Baraza la Soka Afrika Mashariki na Kati ( Cecafa), limemsimamisha mchezaji wa Uganda, Nacakwa Simalei, kuendelea kucheza katika mashindano ya Kombe la Chalenji kwa wasichana wa umri chini ya miaka 17, kutokana na afya yake kutokuwa imara.
Simalei alidondoka na kupoteza nguvu katika mechi dhidi ya Burundi na hali hiyo ilijitokea tena walipoivaa Djibouti.
Taarifa za awali zinaonyesha kuwa mshambuliaji huyo anasumbuliwa na maradhi ya moyo, na hivyo Cecafa inataka kuona anafanyiwa vipimo zaidi ili kutambua tatizo halisi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Cecafa (U-17), Doris Petra, alisema uamuzi huo wa kumsimamisha mchezaji huyo umefanywa na kamati yake kwa faida ya kuokoa maisha ya nyota huyo.
Petra alisema wanaamini vipimo atakavyofanya na matibabu atakayopewa, yataimarisha na kuokoa afya yake na atarejea kuisaida Uganda.
"Hatutaki kuona hali inakuwa mbaya zaidi, imetokea mara mbili kwa mchezaji mmoja, hatujui nini kitatokea siku nyingine, kama ni mchezaji muhimu, anatakiwa kutibiwa kwanza na baadaye ushauri ya kitaalamu kutoka kwa madaktari," alisema Petra.
Mechi atakazokosa mchezaji huyo ni dhidi ya Tanzania Bara ambayo ilichezwa jana jioni na mchezo wa mwisho wa mashindano haya utakaochezwa kesho dhidi ya Kenya.
0 COMMENTS:
Post a Comment