UONGOZI MPYA YANGA WATUMA SALAAM YA KUTISHA SIMBA, WAONYA
MWENYEKITI mpya wa Yanga, Dk Mshindo Msolla, amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo akisema: “Waacheni wapinzani wetu wachonge, lakini msimu ujao watatutambua.”
Uongozi wa timu hiyo tayari umeanza mikakati ya kuanza kuisuka Yanga mpya kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwa kusajili wachezaji wenye hadhi na viwango vya juu vya kuichezea timu hiyo.
Mabosi hao wapya chini ya Msolla na makamu wake, Frederick Mwakalebela juzi walifanya kikao kizito cha kwanza cha kamati ya utendaji ambacho kilishindwa kumalizika na kumalizikia jana Jumapili.
Msolla ambaye alishinda kwa kishindo, alisema msimu ujao wa ligi utakuwa wa furaha na shangwe kwa mashabiki wao kutokana na mikakati mizito waliyoipanga uongozi wake pamoja na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera.
Msolla alisema, lazima heshima ya Yanga irejee kwenye msimu ujao kwa kuhakikisha wanasajili kikosi imara kitakachoipa makombe mbalimbali, likiwemo la ligi.
Aliongeza kuwa, tayari wameanza mikakati hiyo ya kurejesha Yanga ya kimataifa baada ya wikiendi hii kufanya kikao cha kamati ya utendaji kwa siku mbili mfululizo Jumamosi na Jumapili.
“Huu ni msimu wa pili Yanga imeshindwa kusimama kwa maana ya kuwa kikosi imara na kusababisha kuukosa ubingwa wa ligi kwa mara ya pili mfululizo na kushindwa kucheza michuano ya kimataifa.
“Katika uongozi wangu sitaki litokee hilo, na kikubwa nilichopanga ni kukisuka kikosi kitakachokuwa imara na kuirejesha Yanga ile ya kimataifa iliyozoeleka.
“Tayari tumeanza mikakati hiyo kwa kukutana na kamati yangu yote ya utendaji kwa kufanya kikao maalum kwa ajili ya kuirejesha anga za kimataifa, uongozi mpya unafahamu machungu waliyonayo,” alisema Msolla.
Tangu uongozi mpya uingie madarakani, Yanga imepoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Lipuli kwenye Kombe la FA na Biashara katika ligi kuu, hivyo Msolla na timu yake wanajua kazi kubwa iliyo mbele yao.
0 COMMENTS:
Post a Comment