September 16, 2019




NA SALEH ALLY
TUKUBALIANE, pamoja na kwamba kulikuwa na dalili kuwa Mwenyekiti wa Simba, Swedi Mkwabi anaweza akajiuzulu, lakini habari za uhakika kwamba ameamua kuachia ngazi, zinashitua.

Wako watakaosema kuwa hazishitui, wanajua mambo yatakwenda kama yalivyopangwa, lakini inawezekana hili suala hawaliangalii kwa undani.

Binafsi ninaona kuwa kweli mambo ya Simba yatakwenda tu kama kawaida lakini katika hali ya kawaida kuna kila sababu ya kujiuliza, kwa nini Mkwabi ajiuzulu.

Mfano, tumeelezwa sababu hasa iliyomfanya ajiuzulu ni kutokana na kubanwa na masuala yake ya kikazi, sote tunafahamu kuwa Mkwabi ni mmoja wa wafanyabiashara wanaojituma sana.

Mkwabi ana ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa, ndio maana wakati fulani alijiondoa katika mpira na baada ya hapo mambo yake yakaanza kwenda vizuri akipambana na biashara zake hadi pale baadhi ya wazee kadhaa wa Simba walipomfuata na kumshawishi agombee.

Leo, ameamua kujiuzulu akisema kuwa ni kutokana na kubanwa na masuala yake ya kikazi, yaani biashara zake. Lakini kweli sote tunajua, Mkwabi alikuwa na biashara hizo tokea anaingia. Sasa vipi aseme leo zimembana kiasi hicho? Ndio maana nasema kuna jambo ambalo badala ya Mkwabi kuondoka na kuachia ngazi kwa namna alivyokwenda, basi ingekuwa vizuri akasema.

Naona si sawa kwa Mkwabi kuondoka kimya na kueleza tulichoelezwa. Naona si sawa kukaa kimya bila ya kuweka wazi kama kuna jambo lilimtatiza au hakufurahia.

Simba ina muunganiko wa pande mbili unapozungumzia suala la umiliki, ukianza na ule upande wenye asilimia 49 ambazo zinatakiwa kumilikiwa na si chini ya watu watatu.

Upande wa “keki” kubwa yaani asilimia 51, unamilikiwa na wanachama na Mkwabi ndiye alikuwa mtu ambaye anaongoza sehemu kubwa ya umiliki wa Simba, vipi aondoke wakati ndio kipindi ambacho Simba inataka kwenda kwenye mabadiliko kwa vitendo!

Kuna kitu amekiona hakiendi sawa na baada ya muda kunaweza kuwa na tatizo ndani ya Simba? Ameona kuna mwenendo unaweza kuhatarisha afya ya Simba hapo baadaye na ameshindwa kuzuia? Au kuna kipi kimemshinda?

Mkwabi aseme, ili kama alishindwa yeye, basi iwe wazi. Kama ameshindwa kuzuia kitu fulani na anaona si sahihi, aache mjadala huo ili uwe na msaada kwa Simba wakati mwingine.

Hofu yangu ni kwamba kama Mkwabi ataondoka akiacha kisingizio kisicho na nguvu ya kusikilizwa na kukubalika, wakati mwingine Simba itaingia kwenye hisia na kuishi katika hisia badala ya uhalisia.

Inawezekana kabisa kukawa na mvutano wa ndani ambao unatokana na maslahi ya kila upande na katika masuala ya umiliki wa mgawanyiko huwa yanatokea.

Huenda upande unaomiliki kipande kidogo ukawa na nguvu kuliko anayeongoza umiliki wa kipande kikubwa, hivyo kukawa na “mapambano ya nguvu” ambayo wanachama na mashabiki hawayajui na wakati kukawa na hali ya kuonyesha upande fulani ni mbaya na haufai.

Kawaida yangu nimekuwa na hofu sana na watu wanaojiuzulu katika sehemu mbalimbali. Mara nyingi napenda kusikiliza sababu ili nijifunze na sababu alizotoa Mkwabi zinaonyesha wazi “anaosha ngoma juani” na inawezekana kuna kitu ambacho kama angekiweka wazi, basi mashabiki na wanachama wangefaidika kuendelea kuisaidia Simba hapo baadaye.

Katika kipindi kama hiki, Simba haiwezi kwenda mwendo wa mtelezo na kama ikiwa hivyo basi ujue kuna tatizo kwa watu kuelewa sahihi, kusikiliza sawa na kutekeleza sawa.

Lazima kuwe na eneo watu wanapishana angalau kidogo kwa maana ya utofauti unaendana na mawazo tofauti lakini yenye nia moja ya kujenga.


Kutokea watu kuachia ngazi kama Mkwabi inawezekana lakini haiwezi kuwa kwa sababu nyepesi kama hizo. Msisitizo wangu, Mkwabi aseme jambo kuisaidia Simba na kama halitakuwepo, sawa, acha maisha yaendelee na yeye awe sehemu ya kuendelea kuchagiza maendeleo hayo hata akiwa nje ya uongozi.

8 COMMENTS:

  1. Sasa wewe Saleh unachotaka Mkwabi aseme au afanye nini baada ya kujiuzulu? Unataka afanye kama msaliti kilomoni? Kwa maelezo yako Saleh inaonekana una donge rohoni yakwamba kwanini Mkwabi kaacha wazifa wake ndani ya simba kwa amani? Ulitamani na bado unalia lia kwanini Mkwabi hakuondoka Simba akiirarua na kuzua taharuki ndani ya klabu ya Simba.Labda baadhi ya waandishi mnamufaika na migogoro ndani ya vilabu vyetu? Unachomuomba Mkwabi akieleze ni kipi zidi ya ya yale aliyoyaeleza kuwa kabanwa zaidi na majukumu yake binafsi kiasi cha kushindwa kuitendea haki nafasi yake ya uongozi ndani ya simba. Na hata kama Mkwabi angeondoka simba kwa mizengwe au na donge rohoni, kama mwanasimba halisi au mwanafamilia halisi wa Simba kuna haja gani kwa Mkwabi kutoa mambo ya ndani ya timu na kuyaeka hadharani kwa faida ya nani? Vyombo vya habari? na maadui wa maendeleo wa Simba? Alichokifanya Mkwabi ni cha kupongezwa sana badala ya watu kuanza kumchokonoa aanze kusema au kufanya mambo ya hovyo kwa klabu yake pendwa. Kama kuna tatizo la uongozi ndani ya simba kamwe haliwezi kutatuliwa na Salehe jembe au vyombo vya habari bali ni wanasimba wenyewe ndio watakalolitatua kwa kutumia taratibu muafaka na kanuni zao na sio kwa malumbano na mipasho ya kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Simba ni taasisi kubwa imeajiri wataalam wa nje kadhaa wa kadhaa kuhakikisha wanafanya mambo kwa usahihi sasa kama kuna kiongozi ndani ya Simba anahisi hawezi kuendana na kasi ya mabadiliko ndani ya klabu hiyo kwanini aendelee kuwepo? Nadhani Simba ya sasa kiongozi anatakiwa kuifanyia kazi Simba kwa manufaa ya klabu badala ya kiongozi kutegemea kufanyiwa kazi na Simba kwa maslahi yake binafsi.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Kama mzee Kilomoni anavyotaka kufanyiwa na Simba.Ndio maana namshukuru mwenyezi mungu kwa kutupa Rais Magufuli aliyedhamiria kufanya kazi kwa ajili ya watanzania wote.Hivyo Nkwabi amejiuzulu na ametoa sababu zake za kuachia ngazi hivyo hakuna cha maajabu tunasubiria mwenyekiti mwingine atuongonze na hatutaki mwenyekiti au kiongozi anayeongonza kwa remote control za mzee kilomoni na wazee wenzake wanaongoja kupewa fadhila na Simba.

      Delete
  2. Mkwabi amesema sababu za kujiuzuru wewe huzitaki kwasababu haziiyumbishi Simba. Basi tueleze wewe zile unazoona zitafaa kuiyumbisha Simba labda Chura atapumua.

    ReplyDelete
  3. Salehe ana hoja ya msingi nami naiunga mkono..time will tell soon!

    ReplyDelete
  4. Anataka bilioni 20 ziingizwe katika akaunti yake akugaie na wewe @salehjembe

    ReplyDelete
  5. Hakuna jambo la kuisaidia Simba zaidi ya pesa za mishahara na miundombinu bora kwa timu, hayo mengine hatyataki

    ReplyDelete
  6. Ukweli utasimama tu, tatizo ni mashabiki na wanamichezo, mashabiki husema lolote popote, wanamichezo hutathimini kabla ya kusema. Muda ukifika tutaelewa haya maneno.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic