July 30, 2019


EMMANUEL Amunnike habari zake kwa sasa zimeshafungwa kwa kuwa amekubaliana na hali halisi ya kukiacha kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania.

Matarajio ya wengi ilikuwa ni kwenye michuano ya Afcon kufanya vema na mwisho wa siku kila kitu kikawa tofauti na vile ambavyo wengi walikuwa wanaamini.

Ni jambo jema hasa kwa kuwa hakuna mgogogro wowote na pande zote mbili zimekubalina hasa ukizingatia kwamba watanzania wengi wanapenda kuona matokeo chanya hata TFF nao hesabu zao ni kuona Taifa linapata matokeo chanya.

Rekodi ambayo ameiweka itabaki kwenye kumbukumbu kwani licha ya kutimuliwa ni yeye ameiongoza timu kutinga hatua ya makundi ya michuano mikubwa Afrika ya Afcon akiwa ni Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Hii imewezekana baada ya kupita miaka 39 ambayo wachezaji wote wanaoitumikia kwa sasa timu ya Taifa hakuna hata mchezaji mmoja aliyekuwa anakipiga ndani ya kikosi cha timu ya Taifa kwa wakati huo hivyo inamaanisha kwamba ni muda mrefu umepita.

Mema aliyoyafanya tutayakumbuka na hata maumivu ya kupoteza kwenye michuano yetu ya Afcon haitafutika kwani ni rekodi na hatuwezi kukataa kwamba mechi zetu tatu zote tulifungwa na tulimaliza kundi C tukiwa hatuna hata pointi moja zaidi ya kubeba furushi la mabao nane nasi tukifunga mabao mawili.

Ni rekodi yenye maumivu na uchungu hivyo inatoa taswirwa kwamba wakati ujao TFF ambao ndio wanaochagua kocha wa kuinoa timu ya Taifa wanatakiwa kuwa makini na kusimamia weledi wa kazi na sio kuweka mapenzi yao binafsi kwenye maslahi makubwa ya nchi.

Tukumbuke kuwa kwa sasa timu ya Taifa ipo chini ya Kaimu Kocha Mkuu Ettiene  Ndayiragije akipeana sapoti na wazawa, Suleman Matola na Juma Mgunda na mchakato uliopo kwa sasa ni kufuzu michuano ya Chan.

Ukiachana na Chan bado tunahitaji kuwa na kocha mkuu wa timu ya Taifa ambaye atasuka kikosi kipya cha ushindani kwa ajili ya kufuzu pia michuano ya Afcon.

Hivyo bado kuna uhitaji wa kumpata kocha mwenye uwezo na mwenye kiu ya mafanikio pale ambapo anakuwa anafanya kazi na sio ilimradi tu.

Nasema hivyo kwa sababu ya yale ambayo yamejitokeza kwa Amunike alikuwa ni mpole wa sura ila mengi nyuma ya pazia wanayajua wachezaji wenyewe licha ya kutokusema hata TFF nao wanajua namna alivyokuwa.

Mwalimu wa aina hii kama atapewa nafasi tena basi kuyafikia mafanikio ya soka itakuwa ni historia hivyo kwa hili TFF liwe darasa na maamuzi yao yawe yenye manufaa kwa Taifa.

Ukubwa wa timu ya Taifa uendane na ukubwa wa mwalimu atakayekuja kuifundisha timu, vigezo muhimu vizingatiwe kwa kuifuatilia rekodi yake na kujua namna gani anaweza kumudu mazingira yetu.

Namna pekee ya kumpata kocha bora ni kufanya utafiti mzuri tena wa kina na kutumia jopo la wataalamu kumchunguza huyo ambaye mnahitaji.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic