December 20, 2019








 Na Saleh Ally
MWAKA 2016, Kampuni ya EDF Luminus ilisaini mkataba wa miaka minne na Klabu ya KRC Genk ili jina lake la Laminus litumike kama jina la uwanja wa klabu hiyo.


Laminus ilikubali kumwaga kitita cha euro 680,000 kila mwaka ili kuweza kulitumia jina hilo kama jina la uwanja wa klabu hiyo ya KRC Genk.

Kampuni hiyo ndiyo kubwa ya pili katika zile zinazozalisha umeme, ndio namba moja kwa kuzalisha umeme nchini Ubelgiji na wamiliki wenye hisa nyingi katika hiyo ni Wafaransa kupitia kampuni yao ya umeme ya Electricite de France ambao wana 68.6%.

KRC Genk ndio klabu ambayo Mtanzania, Mbwana Samatta anakipiga na msimu huu aliiongoza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ikiwa kundi moja na vigogo Liverpool, Napoli na Salzburg.

Wadhamini hulazimika kulipa kitita cha fedha ili kuweka majina ya kampuni zao kwa kuwa kupitia klabu yanaweza kujitangaza vizuri.

Mfano ni mkataba kati ya Shirika la Ndege la Emirates la Dubai na klabu maarufu ya Arsenal ya England ambayo iliongezewa takribani pauni milioni 86, ili jina la Emirates litumike katika uwanja wao mpya.

Unaona mkataba wa jezi kati ya Arsenal na Emirates unaisha mwaka 2024 lakini mkataba wa uwanja wenyewe utakwenda hadi mwaka 2028, Arsenal ikiendelea kuingiza mamilioni kutokana na uwanja wake kutumika.

Kwa upande wa Manchester City wao wana mkataba wa jezi na Shirika la Ndege la Abu Dhabi la Etihad, ambao kupitia jezi lakini pia uwanja wanachukua hadi dola milioni 350 na ushee. Imeelezwa kila mwaka, dola milioni 4 imeongezwa kwa ajili ya jina la uwanja.


Hapa nyumbani, hivi karibuni Simba ilifanikiwa kutengeneza uwanja wake wa mazoezi katika eneo la Bunju. Uwanja huo, ndani una viwanja viwili, kimoja cha nyasi asili, kingine bandia.

Simba wakafikia uamuzi wa kuuita uwanja huo, Simba Mo Arena. Jambo ambalo niliamini naweza kutoa ushauri na Simba wakikubali wakaingiza fedha zaidi kupitia viwanja hivyo.

Simba Mo Arena, ilinishangaza kidogo kwa mambo mawili na inawezekana kwa anayelenga biashara anaweza kukubaliana nami, kuwa kuna jambo la kufanya na hasa unapozungumzia biashara na maendeleo ya baadaye.

Kuuita uwanja huo Arena, nilidhani ingekuwa Complex. Arena inabeba maana tofauti kidogo, sawa na kusema uwanja mkubwa ambao utakuwa ukitumika kwa mechi na kadhalika.


Kwa uwanja wa mazoezi kuwa Complex, huenda jina lingebadilishwa baadaye baada ya kuwa umekamilika. Hata hivyo, hii si ishu kubwa sana.

Ishu nilimiani, Simba wangeangalia biashara zaidi. Kutumia jina la Mo ambaye ni mwekezaji, sehemu ya wamiliki wa timu si sahihi kwa kuwa hii ni biashara na inajumuisha wamiliki tofauti.

Wamiliki upande wa uwekezaji na upande wa wanachama. Inawezekana kabisa upande wa wanachama wanaomiliki asilimia kubwa, wawakilishi wao kama viongozi, hawakuwa wakijua kuwa jina tu linaweza kuwa chanzo cha mapato, au walijua lakini hawakulitilia maanani.

Kama Genk, Arsenal, Man City na wengine wanalipwa kwa hilo, vipi Simba isilipwe? Kweli muwekezaji Mohamed Dewji maarufu kama Mo Dewji amesaidia sehemu kadhaa, lakini ninaamini kuna sehemu anakopesha.

Kuna sehemu nyingi Simba wanaweza wakaonyesha fadhila kwake lakini wakati wakitumia uwanja huo kama sehemu ya biashara.

Kama ni fadhila, ingekuwa ni chaguo, mimi ningechagua uitwe Dalali Complex ambaye alinunua kiwanja wakati wa uongozi wake. Ndio maana leo Simba wameweza kujenga uwanja na unaona wakati wa Evans Aveva ndio nyasi ziliagizwa. Hivyo vizuri ingekuwa ni biashara zaidi badala ya fadhila.

Unaona Simba, sasa inaendeshwa kibiashara zaidi. Mambo mengi yanabadilika na biashara inakuwa ndio mlango sahihi wa Simba kwenda katika mafanikio.

Sijajua waliopitisha kama ilikuwa katika ufafanuzi sahihi, au ilikuwa mbiombio na niliona kosa kwa wanachama kutumika kupitisha jina la uwanja hata kama ingekuwa ni Dalali Stadium.

Jina hili, lingeachwa kwenye upande wa masoko wa Simba ambao ungepiga hesabu katika masuala kadhaa kama kuuza jina la uwanja ili kuingiza fedha kila mwaka lakini kuzungumza na makampuni kadhaa ambayo mabango yake yatakaa katika uwanja huo na kuiingizia Simba fedha.


Kuna mabenki, makampuni ya vyakula, makampuni ya simu na makampuni mengine mbalimbali ambayo yana hamu ya kujitangaza.

Pamoja na hivyo, kama Mo atalipa kiasi cha fedha kupitia bidhaa zake, bado kuna nafasi ya kulitangaza jina lake na vizuri ijulikane kuwa ni mkataba wa muda gani.

Angalia ingekuwa CRDB Simba Complex, Vodacom Simba Training Ground, Azania Simba Complex na kadhalika, ingekuwa ni mwendo wa sahihi zaidi wa kibiashara na faida zaidi kwa Simba kwa kuwa wangeendelea kuingia kwenye njia sahihi ya kujitegemea zaidi badala ya kuendelea kubaki moja ya klabu zinazoishi hadi kuwe na huruma.




13 COMMENTS:

  1. Wamekusoma; subiri waje na hoja zao

    ReplyDelete
  2. Very good and valid point.Japo naamini kipindi Magori akiwa kiongozi upande wa wanachama hili lisingewezekana fasta fasta hivi...
    All the best mtani.

    ReplyDelete
  3. Mo kaujenga bure pia kaongezea billion 1 kwenye bajeti ya klabu acha tumuenz

    ReplyDelete
  4. Kinachooneka hapa Simba hawajui thamani ya Club yao ukilinganisha na utajiri wa Mo. Kinachoendelea sasa ndani ya Simba ni kwamba hatima na maamuzi yote ya Club yapo chini ya Mo. Aliyeamua Aussems atoke ni Mo, anayeamua Wabrazil wabaki ndani ya Simba ni yeye. Hamna anayejua kitakachotokea kesho kwa Simba. Wapenzi wanasikilizia tu kocha ameletwa kocha amefukuzwa. Wanashindwa kufahamu thamani yao kama mashabiki na wanachama walioenea nchi nzima. Hicho ndicho Club za Tanzania ikiwemo Yanga wanashindwa kutegua mtego wa kuwa Club kubwa Africa. Mwl Nyerere aliwahi kuwaambia Watanzania ni heri kuendelea kuwa maskini kuliko kuruhusu madini/rasilimali za nchi zikachezewa na watu na kutuachia mashimo. Simba/Yanga zitambua ukubwa wa utajiri walionao na thamani yake. Nawaangalia wapenzi wa Simba nabaki kushangaa. Hivi tumelogwa nini sisi? Eti uwanja unaitwa Mo Simba Arena!!@@. Jamani kizazi hichi cha wasomi kinawezaje kuruhusa haya yatokee. AIBU! Naamini hakuna shabiki wa Simba anayeafiki jina hilo kutoka moyoni. Lakini wamepumbazwa na kujiona wao hawana kitu ni maskini!! Hilo limetokea wakati wapenzi wengi wa Simba hawaelewi kisa kilichomwondoa Aussems. Hivi Aussems na wachezaji Wabrazil kwa kulinganisha na alikuwa na mchango ndani ya Simba. Lakini kwa kuwa alionekana tishio la kuwaambia viongozi ukweli na kutishia maslai ya mtu ndani ya Club akatolewa Kafara. Huwezi kuamini leo wanachama wote wa SIMBA wanashindwa kuwa na sauti na kuamua hatma ya Club???

    ReplyDelete
  5. Kwanza kabisa tukubaliane watu wa Simba ni majasiri kulinganisha na wale wa mtaa wa jirani. Wanasimba kama wangekubali upumbavu na blah blah nyingi za waliokuwa wakimuekea figisu Mo basi mpaka leo hii ni wa kuonewa huruma kwa unyonge,yaani hata hivyo viwanja tunavyovizungumzia hapa visingekuwa vimesimama. Viwanja vya Simba ni maeneo ya wazi bado vipo kwenye process au mikakati ya kuendelezwa ili kuwa viwanja kamili ila inashangaza kuona watu wembeni wakitijitia viherehere na kujifanya wanauchungu na klabu ya simba kuliko wanasimba wenyewe.La msingi hapa hata shetani iblisi anapoona wivu juu ya mafanikio ya mtu fulani na kutaka kumuharibia basi atamjaza mtu huyo na mawazo ya tamaa au shetani anaweza kwenda mbali zaidi kwa kujifanya mwanadamu mwema na kumuibukia mtu laivu kama mtu mwenye busara ila shetani ni shetani na tumeshashuhudia mawazo mengi ya kishetani kutoka kwa watu wanaojifanya wanaitakia mema Simba ila wanasimba si wapumbavu.Simba hawezi kulegeza kamba kwenye mfumo wao wa kujiendesha wa sasa chini ya Mo kama mfumo wa timu ya wananchi kula kukicha ni matatizo matupu. Saleh jembe atatoa mawazo yake ila ndani ya Simba kuna watu makini zaidi na weledi wa Mambo kuliko yeye na hawawezi kuwapangia Simba nini cha kufanya.simba ni taasisi kubwa na kama kuna watu wanaifanya Simba kuwa ni taasisi kubwa basi Mo ni moja kati ya watu hao muhimu kabisa kuwahi katika historia ya simba.

    ReplyDelete
  6. me nilitaka tu kujua timu gani ambayo mnaijua kubwa au ndogo ambayo inauwanja wa mazoezi na umezaminiwa hapa duniani mwandishi katolea mfano viwanja kamili na sio vya mazoezi kwani mifano ya Genk Man city na Asenal hazina viwanja vya mazoezi vinafanyia kwenye viwanja vyao vikubwa suala hapa analo ongea saleh ni siasa tu na polojo uwanja bado upo kwenye process na haujakamilika walichofanya ni kupunguza gharama za kukodi viwanja ungekuwa uwanja kamili na mkubwa nimgeunga mkono ila kwa hili hapana sio sahihi

    ReplyDelete
  7. Haina validity yoyote mbwembwe nyingi tu. Huo uwanja MO kajenga kwa pesa yake wala sio wajibu katika uwekezaji.

    ReplyDelete
  8. Makubwa na tutabaki ombaomba hadi

    ReplyDelete
  9. Wovuuuu amayetaka kuweka tangazo anaruhusiwa hata ulivyotolea mfano vinamatangazo mengine tofauti na mdhamini mkuu,ushauri wako peleka yanga

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic