October 7, 2019




WACHEZAJI wa Kigeni wana faida nyingi sana kwenye ligi yetu. Tatizo letu hatuwatumii ipasavyo. Tunaishia tu kunywa nao pombe mtaani. Tunaishia tu kubadilishana nao wanawake! Hatuvuki zaidi ya hapo.

Wachezaji wa Kigeni sio tu kwamba wanatetemekewa na viongozi wa klabu Tanzania, lakini hawa jamaa wanajitambua pia. Uelewa wao kwenye haki zao ni mkubwa mno kuliko sehemu kubwa ya wachezaji wetu.

Wapo wachezaji wazawa wanaojielewa lakini idadi ni ndogo mno. Watu kama kina Emmanuel Okwi walipaswa kuamsha wachezaji wetu.

Tuna orodha ya wachezaji wengi wazawa wanaocheza wakidai mishahara. Tuna wachezaji wengi wazawa wanaocheza bila hata kulipwa fedha zao za usajili!

Pale kwenye Klabu ya Yanga kwa sasa wapo wachezaji nane ambao wanadai fedha zao za usajili wa miaka miwili mpaka mitatu iliyopita! Nimemsikiliza makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela wiki iliyopita amekiri kuwepo kwa madai hayo.

Wachezaji kama Mwinyi Haji Mngwali, Pato Ngonyani na Andrew Vincent mpaka leo wanadai fedha zao za usajili wa miaka miwili iliyopita! Inashangaza sana! Ina huzunisha sana.

Hawa wachezaji wote mikataba yao ilimalizika na sio sehemu ya timu msimu huu. Najiuliza tena, Hawa wachezaji walimuona kweli Emmanuel Okwi alivyokuwa anaendesha mambo yake?

Emmanuel Okwi ni moja kati ya wachezaji wa kigeni waliokuwa wanajitambua sana kwa miaka ya hivi karibuni. Hakuna klabu yoyote ambayo imewahi kumchezea. Hakuna kiongozi yeyote aliyewahi kufanya hivyo mbele ya Mganda huyo.

Ni mchezaji aliyetimiza wajibu wake lakini pia ni mchezaji aliyesimamia vizuri maslahi yake. Amecheza Simba, amecheza Yanga. Isingewezekana kwa Okwi kumaliza mkataba bila kupewa fedha yake ya usajili. Isingewezekana.

Okwi ni mchezaji ambaye asingeweza kusaini mkataba wowote ule bila ya kumuhusisha mwanasheria wake. Isingewezekana kabisa. 

Wachezaji wetu wanapaswa kujifunza namna ya kulinda maslahi yao. Wachezaji wanapaswa kujua thamani yao. Mpira wa miguu ni mchezo wa muda mfupi sana. Ni Maisha kama ya miaka 10 mpaka 15.

Mchezaji anapaswa kutengeneza fedha nyingi sana kipindi hiki na kufanya uwekezaji mkubwa utakaomfanya aendelee kuishi maisha mazuri hata akiwa nje ya uwanja. Wachezaji wetu wazawa wengi hawalitambui hili. Wachezaji wetu wengi wanakosa wasimamizi.

Wachezaji wa kigeni kuna namna tunaona kama wanatetemekewa, lakini hawa watu pia wanajitambua sana. Hawa wana watu wa kuwasimamia mambo yao. Wachezaji wa kwetu wengi wako wao tu. Wanasaini wao. Wanaibiwa wao!

Hakuna mtu anayejua kila kitu, ndiyo maana hata matajiri nao wana madaktari wao, wana wanasheria wao na wahasibu wao. Mchezaji kazi yake ni kucheza mpira, mambo ya maslahi anahitaji mtu wa kumsimamia.

Mchezaji kama Okwi asingekubali kuendelea kucheza wakati fedha yake ya usajili hajalipwa. Asingekubali. Wachezaji wetu wazawa wameendelea kuwa wanyonge na Viongozi wa klabu kubwa wanaendelea kuwaumiza! Inasikitisha sana.

Muda si mrefu umri wa mpira utakwisha kwa hawa wachezaji na tutaanza kuwachangia fedha za kuendesha maisha! Inasikitisha sana! Natamani Okwi angerudi tena Tanzania ili awafundishe wachezaji wetu umuhimu wa kuchota fedha nyingi wakati wa kucheza soka.

Wachezaji wetu bado wamelala. Watu kama kina Obrey Chirwa, Donald Ngoma, Kipre Tchetche wasingeweza kumalizia miaka miwili bila kupewa chao.

Kuna kipindi Mbwana Samatta aliwahi kuigomea Simba kwa sababu ya kutopewa mahitaji yake. Simba ilitimiza fasta kwa sababu walihitaji huduma yake. Mchezaji ni lazima kwanza atimize wajibu wake na kisha upande wa muajiri ufuate.

Mwinyi Haji alikuwa mlinzi mahari sana wa Yanga. Inasikitisha kuona mpaka mkataba wake unamalizika mchezaji wa kiwango chake kwa wakati ule hakuwa amelipwa fedha yake ya usajili. Inasikitisha sana.

Pato Ngonyani ni miongoni mwa watoto wa nyumbani kabisa pale Yanga. Unashangaa ni kwa nini mpaka leo hajapewa chake. Andrew Vincent ni moja kati ya wachezaji waliokuwa imara sana kwenye idara ya ulinzi lakini naye thamani yake haitambui! Sarakasi hizi usingeweza kuzifanya kwa mtu kama Emmanuel Okwi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic