MISS UNIVERSE TANZANIA YAREJEA KWA KISHINDO
BAADA ya kimya cha mwaka mmoja, kampuni ya Compass Communication imeandaa tena mwaka huu, shindano la Miss Universe Tanzania.
Baada ya kufanya usaili na warembo takriban 90 kutoka mikoa tofauti nchini, shindano hili la kitaifa la mwaka huu linahusisha warembo 10 kutoka mikoa ya Mwanza, Arusha, Dodoma na Dar es Salaam linatarajiwa kufanyika tarehe 12 mwezi wa kumi katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam kuanzia saa moja jioni.
Katika miaka ya nyuma shindano hili limeweza kuibua vipaji vya wengi ambao wameendelea kufanya vyema katika ulimwengu wa urembo na kuipeperusha vyema bendera ya taifa. Baadhi yao ni pamoja na Flaviana Matata, Nelly Kamwelu na Hellen Dausen.
“Urembo ni sanaa na urembo ni kazi, na ndiyo maana sisi kama Compass Communications tumeona fursa na kuamua kuendeleza vipaji vya wasichana wengi wenye ndoto na wenye kuamini kuzifikia kupitia tasnia hii ya urembo,” ameeleza mkurugenzi wa kitaifa wa shindano hili, Maria Sarungi Tsehai
Pia kwa mwaka 2019 mashindano haya yanaadhimisha miaka 12 tangu kuanza kufanyika hapa nchini mwaka 2007. Kama ilivyo adha, mshindi wa Miss Universe nchini ataenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia hapo baadaye mwaka huu.
Tsehai ameeleza kuwa mafanikio haya yametokana na ushirikiano mzuri na wadau wote wa tasnia.
“Tunaishukuru sana serikali, wizara husika na Baraza la Sanaa (BASATA) kwa kutupatia ushirikiano kwa miaka yote na ni matumaini yetu tutazidi kupata ushirikiano kutoka kwenu na kusongesha kwa pamoja hili gurudumu la sanaa,” ameongezea Tsehai.
Miss Universe kwa mwaka 2019, imedhaminiwa na Precision Air, Serena Hotel, Sea Cliff Luxury Apartments , Kwanza TV, Pepsi , Samaki Samaki Fish and More na Timeless Saloon.
Imetolewa, Dar es Salaam 09/Oktoba/2019.
0 COMMENTS:
Post a Comment