May 4, 2019


KUPOTEZA kwa nafasi ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 kushiriki michuano ya Afcon bado inabidi itushtue kutoka kwenye usingizi ambao tumelala kwa muda hasa kwenye kutafuta mafanikio ya Soka ambayo tunayaota siku zote.
Muda hautusubiri sisi bali unazidi kusonga mbele huku mafanikio nayo yakitushangaa namna tunavyozidi kudumaa kila iitwapo leo inashangaza na inafurahisha pia kwa kuwa tunachezea bahati pasipo kujua kwamba ni bahati.
Hebu fikiria timu kama Angola ambayo mara ya kwanza tulipokutana nayo kwenye michuano tofauti tuliifunga na kombe tukabeba sasa sijui tunakwama wapi kama sio uzembe ama kuchukulia kila kitu kawaida ilihali ni kizito.
Tunatia huruma na Shirikisho letu la Soka Tanzania (TFF) bado halijashtuka zaidi ya kuendelea kusema kwamba ni matokeo na sehemu ya mpira inashangaza kama tutaendelea kukubali matokeo tunayoyapata bila kuchukua hatua tutaendelea kuwashangaza wengi.
Tumeona namna wapinzani wetu waliojipanga wakibeba kombe nyumbani pamoja na zawadi wakisepa nazo huku wenyeji tukibaki kuwa watazamaji hii ni aibu kubwa licha ya kwamba kwenye soka kila kitu kinawezeka kutokea.
Vijana wetu wanashindwa kutumia nafasi ambazo wanazipata baada ya kulewa sifa na maelekezo ambayo wanapewa wanayapuuzia na kufanya kile ambacho wanakijua wao hili ndilo tatizo ambalo linapaswa litafutiwe dawa.
Pia kabla ya kuendelea kuacha mzigo wa lawama kwa TFF hebu tuzitazame na klabu zetu namna ambavyo zinawekeza kwa vijana ni kwa kiasi gani zinawakuza na kuwalea hasa ili kuwaongezea ujuzi licha ya kuwa na timu za vijana?
Ila bado TFF haiewezi kukwepa lawama kwa kuwa wao ndio walezi na wenye maamuzi kuhusu uendeshwaji wa timu zetu, hivyo kuna haja ya kuwa na mpangilio mzuri kwa timu zetu zinazoshiriki ligi kukuza vijana.
Uwepo wa mashindano ya vijana yatasaidia kupata timu imara ambayo itasiaidia kujenga taifa imara lenye ushindani pia kama kila timu itakuwa na timu za vijana hapo itakuwa  imepunguza ule ukame wa kutafuta vipaji maporini ilihali kila timu ina vijana wake.
Pia mpango mzuri wa TFF kama itaamua kuwekeza kupitia timu zetu na kufuatilia hasa kwenye timu za wakubwa kuona vijana wanapewa nafasi ya kuonyesha ule uwezo wao ili kupata uzoefu kwanza kwenye mashindano ya ndani.
Kitu pekee ambacho kwa sasa hakuna anayejua ni hatma ya vijana ambao wametoka kushiriki mashindano ya Afcon ukiuliza sasa walipo utapata majibu ambayo yatakulazimu uchukue panaldo upunguze maumivu kidogo kisha uendelee kusikiliza hoja.
Jambo lililopo ni kwamba vijana wetu tunawakusanya wakati wa mashindano kisha mashindano yakiisha kila mtu kwao mawasiliano yanakuwa kupitia simu na meseji na muda mwingine ni mpaka utokee mchezo ndio tunaanza kutafutana.
Hili janga kama likiendelea litatumaliza na kutufanya tubaki pale tulipo ama kama sio kushuhudia anguko kabisa kwenye soka letu la vijana pamoja na wakubwa kwa kuwa huku ndiko chimbuko linakoanzia.
Tazama mfumo wa timu zetu kubwa ulivyo, kwa timu zenye mafanikio zimejaza wageni wengi na wanapata nafasi kikosi cha kwanza huku wazawa wakisotea benchi hii inamaanisha kwamba ambao watakuwa bora ni wachache na watakaoonekana ni wachache kwa kuwa wengi hawafanyi kazi yao.
Ila kama kukiwa na ufuatiliaji na uwekezaji mkubwa tutapata matokeo chanya ambayo tunayafikiria hapo baadaye na sio haraka kama tunavyofikiria kwenye soka.
Hebu tujikumbushe baada ya kuondolewa Serengeti kwenye michuano ya Afcon hatua ya nusu fainali walicheza Nigeria na Angola, mshindi  wa pili alikuwa ni Angola hapo kumbuka Nigeria alimfunga Tanzania mabao 5-4 na Angola alimfunga Tanzania mabao 4-2 inamaana uwezo wa Angola umekuwa mkubwa wa kwetu ukadumaa.
Tukimaliza mshindi wa kwanza Cameroon huyu alishinda kwa penalti 5-3 dhidi ya Guinea timu zote zilizotinga fainali zimetoka kundi B hivyo kundi letu lilikuwa jepesi lakini sisi tumeboronga na kupigwa mechi zote tatu kisha tunarejea benchi kuwatamaza wenzetu.
Kuna kitu cha kujifunza hasa uwekezaji kwa wenzetu ambao wamefanikiwa ni wakati sahihi kwetu kuzinduka na kuweka akili zetu kwenye mpango kazi na kuboresha maandalizi ya timu zetu za vijana.
Vituo vya watoto vinasaidia kukuza vipaji vyao pia na walimu wenye uzoefu watasaidai kuibua vipaji halisi na kuwafanya vijana wawe na nguvu ya kushindana kwenye michuano mikubwa ambayo tutashiriki.
Kama tutaendela kufanya yale yaliyozoeleka tutaendelea kupata matokeo ambayo tumeyazoea kila siku ya kutupa maumivu sisi wenyewe, mafanikio yapo mikononi mwetu endapo tutaamua kuyatumia makosa kama sehemu ya kujifunza na sio kulaumu.

2 COMMENTS:

  1. Usisahau kwamba always next time?

    ReplyDelete
  2. Huyu Ammy Ninje ambae ni mkurugenzi mkuu wa masuala ya ufundi ndani ya TFF tuliambiwa yakwamba maisha yake ya kazi karibu yote amekuwa kuifundisha soka la vijana uengereza na si kufundisha tu Bali Raisi wa TFF Karia kuna wakati alikuja juu kumkingia kifua baada ya kuboronga kwa aibu wakati akifundisha timu ya Taifa ya bara.Karia alimwagia sifa Ammy Ninje kwa kusema huyu jamaa ni fundi hasa katika masuala ya mpira kwani amefanya makubwa huko ulaya? Na licha ya kuonesha kiwango duni katika masuala ya soka TFF ikamzawadia Ammy Ninje nafasi nyeti kabisa ya ukurugenzi wa ufundi ndani ya TFF. Sina nia ya kumchakaza Ammy Ninje kwa personal attacks ila mkurugenzi wa ufundi wa masuala ya soka ambae kama inavyodaiwa kuwa ni mtaalam wa soka la vijana halafu tunakwenda kushika mkia kwenye mashindano ambayo yamefanyika kwenye ardhi yetu? Unajua tatizo kubwa la viongozi wa taasisi mbali mbali Tanzania ni Ulaini wa akili na mazoea ya kuishi kama bosi kazini. Boss ni mtu anaekaa ofisini na kutoa maagizo bila ya kufuatilia kwa karibu kujua uwezo wa watendaji wake.Na kiongozi au a leader ni mtu anaefanya kazi kwa kufuatilia kwa karibu watendaji wake kujua uwezo na mapungufu yao katika utendaji wao huku akiwaongoza kwa mfano. Haiwezekani watendaji wawe wanaendelea kufanya madudu lakini huoni hatua zozote zikichukuliwa juu yao halafu useme kuna kiongozi hapo? Kwa Dunia ya sasa tutachelewa sana.Hasa kama mtoa mada hapo juu alivyokwisha bainisha kuhusu suala la wakati. Unapozembea kumuwajibisha mzembe fulani kazini usidhani muda au wakati utazembea kutimiza wajibu wake wa kusonga mbele na kukuacha ukidumaa.Na bado nitarudi kunako siasa kwanini kama viongozi wa taasisi nyengine tunashindwa kufuata kwa vitendo anayoyafanya Magufuli? Magufuli alijua ana kipindi cha miaka mitano kuyafanya aliyotakiwa kuyafanya kama kiongozi na alijua kamwe muda hautakuwa rafiki kumsubiri kufanya anayoyataka kuyafanya kama hakuwa na ufikiri na maamuzi ya haraka kuwawajibisha au kuwaondosha bila ya mughali wale wote wasioendana na kasi yake. Maamuzi ya Magufuli yalitakikana zaidi ndani ya soka letu kuanzia nagazi ya kijiji hadi taifa. Lazima kuwepo na uwajibikaji wa viongozi wa mpira kwa ngazi zote ili kupata viongozi wenye uwezo wasiopatikana kwa rushwa au upendeleo kama kweli tunataka kuleta mabadiliko ya kweli ya mchezo wa mpira nchini .

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic