December 31, 2019


JOTO la mechi ya watani linazidi kupanda kwa sasa ambapo kila mchezaji na benchi la ufundi wa timu hizi mbili, hawana kingine wanachofikiria kwa sasa zaidi ya kuona ni namna gani watatoka baada ya dakika 90 kupita Januari 4, 2020.

Ukipiga hesabu tangu leo Desemba 30, zimebaki siku nne tu kabla ya watani hawa kumenyana pale Uwanja wa Taifa.

Wakati mechi hiyo inakuja, kuna wachezaji ambao waliondoka moja ya timu hizi na kutua sehemu nyingine.

Wachezaji hao ni Ibrahim Ajibu na Gadiel Michael aliyesaini kandarasi ya miaka miwili ambao walitoka Yanga na kuja Simba.

Championi Jumatatu limefanya mahojiano na Gadiel kuhusu namna anavyokiona kikosi chao cha Simba pamoja na maandalizi kuelekea kwenye mechi hiyo pamoja na nyingine ambazo zinawahusu wakiwa ni mabingwa watetezi.

Kumbuka Gadiel ndiyo anacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Yanga tangu atue Simba. Huyu hapa anaanza:

“Nimekuwa kwenye maisha ya soka la ushindani kwa muda mrefu na inanifanya nakuwa bora siku zote, kutokana na muda ambao nimecheza jambo ambalo linanifanya nizidi kupambana siku zote nje na ndani ya uwanja.

KIPI KINAKUFANYA USICHUJE?

“Nidhamu katika kila jambo ambalo ninalifanya na kutambua nini ambacho ninakitaka na kwa wakati gani ambao ninafanya.

“Katika kila ambacho ninakifanya ninamtanguliza Mungu ambaye yeye ni mpaji wa yote jambo ambalo linanifanya niwe kwenye ubora wangu muda wote.

UNAITAZAMAJE SIMBA?

“Ni timu ya kipekee ndani ya Bongo, imejipanga katika kila idara kuanzia uongozi na wachezaji wote wanatambua wanatakiwa kufanya nini na kwa wakati gani wafanye hayo mambo jambo ambalo linaifanya iwe hapa ilipo kwa sasa.

ULIKUWA YANGA NA SASA SIMBA KWA NINI?

“Maisha ya mchezaji na kazi anayofanya havimfanyi awe wa muda wote sehemu moja kwa wakati wote. Mchezaji anaweza kuhama timu moja kwenda timu nyingine kulingana na makubaliano na hicho ndicho kilichonitoa ndani ya Yanga na sasa nipo Simba naendelea kupambana.

KUNA KITU CHA UPEKEE NDANI YA SIMBA?

“Kuna upekee katika maisha, hasa ukiangalia namna ambavyo ninaishi na wenzangu ndani ya Simba. Hapa sisi ni familia moja na kila mmoja anafanya jambo lake akitambua ni la familia

UZITO WA MECHI ZENU ZA LIGI UPOJE?

“Kila mechi ni ngumu na wachezaji wanatambua kazi ya kufanya, tunashirikiana katika kila mechi na kupeana majukumu ya kufanya hilo, linatufanya tuwe tunapata matokeo kwenye mechi zetu tunazocheza.

MECHI YENU DHIDI YA YANGA UNAITAZAMAJE?

“Ni mechi ngumu na kila mmoja anatambua kwamba kila tunapokutana na timu yoyote tunahitaji pointi tatu ambazo zitatufanya tufikie malengo yetu tuliyojiwekea.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu na tunajua kwamba ni timu bora ila tutapambana tucheze tukiwa ni timu, kwani tunazitaka pointi tatu zao, ni muhimu kwetu kama ilivyo kwao.

UNADHANI KUONDOKA KWAKO YANGA KUMEKUINGIZA KWENYE UADUI?

“Hapana sina ugomvi na Yanga, nina marafiki zangu pale na bado tunawasiliana nao kwani mpira siyo vita. Vita yetu sisi ni ndani ya uwanja baada ya hapo maisha yanaendelea, ndivyo ilivyo duniani kote.

UNAJUTIA KUONDOKA YANGA?

“Ni maamuzi yangu mwenyewe kuondoka sikulazimishwa, hapa nilipo nina furaha.

VITA YAKO YA NAMBA NA TSHABALALA IPOJE?

“Naipenda na ni nzuri kwani hata nilipokuwa kulikuwa na ushindani wa namba. Kuhusu kuanza ama kutoanza hilo mimi silijui lipo mikononi mwa mwalimu.

UNAFANYAJE KUWA BORA?

“Mazoezi na kujituma ndani ya uwanja pale ninapopata nafasi na kucheza kwa juhudi nikiwa mazoezini hata kwenye mechi pia,” anamalizia Gadiel.

KUMBUKA Gadiel ndiyo anacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Yanga tangu atue Simba. Huyu hapa anaanza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic