SIMBA NA TUYISENGE SASA MAMBO SAFI
SIPATI picha Simba itakuwaje. Kwa muziki huu wa sasahivi tu Haji Manara anakwambia Uwanja wa Taifa hata ikija Barcelona ile yenyewe, Taifa inaacha pointi tatu. Itakuwaje akiongezeka na mtu mmoja hatari sana Jacques Tuyisenge. Huyu aliifunga Everton tena ile yenyewe ndani ya Taifa.
Huyo straika ndiye yule pacha aliyekuwa anatisha na Meddie Kagere pale Gor Mahia na yeye ni Mnyarwanda pia kama Meddie. Championi Jumamosi limejiridhisha kwamba Tuyisenge amewaambia viongozi wa Simba kwamba amemmisi Kagere hivyo wakamilishe mipango atue Msimbazi.
Huyu Tuyisenge ndiyo mashine ya mabao iliyobaki pale Gor Mahia kwa sasa, ametupia nje ndani mpaka timu hiyo ikatinga hatua ya makundi ya Shirikisho juzijuzi na sasa ipo robo fainali. Muda wote kuanzia mwezi ujao unaweza kuwasha WhatsApp yako au Instagram ukakutana na posti ya Manara; “Tumemsainisha.
”Mwekezaji bilionea, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ aliwahi kusema anataka Simba iwe moja kati ya klabu kubwa Afrika na iheshimike na hilo limeanza kutimia.
Katika kuhakikisha timu hiyo inakuwa vizuri zaidi msimu ujao, uongozi wa Simba uko kwenye mipango ya kimyakimya ya kuboresha kikosi chake huku jina la mshambuliaji wa Gor Mahia, Tuyisenge likitajwa na yeye mwenyewe kuonyesha nia ya kuwa tayari kutua Msimbazi.
Chanzo kutoka ndani ya Simba kinasema, Tuyisenge ambaye anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kucheka na nyavu yupo tayari kujiunga na mabingwa hao wa ligi kuu msimu ujao ili aweze kucheza sambamba na pacha wake, Meddie Kagere ambaye aliwika naye Gor Mahia.
Tuyisenge amekuwa mchezaji tegemeo ndani ya Gor Mahia kwani mabao yake manne aliyofunga kwenye michuano ya kimataifa msimu huu yameifanya timu yake kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho.
Hivyo kutokana na kasi hiyo, Simba imepanga kumsajili staa huyo kwa ajili ya msimu ujao ambapo pia wamepanga kufanya usajili kwa mfumo wa kisasa zaidi.
“Tuyisenge ameonyesha nia ya kuja kuichezea Simba, ni mchezaji mzuri ambaye anafaa kucheza timu yoyote kubwa.
Anataka kuja kucheza na pacha wake Kagere ambaye alikuwa Gor Mahia. “Kwa sasa viongozi wako bize mawazo yote yapo kwenye mechji yetu ya kimataifa. Lakini suala la usajili litafanyika kwa umakini mkubwa na mfumo wake utakuwa wa kisasa,” kilisema chanzo hicho.
Hivi karibuni wakala wa Tuyisenge, Patrick Gakumba aliliambia Championi Jumamosi kuwa anataka kuona Tuyisenge akicheza na pacha wake Kagere pale Simba.
Tuyisenge alifunga bao pekee katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Everton kwenye mechi ya kirafiki iliyoandaliwa na SportPesa Uwanja wa Taifa jijini Dar. Mabao ya Everton yalifungwa na Wayne Rooney pamoja na Kieran Dowell.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment