LIVERPOOL YANUSA UBINGWA, GUARDIOLA AGOMA
LIVERPOOL wameingia kwenye kipindi cha mwezi Desemba wakiwa mbele kwa tofauti ya pointi 11 dhidi ya wapinzani wao wakubwa kwenye mbio za ubingwa wa Premier, Manchester City wakiwa na nafasi kubwa zaidi ya kuutwaa msimu huu, lakini Kocha wa City, Pep Guardiola amedai bado nao wana nafasi.
Liverpool ina pointi 40 kileleni huku Man City wakiwa na pointi 29, katika historia ya Premier hizo ni pointi nyingi zaidi kihistoria baada ya mechi 14, na timu zote mbili ambazo awali zilifikisha pointi hizo ndani ya mechi hizo zilitwaa ubingwa, ambazo ni Tottenham 1961-62 na Man City 2017-18.
Leicester kama walishinda jana, watakuwa wamebakiza pointi nane waifikie Liverpool lakini hawaonekani kuwa wapinzani wakubwa wa ubingwa.
Liverpool juzi walifanikiwa kuwachapa Brighton mabao 2-1 kwenye mchezo ambao walipata pigo baada ya kipa wao Alisson Becker kupewa kadi nyekundu.
“Tunaonekana kuendelea vizuri, lakini wigo wa pointi kwenye Ligi Kuu England mara nyingi huonyesha tofauti kwenye mchezo wa mwisho, hivyo ni vyema tukasubiri,” alisema kocha wa Liverpool, Juggen Klopp.
Guardiola alipoulizwa kama anaamini sasa vita ya ubingwa imeisha, alisema: “Tuna mpinzani mwingine mbele yetu, sasa tunatakiwa kujaribu kushinda michezo, kushinda michezo na kuona kitakachotokea.
“Nilisema jana kuwa siyo wazo zuri kufikiria kuhusu Premier au kufikiria pointi nyingi ulizoachwa.
Tunatakiwa kushinda michezo, kushinda michezo, na unapokuwa hushindi, itakuwa ngumu zaidi.”
0 COMMENTS:
Post a Comment