July 18, 2019


TUNAJIFARIJI kweli kwa sasa kwa kuendelea kuwa watazamaji wa michuano ya Afcon inayoendelea nchini Misri kisa timu za kundi C zimepenya mpaka hatua ya fainali.

Ijumaa miamba hii itakutana kwenye hatua ya fainali ili kumsaka bingwa mpya wa Afrika baada ya bingwa mtetezi Cameroon kutolewa na Nigeria hatua ya 16 bora, kwenye michuano hii inayofanyika Misri.

Ni jambo zuri kwa kujifunza na kujiuliza tumetumiaje fursa ya kucheza na timu kubwa  kwenye michuano ya Afcon na tumejifunza nini?

Kufurahia pekee hakuwezi kutupa jambo la kujifunza kwani wao ni Algeria wametufunga mabao mengi na wametinga hatua ya fainali hata Snegal pia wametufunga wametinga hatua ya fainali.

Tulikuwa na nafasi ya kufanya makubwa na kuonyesha ushindani endapo tungejipanga tangu awali na kupunguza kabisa siasa kwenye michezo.

Hakuna ambaye amebebwa kwenye michuano ya Afcon kila mmoja amepambana na kutafuta matokeo kwa hali na mali bila kukata tamaa.

Dunia nzima kwa sasa inatambua kwamba Tanzania ilikuwa kundi C na haijaambulia hata pointi moja hicho ndicho kikubwa suala la kusema timu za Tanzania zimetinga fainali hilo ni kujilisha upepo.

Kila timu zimepambana tangu awali kwenye hatua ya makundi mpaka kutinga robo fainali hali inayozifanya zinakutana tena kumtafuta mbabe wa Afrika.

Kumbuka kwamba Algeria walimaliza kundi C bila kupoteza mchezo hata mmoja wamejikusanyia pointi  9 na Senegal wao walipoteza mchezo mmoja mbele ya Algeria hivyo kazi ipo.

Hapo tunaona kwamba kila mmoja anahitaji kulinda rekodi yake, Senegal wanampango wa kuipoteza ile rekodi ya kufungwa na Algeria wao wanahitaji kulinda rekodi waliyoanza nayo.

Kazi ni kubwa na mshindi lazima apatikane hivyo hapa ni somo tosha kwetu baada ya kutolewa kwenye michuano hii ya kimataifa.

Kilichowabeba wenzentu ni  juhudi, jitihada na nidhamu hasa wakiwa ndani na nje ya uwanja mwisho wa siku wanapata kile wanachokitaka

Senegal wao walijiandaa kufanya kweli maana tangu mwanzo walionekana wakipambana licha ya kupitia ugumu mwisho wa siku wamefikia safari yao kwa kuvuka vikwazo vyote.

Algeria nao wapo vizuri mwanzo mwisho wamecheza kwa kujituma na walikuwa wanawasiliana ndabi ya uwanja kwa kutafuta matokeo chanya muda wote.

Haina maana kwa sasa tujikatie tama hapana kwani timu yetu ni bora na ilikuwa vizuri isipokuwa hatukuwa tumejua kipi ambacho tunakihitaji.

Tulipotimiza lengo la kushiriki michuano ya Afcon baada ya kupita miaka 39 tukawa hatuna mpango mwingine maalumu ambao ungetupa nafasi ya kusonga mbele zaidi ya tulipoishia.

Kifupi hatukuwa siriazi katika kile tunachokifanya ndio maana hata kambi yetu ilikuwa ina mambo mengi ambayo si ya kimchezo hivyo tulikuwa tunajipoteza wenyewe na kuchezea nafasi ambayo tuliipata.

Wachezaji hawakuwa wanapewa ushirikiano wa kutosha na mashabiki pamoja na wachezaji wenye uwezo kwenye michuano ya Afcon.

Kikubwa kilichoturudisha nyuma ni kuchanganya mambo mengi kwa wakati mmoja ilihali bado hatukuwa na uzoefu wa kutosha.

Kila mmoja aliamua kujibebebesha jukumu la kupambania timu ilihali kazi ya kocha inafahamika pamoja na wale watu wa hamasa hapa ndipo tulipojifelisha.

Hamasa ilikuwa chini mwanzo mwisho ilikuwa kama hakuna kitu kikubwa ambacho kinatokea, matarajio yetu yalikuwa ni makubwa na kile tulichokipata kilikuwa ni kidogo.

Tuliingiza siasa badala ya kutumia watu wenye uzoefu kufanya kazi ya kuamsha na kuzindua hamasa ambayo ilianguka kwa kiasi kikubwa tulipopata nafasi ya kukwea pipa kwenda Misri.

Wakati mwingine tuwatumie wachezaji wazoefu kurejesha morali na kuipa matumaini timu pamoja na mashabiki ambao imani yao imeanza kupotea.

Tumeona namna uendeshaji ulivyo kwenye michuano ya Afcon hivyo ni wakati wetu pia kuangalia ni namna gani michuano yetu ya ndani tutaiendesha msimu ujao ambao unaanza Agosti 23.

Bado tuna kitu cha kujifunza hata kama hatuna pointi mkononi kushiriki kwetu ni hatua moja na kukosa kwetu pointi ni hatua kwa kuwa hatukujipanga kuwe ni darasa.

Timu bora inayoshinda  ni ile iliyojiandaa vema kupata matokeo ndani na nje ya uwanja nina imani wachezaji wana kitu cha kipekee ambacho wamekipata.

Ushindani ni muhimu kupata timu bora na watu bora ambao wataiongoza timu yetu tuna safari ndefu na kazi kubwa ya kufanya kwa ajili ya wakati ujao.

Wakati mwingine ni lazima kupambana na wale walio imara ili kuwa bora na kupata kitu kitakachotufanya tujivunie kwani ilikuwa ni bahati kupangwa kwenye timu lenye wachezaji bora na wanaoelewa nini wanakitaka.

Pia kujikatia tamaa mapema ni mbaya na haifai kwenye soka tuna nafasi ya kufanya vema iwapo tutaamua kupambana na kujituma bila kujidharau wenyewe.

Kila mmoja ana uwezo wa kushindana iwapo ataamua hivyo wakati wetu tulioupoteza unapaswa uwe darasa la kweli litakalotufanya wakati mwingine tuwe siriazi.

Bahati kubwa ambayo tuliipata kucheza na timu kama Algeria na Senegal kimahesabu zingejibu wote tungekuwa na furaha kubwa.

Fikiria mtu kama Sadio Mane anayekipiga Liverpool pamoja na Mahrez anayekipiga Manchester City ni fursa ambayo wachezaji wetu hawakuiona.

Endapo wangekuwa makini leo hii tungetoa hata wachezaji wawili kwenda kufanya majaribio nje ya nchi kwa kuwa mawakala wengi wanafuatilia michuano ya Afcon.

Wale ambao wanaipenda Liverpool ilikuwa ni lazima waitazame kwa ukaribu timu ambazo zipo kwenye kundi moja na Senegal hivyo nafasi ya wachezaji ilikuwa kubwa.

Kwa kuwa tumepoteza kila kitu hakuna haja ya kupoteza na matumaini maisha lazima yaendelee hasa kwenye soka na maandalizi yetu yanatakiwa yawe makubwa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic