote. Kikubwa ni maandalizi ya mechi hiyo muhimu na wanapaswa kujadili mambo kadhaa muhimu yanayoihusu mechi hiyo.

Yako yatafanywa na uongozi, lakini muda wanaotumia mashabiki hao kumjadili Manara, basi wangeutumia namna ya kuandaa vikundi vya ushangiliaji, namna ya kuingia uwanjani kwa wakati, jinsi ya kuungana na kushangilia na kadhalika ili kuwa sehemu ya mchezaji namba 12 atakayeisaidia timu hiyo kesho.

Kawaida ushindi unahitaji mikakati, ushindi hauwezi kusimamiwa na uongozi, makocha na wachezaji pekee. Ili Simba ifanye vizuri lazima kuwe na muunganiko wa pamoja.

Muunganiko huo utajenga kitu kimoja ambacho kitaifanya Simba kuwa kitu kimoja chenye lengo moja kuhakikisha wanamuangusha Golliath. Itawezekana kukiwa na umoja huo.

Manara hatakaa Simba milele, siku moja ataondoka akiwa anapenda au la. Hivyo jambo lake hasa kulizungumza linaweza kuwa na umuhimu zaidi baadaye kwa Simba na si sasa.

Vizuri Wanasimba mkautumia muda wenu vizuri kwa kuhamasisha, kukumbusha, kutahadharisha na kuungana kwa ajili ya kutoa nguvu au kuongeza nguvu katika kikosi chenu na kutafuta makosa ili kumtwika mtu.



2 COMMENTS:

  1. Manara n muhimu kuliko hata baaadhi ya wachezaji mfano kuna haja gani ya kuwa na mchezaji kama zana na tukamlipia kodi wakati hana faida kwenye timu manara brings motivation to all simba followers tutakosa ladha ya simba bila manara

    ReplyDelete
  2. Vipi utamtaja Manara bila ya kuitaja Simba na vipi utaitaja Simba na kumsahau Manara ambaye ni kipenzi wa hata wale wasiompenda

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic