May 4, 2019


JAMBO pekee ambalo linasubiriwa kwa hamu kubwa zaidi kwa sasa kwenye soka ni uchaguzi wa Yanga ambao utafanyika kesho Jumapili.

Huu ni uchaguzi muhimu sana kwenye timu hiyo ambayo imepita kwenye kipindi kigumu sana kuanzia alipoachia ngazi aliyekuwa mwenyekiti wao, Yusuf Manji.

Tangu kuondoka kwa Manji, Yanga mambo mengi yalianza kuanguka na kila kitu kilikuwa kinaonekana kuwa hovyo na mwisho kila mmoja alianza kuachia ngazi, kuanzia makamu mwenyekiti.

Mwisho aliyekuwa anaonekana kuwa na roho ngumu sana Boniface Mkwasa, ambaye alikuwa katibu mkuu, naye uzalendo ukamshinda akaachia ngazi kutokana na ugonjwa.

Baada ya hapo, Yanga ilishindwa kuhimili na mwisho ikaanza kuaguka bila kuwa na kiongozi sahihi, kila mmoja alikuwa akikaa kwenye kiti cha uongozi anaachia ngazi baada ya muda mfupi.

Lakini ajabu ni kwamba kila ulipokuwa ukiitishwa uchaguzi zilitokea figisu za hapa na pale na wengine wakaenda mahakamani kuzuia uchaguzi huo kwa kile wanachodai kuwa wana mapenzi na Yanga, kumbe siyo kweli.

Uchaguzi huu sasa ni muhimu sana kwa Yanga kuliko kutwaa ubingwa wa ligi, Yanga kwa sasa wanahitaji uongozi thabiti ambao unaweza kuwatoa hapa walipo waende mbele.

Yanga inahitaji viongozi ambao watapiga marufuku bakuli jukwaani na siyo wale ambao watakuwa wanateua watu wa kutembeza bakuli hilo.

Yanga inahitaji viongozi ambao watatengeneza mhimili bora kwenye klabu hiyo, inahitaji kiongozi ambaye anaweza

kuwashawishi wadau wakawekeza kwenye timu hiyo na siyo bora kiongozi ambaye kila atakayesikia jina lake atakimbia.

Kiongozi wa juu atakayechaguliwa kesho kwenye timu hiyo ni yule ambaye anaweza kupenya kokote lakini ambaye anaaminika na anawezeza kuwa na ushawishi mkubwa hata kwa wachezaji wapya kwenye timu hiyo.

Ni uongo kwa sasa kama kuna ambaye atasema kuwa timu hiyo inahitaji kiongozi ambaye atawapa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hili haliwezi kuwa jambo la kampeni kwa kiongozi wa timu hiyo kwa kuwa hata kama haina uongozi bado inaweza kutwaa ubingwa huu.

Yanga haihitaji kiongozi ambaye atapeleka makundi ya kusema watu wangu ni hawa na hawa siyo wangu kwa kuwa timu hiyo kwa sasa inahitaji umoja zaidi kuliko mtengano kwa kuwa imeshatengana kwa muda mrefu sana.

Yanga inatakiwa kuwa kitu kimoja na kuondoka kwenye mfumo wa sasa kwenda kwenye mfumo wa kisasa zaidi.

Wanaopiga kura kesho ndiyo wanajua wapi wanaipeleka Yanga kwa kuwa wao ndiyo wanachagua kiongozi wanayemtaka.

Kama matumbo yao, zawadi au chochote watakachopewa kitawafanya wachague bora kiongozi basi wao ndiyo watakuwa wakilia kila siku, lakini kama watatumia kura yao vizuri na kuchagua kiongozi ambaye hana kashfa lakini anaweza kuongoza basi watakuwa wakichekelea kila siku.

Klabu hii inahitaji kiongozi ambaye atahakikisha kabla hajaondoka kwenye uongozi wake anaacha alama ya kukumbukwa, inahitaji kiongozi anayefahamu changamoto muhimu za klabu.

Yanga inahitaji kiongozi anayefahamu kuwa timu haina uwanja wa mazoezi, lakini inahitaji kiongozi ambaye ataweka umoja kwa viongozi wengine.

Jambo pekee ambalo kiongozi wa Yanga anatakiwa kufanya ni kuhakikisha timu hiyo inakuwa na mafanikio kimataifa, kufika nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, kufika nusu fainali Kombe la Shirikisho Afrika ni alama ambayo haiwezi kusahaulika kwenye timu hiyo kuliko ubingwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic