December 31, 2019


PENGINE ni maneno ya mtaani. Pengine Said Ndemla kweli ana kipaji. Nimekuwa na mashaka makubwa sana juu ya kipaji cha mchezaji huyu namna kinavyozungumzwa na namna kinavyoonekana.
Kwa mashabiki wa soka bila kujali itikadi zao, Ndemla anazungumzwa kama moja ya wachezaji wenye kipaji kikubwa sana, lakini kiufundi makocha wengi hawana mpango naye.
Ndemla ni aina ya wachezaji ambao wanapendwa sana na mashabiki, lakini makocha wengi pengine wanamuona wa kawaida sana.
Simba imekuwa ikibadili makocha mara kwa mara, lakini hakuna kocha hata mmoja aliyewahi kumfanya Ndemla kuwa chaguo la kwanza kikosini.
Katika kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni, Simba haijawahi kuwa na kocha mmoja kwa misimu miwili mfulululizo. Kila siku inabadili makocha, lakini kila anayekuja hampi Ndemla nafasi ya kwanza. Lazima kunakuwa na tatizo hapa!
Ingekuwa pale Simba miaka yote kocha ni mmoja angalau ingeeleweka kwamba labda Ndemla siyo chaguo la kocha. Ingekuwa Simba ina kocha mmoja kama Manchester United ilivyokaa miaka 26 na Sir Alex Ferguson, hapo tungepata cha kusema.
Pia kama ingekuwa Simba imekaa na kocha mmoja kama Arsenal walivyokaa miaka 22 na Arsene Wenger, hapo kungekuwa na cha kusema.
Simba ni bandika bandua. Leo wanaweza kuwa na Joseph Omog, kesho wakawa na Patrick Aussems. Inachanganya kidogo, lakini ndiyo ukweli.
Kipaji cha Ndemla kinaonekana zaidi kwa mashabiki kuliko makocha wa Simba. Inachanganya kidogo. Anatajwa kuwa na kipaji kikubwa, uwezo wake wa kukokota mpira na kupiga mashuti ni balaa. Lakini hayo yote hakuna kocha hata mmoja ambaye amewahi kumuamini na kumfanya kuwa chaguo la kwanza. Inaibua maswali mengi.
Kuna kipindi Simba ilikuwa chini ya kocha Pierre Lechantre, Shomary Kapombe aliwahi kutumika kama kiungo wakati, Ndemla akiendelea kuwa benchi. Unapoona kocha anaamua kumtumia mchezaji wa nafasi nyingine kwenye eneo ambalo wewe ni mchezaji asili, ujue kuna jambo haliko sawa.
Simba ingekuwa inaongozwa na kocha mmoja pengine tungesema ni mtazamo wa kocha mmoja. Simba wanapita makocha kila kukicha na kila anayekuja hana muda na Ndemla! Hapa lazima kutakuwa na tatizo kwa mchezaji mwenyewe.
Haiwezekani kipaji kikubwa anachotajwa kuwa nacho kisionekane mbele ya makocha wote waliopita Simba. Makocha wa Simba hawamuoni, makocha wa Taifa Stars hawamuoni.
Ndemla mara nyingi ametajwa kufanya majaribio nje ya nchi, lakini hakuna timu iliyowahi kumsaini. Kuna siasa ambazo huwa zinazungumzwa kwamba eti Simba imekuwa ikimzuia kuondoka! Napata mashaka sana kwenye kauli kama hizi.
Mchezaji ambaye timu yake haimtumii kama mchezaji wa kikosi cha kwanza, Simba wasingemng'ang'ania. Ndemla anapaswa kujitafakari sana yeye mwenyewe. Pengine ameridhika kuendelea kukaa benchi pale Msimbazi. Pengine na yeye anajua kama uwezo wake ni wa kawaida.
Natamani sana kumuona akicheza msimu mzima kama chaguo la kwanza ili kuona kama yaliyomo yamo. Habari za kuendelea kuambiana kama ana kipaji kikubwa wakati makocha wote wanamtupa nje sizitaki kuelekea mwaka 2020.
Mchezaji mwenye kipaji kikubwa ni yule ambaye kile mwalimu mpya anapofika nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza iko palepale. Hakuna mchezaji mwenye kipaji kikubwa asiyetegemewa na timu.
Mashabiki wa soka Tanzania waache kumdanganya Ndemla. Wamueleze ukweli. Hawa makocha wote wanaopita Simba sio wajinga, kuna kitu kinakosekana kwa Ndemla. Anapaswa kupata kocha ambaye ataifahamu shida ya Ndemla na kumsaidia. Hizi sifa za mtaani anazopewa na mashabiki sidhani kama anastahili.
Huwezi kuwa mchezaji bora duniani kwa kukaa benchi. Kama kweli Ndemla ana kipaji kwa mtazamo huo wa mashabiki, basi ni bora akatafuta timu ambayo itampatia nafasi ya kwanza kikosini.
Pengine anapewa sifa nyingi ambazo hastahili. Pengine mashabiki ndiyo wanamuharibu kwa kumfanya ajione yeye mkali sana. Mchezaji mwenye kipaji kikubwa hawezi kukubali maisha yake yote ya soka yale ya kutokea benchi. Hayupo mchezaji wa aina hiyo.
Kubadilika kwa makocha mara kwa mara ndani ya Simba na hakuna aliyekuja na kuona ukubwa wa kipaji cha Ndemla, kunanipa wasiwasi mkubwa juu ya uwezo wa mchezaji huyu.

8 COMMENTS:

  1. Kwa mawazo yangu.. Ni kweli Ndemla ana kipaji tena kikubwa sana sema kuna vitu hatoi kama wanavyo toa kina Mkude, Fraga, Muzamiru, Chama na Shiboub, hawa wote ni viungo wa kati, ukiacha Dilunga, Kanda, Kahata na Miraji ambao ni winga au viungo wa pembeni. Ukimuangalia Ndemla kuna wakati hayupo uwanjani anapotea....lakini hao waote wako vizuri mda wote wa mchezo. Nafikiri inabidi ajiangalie wapi anakosea ili apate namba. Ajibu nae kama ataendelea na tabia ya kuzurura uwanjani basi nae atakua kama Ndemla. Wapamnane wakipewa nafasi ili wamvutie mwalimu awe anawapa nafasi. Muzamiru na Chama wamebadilika sanaa... wawaige.

    ReplyDelete
  2. Zungumzia kuhusu kipaji cha Ndemla ila unapojikanyaga kuzungumzia suala la Simba kubadilisha makocha hapo ndipo unapojitekenya mwenyewe na kucheka mwenyewe. Azam na uchanga wake ndani ya mwaka mmoja hubadalisha makocha mara ngapi? Yanga wamebadilisha makocha mara ngapi? Tangu aondoke Ferguson Manchester wamebadilisha makocha mara ngapi? Tangu aondoke Wenger pale Arsenal makocha wangapi wanaingia na kutoka. Kubadilisha kocha sio dhambi kwa klabu yenye uchu wa mafanikio na ndio maana Liverpool wanacheka hivi sasa. Tofauti na imani za kijinga ya kwamba hata kama kocha haitendei haki kazi yake basi aachiwe tu kwa sifa za kwamba timu fulani inakaa na makocha. Ndemla kama vijana wengine wa kitanzania utajiri wanao lakini wanasubiri miujiza kuja kuleta maajabu yake na kuja kuwatajirisha kuliko kuekeza katika kujituma na kufanya kazi kwa bidii na kutenda miujiza na kwa vijana wetu hawa wasipobadilika hata waletewe Guadiola sio rahisi kutoka.

    ReplyDelete
    Replies
    1. wewe ni mwehu, umeona popote mwandishi analaumu kwamba kwa nini simba wanabadilisha makocha?? wabongo sijui lini tutakua na utulivu kwenye details!! ni mihemko tu ndo inatuendesha. kubaki kweny fact limekua tatzo sugu na hasa kwa mashabiki uchwara wa simba kama ww. shenzi kabisa. badala upongeze hii makala nzuri itamzindua kijana akiwashe kwa mafanikio yake na klabu yake, wewe unaanza kuleta upuuzi wako apa.

      Delete
  3. You nailed it Dina la kuo ngeza.Makanjanja utafikiri Ndemla ndio mchezaji pekee asiyepata namba.KMC wanatafuta kocha kama una credentials wewe mwandishi waandikie wakuajiri.Makocha ndio waamuzi wa mwisho wa nani acheze.

    ReplyDelete
  4. Makala imeeleweka hata haihitaji ufafanuz zaidi ya hapo, Ndemla fanyia kazi hayo.

    ReplyDelete
  5. Hi makala kafanya kuikop na kuiweka humu aonekan yy ndie mwandish....sikiliz bro mpira wa simba ni pasi fupi na ndemla ni mtu wa long pass sio kwamba haendan na simba la hasha ila kila mechi ina mbinu zake na wachezaj wanao hitajika.....mbona kipind cha masoud juma ndemla alicheza sana sababu gani pace ya okwi na kichuya....halaf kuhus majiribio nje hakuna pande yyt iliyowah kutuweka waz either simba, ndemla au huko alipofaya trial kwahy tusikae kwa kuhisi t....m ni fan namba moja wa ndemla na naumia nnapo mwena bench but siwez pinga mbinu za mwalimu

    ReplyDelete
  6. Muandishi anataja kubadili makocha kwa lengo zuri tu soma. Post vizuri, anamaanisha simba ingekuwa na kocha mmoja tu kwa muda mrefu halafu hampangi NDEMLA tungekuwa na sababu labda kocha anambania au hampendi lakini kila kocha anaeingia simba bado hampangi Ndemla, wote walioingia na kutoka simba hawajamweka Ndemla kikosi cha kwanza, maana yake Ndemla ana tatizo lake mwenyewe, si makocha waliopita hapo

    ReplyDelete
  7. Leo kapewa nafasi. Aitumie. Makanjanja huwa wanaimba kocha asiingiliwe.Akipanga wachezaji anaona wanafaa kwa gemu plan yake basi makala haziishi za kuuliza mantiki ya kumpanga au kutompanga mchezaji fulani.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic