Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kwenda jela aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa miguu ( TFF) , Jamal Malinzi na aliyekuwa katibu wake, Selestine Mwesigwa kulipa faini ya Shilingi laki tano ama kwenda jela miaka miwili huku Selestini akitakiwa kulipa faini mil moja ama kwenda jela miaka miwili.
Aidha, mahakama hiyo imemuachia huru aliyekuwa Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani wa TFF, Flora Rauya kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake.
Hukumu ya Malinzi na wenzake ambao wamesota mahabusu kwa takribani miaka miwili imechukua takribani saa 5 ambapo ilianza kusomwa saa 8 mchana hadi saa 12 jioni.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, Maira Kasonde amesema amepitia ushahidi wa pande zote mbili baina ya utetezi na mashitaka ambapo amewatia hatiani washitakiwa katika makosa mawili kati ya 20.
"Mahakama inaona mshitakiwa wa kwanza na wa pili wana hatia kwa shitaka la tatu na mshitakiwa wa pili ana hatia katika shitaka la nne,"amesema.
Akitoa adhabu Hakimu Kasonde amesema Shitaka la 3 ambalo ni kughushi nyaraka kila mshitakiwa anatakiwa kulipa faini ya laki 5 ama kifungo cha miaka miwili jela na kwa mshitakiwa wa pili katika kosa la nne la kuwasilisha nyaraka za uongo Benki anatakiwa kulipa faini ya Shilingi laki tano ama Jela miaka miwili.
Pia Hakimu Kasonde amesema mahakama hiyo imewakuta washitakiwa hao hawana hatia katika mashitaka 18 ikiwemo la utakatishaji fedha.
Awali kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
Kwa upande wake wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko amedai kuwa washitakiwa hao ni makosa yao ya kwanza kutenda na hawajawahi kushitakiwa.
Awali kesi hiyo ilikuwa na mashtaka 30 lakini ilipofikia katika uamuzi wa kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama la walipunguziwa mashtaka 10 na kubakiwa na mashitaka 20.
Katika hatua hiyo mshtakiwa watano Miriam Zayumba aliachiwa huru kwa sababu alionekana hana kesi ya kujibu kwa mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili.
Kwa pamoja walikuwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 20 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017.








0 COMMENTS:
Post a Comment