March 1, 2019


Na Saleh Ally

HABARI za asubuhi Ruge,

Nilitamani nisingeandika chochote kuhusiana na wewe lakini nimeshindwa rafiki yangu, historia inanibana kuumiza moyo wangu. Nimeumia sana kwa kuwa muda mchache baada ya kuondoka nimeshuhudia mengi sana kuliko nilivyotarajia.

Kilichokuwa kikinizuia kuandika ni maneno yako, siku ile usiku, nakumbuka ni kama miaka 15 iliyopita au zaidi tukiwa katika studio za Master Jay pale Masaki. Kama unakumbuka tulikuwa mimi, wewe, Marlon Rinje na msanii Mr Paul. 

Mr Paul alikuwa ndio amemaliza kurekodi ule Wimbo wa Zuwena, baada ya wazo na uamuzi wako wa kumfuata mtoto wa marehemu Marijani Rajab kuingia naye makubaliano ili Mr Paul aurudie wimbo huo katika mfumo wa kisasa.

Baada ya kuusikiliza na tukakubaliana hakukuwa na marekebisho tena, uliingia katika mashairi ya wimbo huo na kukumbushia namna binadamu hupenda kuwasifia wale waliotangulia mbele ya haki badala ya pale wanapokuwa hai.

Kuna kale ka msemo "Ishi ulaumiwe, kufa usifiwe", tangu umeondoka hiki ndicho kinachoendelea lakini nilitaka kukueleza, hakika asilimia zaidi ya 85 ya watu, wanakupa sifa zinazostahili na ilikuwa ni vigumu sana wasifanye hivyo.

Hawakuwa na ujanja, hawakuwa na njia ya kulikwepa hili na ilikuwa lazima wafanye hivyo. Ulichokisema wakati huo ni sahihi, lakini kinachofanyika sasa, kinadhihirisha uanadamu wetu.

Kama utaweza angalau ungerudi kidogo, hata dakika chache uone yanayoendelea katika dunia hii. Hata wale waliokulaumu sana, leo wamekuwa waungwana na wanaendelea kukupa sifa zako ambazo ninaamini, wengi hawakufahamu vizuri hawakuwahi kujua ulichokifanya kwa taifa hili.

Nakumbuka siku moja uliwahi kunikataza kusema maneno haya wakati tukiwa tumeenda Tanzania House of Talent (THT) kwa mara ya kwanza kabisa wakiwa ndio wasanii wameanza kuja. 

Ukiwa umebeba maji mkononi, uliniambia: "Hawa wasanii leo wanaonekana hawana lolote, lakini niamini watakuja kuwa watu wakubwa sana ingawa ninaamini kati yao, kuna siku watalalamika mimi nimewashusha au kuwabania."

Nilitabasamu na kusema ni mambo yaliyozoeleka na mwisho tulianza kugawa maji. Hili wazo la THT ni lako pia na limezalisha idadi ya wasanii lukuki ambao leo wana maisha yao na mimi ninaamini wako ambao kama wasingekuwa kwenye muziki baada ya kuwaona na kuwapigania, leo wasingekuwa hapo na huenda wangekuwa wakifanya kazi za kiwango cha chini sana.

Nilizizoea lawama dhidi yako, wengi waliozibeba walikuwa ni wale wasiojua lolote kama wakati ule kipindi cha ile albamu ya Ant Virus, mwisho wakaishia kuomba msamaha kwa kuwa hawakujua mwendo sahihi wa vita ambayo waliivaa.

Nimeona sifa nyingi sana za Ruge, hali iliyonifanya nimkumbuke kwa kuwa nimekuwa na bahati ya kufanya naye kazi kwa miaka tisa katika tasnia ya muziki na nilijifunza mambo mengi sana.

Ruge rafiki yangu zaidi ya miaka 18, sijawahi kujua utajiri wako kimaisha zaidi ya utajiri wa kusaidia watu walioishia kukulaumu na hadi sasa wakiwemo wendawazimu wameendelea kukulaumu.

Kama unakumbuka, wakati kinaanzishwa kipindi cha michezo cha Clouds FC, bosi akiwa Ephraim Kibonde na 'vidampa' mimi na George Njogopa, ulimuasa Njogopa kwamba redio ni hatari, inakuza umaarufu haraka na anapaswa kuwa na nidhamu kubwa.

Watu wengi waligombana nawe sababu ya nidhamu ya kazi kwa kuwa ulikuwa na moyo wa simba, ukitaka kushinda kila jambo.

Wakati wanaanza, walianza pamoja nawe lakini walipofanikiwa wakajisahau kabisa na kuanza mwendo wa pole, mwisho ukaamua kufanya kazi na mtu mwingine, alipopata umaarufu yule mwenye nidhamu mbovu alianza kulalama.

Nimekukumbuka sana ulivyokuwa tayari kusuluhishwa kila kunapotokea tatizo. Nakumbuka uliniita nimshauri rafiki yangu Sugu ili mpatane, ukanieleza kutokuwa na faida ya ugomvi kwa kuwa nilikueleza hoja zake ambazo hakika tuliziona na msingi.

Mara nyingi, nimeshirikiana na wewe na tofauti kadhaa ukitaka tuzimalize zikiwemo tofauti zako na bosi wangu Eric Shigongo. Mazungumzo yako ya mwisho na mimi ilikuwa ni wewe kumalizana na Shigongo baada ya kuwa mmekutana mjini Mwanza katika msiba wa dada wa Rais John Pombe Magufuli na ukasema, mmekubaliana Global Group na Clouds Media kufanya kazi kwa pamoja bila ya tofauti kama ambavyo tuliwahi kufanya.

Ukanialika kufika ofisini ili unikabidhi mtu lakini ikawa bahati mbaya sikuwahi kukuona tena.

Nimeona January Makamba akieleza ulivyopambana hadi kupewa jina la Fighter. Nimeshangazwa sana kuona unapambana hadi ukiwa kitandani. 

Najua ulitamani kurudi kwa kuwa ulijua watu wengi sana wako nyuma yako na wataanguka au kuonewa usiporejea.

Hakuna anayeweza kumuonea Profesa Mutahaba, lakini vijana wengi wa Kitanzania ndio waliokufanya utamani kurejea. Haikuwa  hivyo kwa kuwa Mwenyezi Mungu ana mipango yake na kamwe haijawahi kuwa na makosa.

Sina uwezo wa kumuomba urudi, lakini nilitamani urudi kidogo tu. Uwaone eti kuna wasanii, mameneja wao au viongozi wao wamesusa hata kusema pole au kusikitishwa na kifo chako. 

Wakati ukiwa hai walikuwa marafiki zako na ndani ya maendeleo yao, kuna "matofali" ya akili zako kuwafikisha hapo walipo.

Nimegundua ni watu wasio na busara na kama unakumbuka wakati fulani wakiwa na tofauti dhidi yetu tulipokutana ofisini kwako mwaka jana, nilikueleza kwamba kiongozi wao mmoja hana busara na ni mtu wa kukurupuka.

Hicho ndicho alichokifanya yeye na timu yake baada ya wewe kuondoka lakini ninajua Mungu atawalipa hapa duniani.

Ruge nakujua kwa mengi sana namna ulivyonituma kumfuata Bi Kidude Zanzibar ili wimbo wake uimbwe kisasa na baadaye Lady Jaydee akaurudia Muhogo wa Jang'ombe. 

Namba Njiwa ya Patricia Hilary iliyobadilishwa kwa mawazo yako, namna muziki wa dansi ulivyotengeneza matamasha na ushindani wa Msondo Ngoma na Sikinde Ngoma ya Ukae.

Sijui ulikuwa na akili kilo ngapi rafiki yangu Ruge, maana katika michezo na hasa soka na ngumi, ulikuwa na mchango mkubwa kutumia akili hizo na kamwe sikuwahi kuona ufahari wa utajiri zaidi ya mafanikio ambayo mengi yalikwenda kwa watu wakiwemo wale walioishia kukulaumu tu.

Hakuna aliye mkamilifu, ninaamini makosa yako ni machache mara mia ya mazuri uliyofanya. Natamani urudi kidogo Ruge ili ukiondoka uende na funzo la dunia hii licha ya kwamba ulishaona kabla ya kuondoka.

Najua kila mmoja ana mwisho wake, wako umekuwa wakati unahitajiwa na wengi sana. Sina chochote cha kuongeza au kulalamika badala yake namshukuru Mungu kwa kuwa bila yeye nisingekujua na kujifunza. 

Wamekuita mtafuta njia, mimi nakuita ni "Simba wa Vita" kwa kuwa ulikuwa Brigedia uliyeongoza mapambano kwa ajili ya maisha ya watu wakati yako yakibaki vilevile.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic