SEHEMU tatu kwa sasa ndizo zimegawanya Ligi Kuu Bara ambayo moto wake sio wa kitoto kila mmoja anapambana kwa uwezo wake kufikia malengo.
Mgawanyo wa kwanza unaanzia kwenye timu ambazo hesabu zao kubwa ni kuona zinabeba kombe la Ligi Kuu Bara, kundi hili nguvu kubwa wameweka kwenye kushinda mechi zao zote ili wafikie lengo lao.
Pili ni kundi ambalo linapigia hesabu kuwa kwenye nafasi tano za juu msimu huu kulingana na vile ambavyo wamejitathimini na kuamua kupambana kwa hali na mali kufikia lengo mwisho wa msimu.
Tatu ni wale ambao wapo nafasi mbili za mwisho hawa wanapambana kujitoa pale walipo mchana hata usiku ili wajinasue kwenye nafasi hizi ambazo hatari yake ni kushuka daraja msimu unapokamilika.
Kuna ushindani fulani hivi ambao upo msimu huu tofauti na msimu uliopita hali ambayo inaleta ladha ya kipekee kwenye mbio za kumtafuta bingwa wa ligi.
Imani yangu ni kwamba kila timu imejipanga sawasawa kuona inashinda mechi zake kuanzia zile za nyumbani na ugenini hapo ndipo utamu unazidi kunoga kila timu inaposhuka uwanjani.
Kama ligi ingekuwa na mdhamini naamini ushindani ungekuwa ni mkubwa maradufu zaidi ya sasa, kwani ipo wazi timu nyingi zinajiendesha kwa kuungaunga bila uhakika wa kesho ila zinasonga na zinapata matokeo.
Kila timu inaonyesha ari na ushindani mkubwa bila kujali inacheza na nani ama ni wakati gani inapitia hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika kitu ambacho wanapaswa wakitazame msimu ujao ni mdhamini mkuu atakayeokoa jahazi ndani ya ligi.
Timu nyingi zina uwezo wa kutafuta matokeo ila zinakwamishwa na kitu kinaitwa Uwanja wa kuchezea, hili lipo wazi na linaumiza kwa benchi la ufundi pamoja na wachezaji kupoteza mchezo kisa uwanja sio rafiki hili nalo TFF lisisahau.
Kwa mfano Uwanja wa Sokoine uliopo Mbeya umekuwa ukilalamikiwa na timu nyingi zinapopoteza matokeo timu kama Mtibwa Sugar, Mbao FC na Stand United ni miongoni mwa timu ambazo hazikufanya vizuri na ukiangalia sababu ya kiufundi inasababishwa na uwanja.
Wahusika wa masuala haya ikiwa ni pamoja na TFF iangalie namna bora itakayosaidia kuwa na viwanja safi ambavyo vitatupatia matokeo bora, hali ni mbaya kwenye viwanja ambavyo wachezaji wanachezea.
Uwanja ukiwa mbovu inakuwa ngumu kupata matokeo mazuri kwa timu pamoja na mashabiki kupata ile burudani ambayo wanaistahili kutoka kwa timu zao zinapokuwa kwenye uwanja akiwa na hofu ya kuumia ama kupoteza mpira hali inayomfanya asiwe sawa.
Kuna baadhi ya viwanja ambavyo kila mmoja anapata burudani ya kweli kuanzia wachezaji na mashabiki wenyewe wanaona kile ambacho wanastahili kutoka kwa timu zao na hata matokeo yanayopatikana yanakuwa chanya.
Mfano uwanja ule wa Nyamagana ambao ni wa nyasi bandia, CCM Kirumba, Samora hivi viwanja ni bora na vinastahili kuchezea ligi na kuwapa ladha mashabiki pamoja na wachezaji kucheza kwa umakini.
Kwenye uwanja bora mchezaji anafanya alichoagizwa na mwalimu bila hofu, fursa kubwa ya kutoa burudani kwa mashabiki ambao wamefika kuwaona wachezaji wakiwa kwenye majukumu yao hata wale ambao wanatazama kupitia Azam TV nao wanapata raha.
Wahusika hasa kwa msimu ujao itakuwa bora wakiweka mkazo kwenye viwanja, kila timu ina nafasi ya kuwa na kiwanja bora kwa mipango bora ambayo itakuwa na manufaa kwa timu pamoja na taifa kwa ujumla.
Mpango huo uwe ni kwa kwa kila timu inayoshiriki ligi kuwekeza kwenye viwanja bora na sio bora viwanja kwa ajili ya kuchezea na hilo linawekezekana endapo kutakuwa na nia itasaidia kukuza uwezo wa wachezaji.
Ifike mahali kuwe na msimamo na utaratibu kwamba kiwanja kikiwa kibovu kisitumiwe kwenye michezo ya ligi, maana hadhi ya ligi ni kubwa tofauti na mashindano mengine ya mchangani yanayofanywa.
Burudani inakosekana kwa mashabiki na kuondoa ile ladha ya Premier inakuwa kama vile mashindano ya mabonanza tu kwa muda ilihali ni mashindano yanayompata mwakilishi wa nchi kimataifa hili si sawa.
Mashabiki wengi pia ambao wapo nje ya nchi wanashindwa kufurahia, nimekuwa nikipata malalamiko mengi kutoka kwao hasa ambao nafahamiana nao mara kwa mara wamekuwa wakihoji ligi yenu hiyo namna gani tena?
Wanashangwaza na Viwanja ambavyo tunatumia havilingani na hatua ambayo tunaifikiria kwenda pamoja na kukua kwa sayansi jinsi kunavyoleta mabadiliko nasi pia ni wakati wetu kubadilika na kuleta mapinduzi ya kweli.
Wengi kutoka nje wanafuatilia ligi kupitia Azam TV sasa kama itaendelea hivi hasa la viwanja vibovu linatia aibu na doa kubwa kwa taifa, ili mshindi apatikane ni lazima kusiwe na sababu kwa timu nyingine miongoni mwa sababu ni ubovu wa viwanja, lifanyiwe kazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment