May 4, 2019


LIGI kuu Bara sasa inaelekea ukingoni kutokana na timu nyingi kukamilisha nusu ya michezo yao ambayo walitakiwa kucheza huku timu nyingine zikikamilisha vile viporo vyao ambavyo ni lazima viishe.
Hamna namna ushindani ambao tunauona ni mkubwa licha ya kilio cha timu nyingi kushindwa kumudu gharama za uendeshaji wa timu kutokana na ukata ambao haufichiki ila zinapambana kupata matokeo.
Kwa nyakati hizi za lala salama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halipaswi kulala wala kuzembea hata kidogo kwani mbinu chafu zinatumika ili kupata matokeo kwa timu zinazocheza.
Ipo hivi kwa sasa kila timu imeshapiga hesabu zake na kuona kile ambacho inastahili kukivuna baada ya kuvuna kwenye michezo yao iliyopita ambayo wamecheza.
Tunaona kila mmoja anapambana na hali yake hilo ndilo linahitajika cha msingi ni kujua ni kwa namna gani inapambana ili kupata matokeo uwanjani?
Kwa sasa TFF hampaswi kulala ule moto wenu ambao mlishtua kidogo kwa waamuzi wa mchezo kati ya KMC na Simba usizimwe ghafla.
Kwa kitendo ambacho kimefanyika nawapa heko TFF hasa kwa kutoa maamuzi haraka na yenye kuridhisha licha ya pointi kubaki mikononi mwa Simba ila kuna kitu waamuzi watakuwa wamejifunza.
Maana halisi ya uongozi ni kutoa maamuzi na kusimamia kile ambacho kina maslahi kwa wengine na kwa muda sahihi hali kama ile ikiendelea italeta heshima na nidhamu.Waamuzi wengi wamekuwa wakijisahau na kutoa maamuzi ambayo hayana msingi.
Pia dharau zimekuwa nyingi kwa kuwa hakuna ambaye anajali hivyo kwa kuanza mmejitahidi itawafanya wengine kuhofia kufanya maamuzi ambayo hayatazingatia sheria 17 za mpira.
Waamuzi wamekuwa wanafanya maamuzi yao kwa kuwa hakuna aliyekuwa anawafuatilia na hata kama wanafuatilia basi walikuwa wanachelewa kutoa maamuzi hali iliyokuwa inaongeza kiburi.
Timu nyingi zinacheza mechi ambazo hazirushwi na Azam TV hili ni baya kutokana na rekodi zao kuwa mbaya pindi wanapochezesha mechi za aina hii na ushahidi kukosekana hasa kwa wale ambao wataamua kutoa malalamiko yao.
Hivyo rai yangu kwa TFF kuwa macho muda wote kwenye mechi hizi ambazo kila mmoja anapigania timu yake ipate matokeo bila kujali anacheza na nani na katika wakati gani hilo hajui zaidi ya kutazama matokeo chanya kwakwe.
Mechi za ugenini kwa sasa zinakuwa ngumu kwa timu zote kutokana na kuwepo kwa kampeni ya kila timu ishinde mechi zake za nyumbani hili ni gumu na baya kwenye soka letu kwani halileti ushindani bali linazalisha chuki.
Hakuna ambaye anapenda kupata matokeo mabaya kwenye michezo yake ya mwisho hali inayofanya wengi kulazimisha mambo ambayo wanayatarajia kutokea hili halijakaa sawa.
Kwa mechi ambazo hazitarushwa moja kwa moja wapelekwe waamuzi maalumu ambao watakuwa wanakusanya ripoti na kutoa taarifa kwa wakati na sio baada ya muda kupita italeta mvurugano kwenye ligi na kupoteza ladha ya ushindani.
Ili kuepukana na maamuzi haya TFF ni lazima iwafuatilie waamuzi kwa ukaribu hatua kwa hatua na kutoa maamuzi hapohapo na sio kuwafungia macho wanaua soka letu kwa mapenzi yao binafsi.
Sheria 17 lazima zifuatiliwe na viongozi wa timu wanapaswa wakomae kwenye maandalizi na sio kutaka kushinda nje ya uwanja hili halipo sawa ndio maana tunapata timu ambazo zinashindwa kufika mbali.
Ukubwa wa Ligi Kuu Bara unatakiwa uthaminiwe na kila mmoja ambaye ana timu bila kujali aina ya timu aliyonayo na ile ambayo anacheza nayo itakuwa ajabu kupata matokeo ya mezani.
Naona kuna timu ambazo zinajitetea kushuka daraja ila zinatakiwa zitumie mbinu bora ya kushinda mechi na sio kutengeneza hujuma kwa kanda ama mikoa ambayo ina timu ambazo hali yake sio nzuri.
Kila mkoa kwa sasa naona kumekuwa na kampeni ya kutaka kuona timu zao zinashinda michezo yao yote hii ni mbaya na inaua ushindani waziwazi waache timu zishinde kwa kupambana.
Kama kuna timu ambayo inapanga matokeo kwa njia zake za ujanjaujanja ikikibainika inatakiwa ichukuliwe adhabu kali na iwe mfano kwa timu nyingine zenye tabia kama hiyo ziache mara moja.
Tunataka bingwa apatikane kwa uhalali na sio kuungaunga mpaka apatikane italeta dosari kwenye soka letu hasa wakati wa mashindano ya kimataifa.
Kwa timu itakayoshuka daraja tunatarajia kuona inashuka ikiwa kweli imeshindwa yenyewe kihalali na sio kwa kuonewa italeta matatizo.
Uzuri ni kwamba mchezo wa mpira ni mchezo wa wazi hivyo hakuna ambaye anaweza kudanganya kwamba alishindwa kupata matokeo chanya uwanjani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic