October 9, 2019


KUNA timu tano za Kiarabu zimesalia kwenye Kombe la Shirikisho. Yanga huenda ikapangiwa yoyote leo Jumatano saa 2 usiku, kwenye droo itakayofanyika katika Hoteli ya Hilton Pyramids Resort, Cairo, Misri.

Yanga itacheza mechi moja nyumbani na ugenini, kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kuchemka kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, zimekuwa zikihofia kucheza na timu za Kiarabu kutokana na uzoefu wa timu hizo na fitna zao kwenye michuano hiyo, hususani wanapokuwa nyumbani.

Klabu tano ambazo zina uwezekano mmoja wao akakutana na Yanga leo ni pamoja na RS Berkane, Hassania Agadir kutoka Morocco, Al-Masry na Pyramids za Misri, pamoja na Paradou AC ya Algeria. Mechi ya kwanza itapigwa Oktoba 27 na marudiano ni Novemba 3.

Timu nyingine ambazo huenda mojawapo ikapangwa na Yanga ni  Zanaco (Zambia), Enugu Rangers (Nigeria), Djoliba (Mali), ESAE (Benin), DC Motema Pembe (DRC), FC San Pédro (Ivory Coast), Bandari (Kenya), BidvestWits (Afrika Kusini), TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) na Triangle United (Zimbabwe).

Timu ambazo haziwezi kupangwa na Yanga kutokana na kwamba zote zimetokea kwenye Ligi ya Mabingwa ni Guinea Horoya (Guinea), Enyimba (Nigeria), Gor Mahia (Kenya), KCCA (Uganda), Asante Kotoko (Ghana) na UD Songo (Msumbiji).

Nyingine ni Elect-Sport (Chad), Cano Sport (Guinea ya Ikweta), Al-Nasr (Libya), Fosa Juniors (Madagascar), FC Nouadhibou (Mauritania), Cote d’Or (Seychelles), ASC Kara (Togo) na  Green Eagles (Zambia).

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesisitiza kwamba yupo tayari kupambana na yeyote atakayekuja mbele yake kwani kikosi chake kimeanza kuimarika na kuzoeana.

Kama Yanga ikifuzu hatua hiyo ya makundi itakuwa bize hadi Aprili mwakani ikicheza ligi ya ndani na michuano ya kimataifa. Yanga ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia kwenye michuano ya kimataifa baada ya Simba, KMC, Azam, Malindi na KMKM kutolewa kwenye hatua za awali.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic