YANGA KUMEKUCHA, KAMBI YA KISHUA YAANZIA DAR
Yanga jana Jumapili wameanza kambi ya msimu ujao ambapo tangu Ijumaa iliyopita mastaa wapya wa klabu hiyo wamekuwa wakiingia mmoja mmoja.
Yanga wanaanza kambi mapema kwa ajili ya kuviunganisha vifaa vyote walivyosajili ambapo watakusanyana Jijini Dar es Salaam kisha kambi rasmi ya aina yake itakuwa mkoani Morogoro chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila raia wa Zambia.
Kocha mkuu Mwinyi Zahera yeye bado yupo nchini Misri kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Huru Afrika (Afcon) na DR Congo ambayo leo itacheza na Madagascar.
Picha lilianza juzi Ijumaa baada ya kuwasili kwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uganda, Juma Balinya na beki kisiki raia wa Burundi, Mustapha Seleman. Kumbuka wote hawa walikuja kwa ndege na wakapokelewa pale Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar.
Wakati watu wakiwa hawajakaa vizuri fasta akashuka straika Maybin Kalengo raia wa Zambia ambaye yeye aliwasili usiku mnene.
Baada ya Kalengo, kuingia nchini mastaa Patrick ‘Papy’ Sibomana ambaye anacheza
winga sambamba na Issa Bigirimana ‘Walcott’ nao wakaingia jana Jumamosi mchana ambapo ni Spoti Xtra pekee ambalo lilinasa juu ya ujio wa nyota hao ambao ulifanywa siri lakini likapata na fasta kwenda Eapoti wakati wa ujio huo.
Spoti Xtra ambalo linaongoza kwa mauzo Alhamisi na Jumapili liliwashuhudia nyota hao wakitua uwanjani hapo ambapo walipokelewa na mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh kisha wakapelekwa klabuni mitaa ya Twiga na Jangwani kwa ajili ya kuonyeshwa mandhari ya jengo hilo kisha baadae kwenda kwenye hoteli moja ya kishua kupumzika.
Bigirimana na Sibomana walizuiwa na viongozi wa Yanga kuzungumza lolote jana. Bigirimana ambaye anasifika kwa mbio na kufunga mabao akitokea winga ya kulia na kushoto ni miongoni mwa wachezaji wanaosifika Rwanda.
Ujio wa Bigirimana na Sibomana, unaifanya klabu hiyo kubakisha wachezaji wawili pekee wa kigeni beki Mghana Lamine Moro na straika Mnamibia Sadney Urithob kuwasili kwa ajili ya kuanza kambi ambayo viongozi wa timu hiyo wamepanga iwe ya bab kubwa ili kuijenga timu kiushindani.
Wakati wakiwa wamewasili uwanjani hapo, gumzo kubwa lilikuwa ni Bigirimana ambaye amekuja Bongo na mchumba wake raia wa Rwanda ambaye alimvisha pete hivi karibuni. Binti huyo mrembo alikuwa gumzo kwa mashabiki waliokuwa Uwanjani hapo.
Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema: “Kambi yetu tutaanza Jumapili(leo) na itakuwa kambi bora kwa sababu tutatumia kile kiasi cha milioni 930 ambacho tulikipata katika michango ya mashabiki wetu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment