October 6, 2019


Baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza mwezi Septemba, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amemtaka mshambuliaji wa Simba, Miraji Athuman 'Sheva' kutobweteka.

Juzi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimtangaza Sheva kutwaa tuzo hiyo ambayo ilikuwa ni ya pili mfululizo kwa Simba baada ya Meddie Kagere kuibeba pia mwezi Agosti.

Rage amemshauri Sheva kuendelea kupambana zaidi uwanjani huku akimtaka aendelee kuwa na nidhamu ili afikie malengo yake.

Ameeleza kuwa Sheva ni mchezaji mzuri ambaye amekuwa akimfuatilia siku nyingi, hivyo ni vema kuitumia vema fursa aliyoipata ndani ya Simba ili imtimizie ndoto zake.

"Sina shaka na uwezo wake, sijashangaa kabisa kuchukua tuzo hiyo sababu kila mtu anamtazama na anaonekana namna anavyopambana licha ya mara ya kutokea benchi mara nyingi.

"Nadhani unakumbuka wiki kadhaa nyuma nilizungumza na wewe na nikakweleza huyu kijana atafanya maajabu kama ataendelea kuonesha nidhamu na heshima kwa timu na kocha wake, sasa umekiona kilichotokea.

"Kuna uwezekano mkubwa akaendelea kuzibeba zaidi ikiwa tu atajikita na kilichompeleka Simba, nitafurahia zaidi kumuona akija kuwa Mbwana Samatta wa baadaye," alisema Rage.

Katika msimu huu, Sheva ameichezea Simba jumla ya mechi nne na akifanikiwa kuingia kambani mara tatu kwa kufunga bao moja kila mechi ikiwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar, JKT Tanzania na Biashara United.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic