KAMBI YA SIMBA YATAJWA, MAJEMBE MAPYA YAORODHESHWA
Kama Spoti Xtra lilivyokujulisha Alhamisi iliyopita, sasa ni rasmi kwamba Simba itaweka kambi Afrika Kusini kuanzia Julai 15 na mastaa wote lazima watue Dar es Salaam wiki ijayo kushughulikia visa zao.
Simba itaweka kambi yake nchini Afrika Kusini ‘Sauz’ kutokana na hali ya hewa ya baridi tofauti na ile ya awali ambayo walikuwa wamepanga kuweka Ulaya.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Cresentius Magori ameliambia Spoti Xtra kwamba, lengo ni kuweka kambi ambayo itakuwa msaada kwa kikosi chao kuelekea msimu ujao wa ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kambi itakuwa Afrika Kusini lakini kuanzia Jumatatu wachezaji wanatakiwa kuanza kukusanyika kambini na wale wa nje wanatakiwa kuripoti mapema zaidi kwa ajili ya kushughulikia masuala ya visa kwa wale ambao wanaingia kwa utaratibu huo.
“ Kuna baadhi ya wachezaji ambao wanahitaji kupata visa mapema kutokana na nchi ambazo wanatoka ni lazima wawahi kuja kulikamilisha hilo.
“Sababu kambi pale Sauz tutaanza Julai 15, mwaka huu tutakuwa pale Mungu akipenda na tukiwa huko tufanya maandalizi yetu na kama kutakuwa na michezo ya kirafiki tutatoa taarifa kuwa tucheza na timu zipi,” alisema Magori ambaye amewahi kushika nafasi za juu serikalini.
MASTAA KUPAMBANISHWA
Simba imekiri kwamba kutakuwepo na ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho msimu ujao na lazima wachezaji wapya na wa zamani wapambane kupata mseto wa maana.
Mpaka sasa Simba imesajili wachezaji wa kigeni kama Wilker Da Silva (Brazil), Sharaf Shiboub (Sudan), Tairone Da Silva (Brazil), Gerson Fraga (Brazil), Francis Kahata (Kenya) na Deo Kanda (DR Congo).
Wakati msimu uliopita jeshi ambalo liliibeba Simba ni pamoja na liliongozwa na wachezaji kama Meddie Kagere, John Bocco, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Mohamed Hussein, Aishi Manula Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Clatous Chama, Pascal Wawa, Yusuph Mlipili na msimu ujao wachezaji hao wataendelea kuwa hapo.
Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Cresentius Magori amesema hawana hofu kabisa kuelekea msimu ujao kutokana na usajili mpya sababu bado kikosi cha kwanza msimu uliopita kipo imara.
“Unajua ni kweli kuna wachezaji wapya ambao wanahitaji muda flani kuwa sawa na wenzao lakini sisi kama klabu hatuna hofu na hilo sababu kwa asilimia kubwa kikosi cha kwanza msimu uliopita wachezaji wote wapo hivyo halitupi shida hata kidogo.
“Hawa wachezaji wapya watahitaji muda na hata kama inatokea mechi sasa hivi ya maana tunawatumia wachezaji wetu wa kikosi cha kwanza msimu uliopita sababu wapo.
“Lakini kadri siku ambavyo zitakuwa zinaenda kila kitu kitakuwa sawa kwa sababu itafika wakati tutawapambanisha hawa wa kikosi kipya na wale wa zamani na kuangalia ubora zaidi, hii itachukua muda kidogo kuwa sawa ila baada ya hapo tutakuwa na kikosi bora cha kutisha,” alisema Magori.
Msimu ujao wachezaji ambao hawatakuwepo Simba wale wa kigeni ni Haruna Niyonzima, Asante Kwasi, Nicholas Gyan, James Kotei, huku wa ndani ni pamoja na Adam Salamba, Dida pamoja Said Mohamed ‘Nduda’ na wengine watatajwa wiki ijayo.
CHANZO: SPOTI XTRA
Sio kama itakuwa, lakini ni lazima iwepo ya kirafiki, si hivyo vipi mtajuwa baada ya mazowezi mefika wapi timu, wapi penye kasoro na Nani mwenye kasoro panapojitaji kuwekwa sawa na hilo ndio lengo la sawa
ReplyDelete