JINAMIZI HILI LA RATIBA LINAUA SOKA LA TANZANIA
TUNAPOIZUNGUMZIA Ligi Kuu Bara, basi tunaizungumzia ligi ya levo za juu kabisa katika soka la Tanzania Bara na bingwa ndiye anaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hakuna asiyefahamu ukubwa wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa Afrika michuano hiyo ndiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu.
Sasa inapotokea kwenye Ligi Kuu Bara kuna vitu haviendi sawa, lazima tuzungumze ili wahusika kama ni waelewa, basi watayafanyia kazi hayo mapungufu yaliyopo.
Kwa misimu mingi, jambo hili la timu kuwa na viporo vingi limezungumzwa, lakini kwa msimu huu limezungumzwa zaidi kutokana kuonekana kwamba wahusika kama vile hawaelewi watu wanazungumza nini.
Tazama hivi sasa msimamo wa Ligi Kuu, vinara Yanga na wanaofuatia, Azam FC, wote wamecheza mechi 25, bado mechi 13 wamalize msimu, lakini Simba wanaoshika nafasi ya tatu, wenyewe wamecheza mechi 19, wana mechi 19 ili wamalize msimu.
Achana na hao. Kuna timu kama Lipuli, Ruvu Shooting, Alliance, Stand United na Mwadui, zina mechi 10 tu mkononi ili kumaliza msimu. Hapo hakuna usawa hata kidogo.
Ili kuondoa dhana hii, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) mnapaswa kukaa chini na kuhakikisha msimu ujao hili halijitokezi tena.
Msimu huu tukubali kwamba mmeshindwa kulisimamia hilo kwa sababu misimu yote inafahamika wazi kwamba huwa kuna mashindano mbalimbali tena mengi yapo kwenye Kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Msimu ujao hatutaki hili lijirudie, kabla ya kupanga ratiba yenu ya msimu, itazameni kwa kina Kalenda ya Caf na Fifa. Hapo mtakuwa mmetibu huu ugonjwa, vinginevyo hakutakuwa na jipya.
KUTOKA BODI YA UHARIRI, CHAMPIONI
Wanajua wanachofanya
ReplyDeleteHawana utaalam wa kupanga ratiba..... Na hawataki kulikubali hilo. Watafute wataalam na wajuzi wa kupanga ratiba kwa kutumia "App" maalum....
ReplyDelete