KIPA BANDARI KENYA ATUMA AHADI YANGA
KIPA wa timu ya Bandari ya Kenya, Farouk Shikalo ‘Waza’ amekiri kufanya maongezi na viongozi wa Yanga juu ya kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.
Kipa huyo ambaye yupo katika timu ya taifa ya Kenya, amesema anakuja Tanzania kufanya kazi huku akifunguka namna anavyoufahamu uwezo wa mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere.
Shikalo ni miongoni mwa wachezaji wa Kenya walioitwa katika kikosi cha awali cha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) inayotarajiwa kufanyika nchini Misri, Juni, mwaka huu.
Shikalo alisema ni kweli amefanya maongezi ya kujiunga na Yanga, lakini bado hajafi kia mwisho kutokana na masharti anayotaka atimiziwe kwenye mkataba kabla ya kutua nchini.
“Ni kweli Yanga nimezungumza nao, tena ni viongozi wa juu ndiyo nimekuwa nikiwasiliana nao mara kwa mara kwa ajili ya kutaka nije nicheze katika timu yao msimu ujao, binafsi kwangu litakuwa ni jambo kubwa maana ukiangalia ni kipindi sasa hakuna Mkenya anayecheza ligi ya huko.
“Lakini bado hatujafi kia makubaliano ya moja kwa moja kwa sababu kuna mambo nimewaeleza yawe katika mkataba wangu, naamini nakuja kufanya kazi Yanga mambo yakienda vizuri tuombe Mungu tu.
“Najua Simba watakuwa ni wapinzani wetu wakubwa katika ligi, hilo halinipi hofu kwa kuwa nawajua wachezaji wake kama Kagere Meddie ambaye ametoka huku, kikubwa ni kujipanga na kupambana,” alisema Shikalo.
Kipa huyo aliongeza kwa kusema licha ya kuzungumza na viongozi wa timu hiyo lakini bado hajaambiwa chochote na kocha wake, Benard Mwalala kwa kuwa anasubiria mipango ya usajili wake ikamilike ndiyo ataweza kukaa kuzungumza naye.
0 COMMENTS:
Post a Comment