WAKENYA WATUMIKA KUIUA ZESCO
Kabla ya kucheza na Zesco, Yanga imepanga kucheza michezo miwili ya kirafiki ukiwemo mmoja wa kimataifa kutoka moja ya klabu nchini Kenya.
Yanga inatarajiwa kucheza na Zesco katika mchezo wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Septemba 13 hadi 15 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo imefuzu hatua hiyo baada ya kuwaondoa Township Rollers ya nchini Botswana kwa kuwafunga nyumbani kwao bao 1-0 kabla ya ule wa awali uliopigwa Uwanja wa Taifa ambao ulimalizika kwa sare ya 1-1.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, timu hiyo imepanga kwenda kuweka kambi yake mkoani Mwanza ambako huko watacheza michezo miwili ya kirafiki, kwanza watacheza na Mbao FC kisha klabu moja kutoka Kenya.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa timu hiyo kutoka Kenya itatangazwa hivi karibuni mara baada ya kuthibitisha kuja nchini kucheza mchezo huo kabla ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Zesco.
Aliongeza kuwa michezo hiyo miwili ya kirafiki wataitumia vema kama sehemu ya kujiandaa na mchezo huo wa kimataifa ambao wamepanga kuwaondoa Zesco na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa Afrika.
“Tunauchukulia umuhimu mkubwa mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika tutakapocheza na Zesco hapa nyumbani. “Hatutaki kufanya makosa kama yaliyojitokeza katika mchezo wetu na Rollers tuliocheza hapa nyumbani kwa kuruhusu bao.
“Hivyo, tumepanga kumpa maandalizi mazuri kocha wetu, Mwinyi Zahera kwa kumuandalia kambi nzuri pamoja michezo ya kirafiki miwili ukiwemo mmoja wa kimataifa kwa kuileta moja ya klabu kubwa nchini Kenya tutakayocheza nayo,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Hizo taarifa ni kweli tupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha kambi hiyo ya mkoani Mwanza na kama ratiba ikienda vizuri basi tutacheza mechi za kirafiki kabla ya kucheza na Zesco.”
0 COMMENTS:
Post a Comment