December 20, 2019





 NA SALEH ALLY
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amefanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).


Karia ataiongoza Cecafa kwa kipindi cha miaka minne na baada ya hapo kutakuwa na uchaguzi tena katika nafasi hiyo.


 Mwendo wa Cecafa mara nyingi umekuwa ukitegemea nchi mbili zaidi kwa kipindi kirefu sana, nazo ni Tanzania na Rwanda.


Rwanda imedhamini michuano ya klabu bingwa ukanda huu wa Cecafa kupitia rais wao Paul Kagame, ndiyo maana michuano hiyo inajulikana kama Kagame Cup.


Pamoja na hivyo, Rwanda imekuwa ikikubali mara kwa mara kufanyika kwa michuano hiyo kwenye ardhi yake.


 Tanzania nayo kupitia TFF imekuwa ikiisaidia sana michuano ya aina tofauti ya Cecafa. Kuanzia ile ya nchi, klabu lakini usisahau ya vijana na wanawake.
Hii inatokana kwa kiasi kikubwa na Tanzania kuongoza kwa kuwa na mashabiki wengi zaidi wanaoupenda na kuufuatilia mchezo wa soka.


Nchi ambazo zimekuwa zikichukua michuano hiyo kama nilivyosema Tanzania na Rwanda. Mwisho zimekuwa zikiingia kwenye madeni makubwa baada ya kwisha kwa michuano hiyo.


Hakuna ubishi, Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amekaa katika kiti chake au ndani ya baraza hilo kwa zaidi ya miaka 20 na ameendelea tu kuongoza huku wakibadilika aina mbalimbali ya marais kutoka katika nchi mbalimbali.


Mara nyingi, Musonye huangalia penye nafuu na msaada wa kulisaidia baraza hilo kuendelea kupata msaada ili liendelee kuishi.


Mawazo ya Musonye yamekuwa yaleyale. Anayetaka mambo yaende kwa aina ileile na ninaamini mtakubaliana nami, thamani na umaarufu wa michuano ya Cecafa hata ile ya Kagame imepitwa na wakati na imeshuka umaarufu.
Hii inatokana na mambo matatu makubwa ambayo, moja ni kukosa ubunifu, pili siasa nyingi ambazo zinaendana na kuangalia nani anataka nini na mwisho, ubinafsi unaotokana na matakwa binafsi na namna watu wanavyofaidika.


 Ndiyo maana nimekuwa nikiona hakuna faida kubwa ya kuwabadilisha marais katika baraza hilo kila baada ya kufanya uchaguzi wakati Musonye anaendelea kubaki hapo.


Kubaki kwake maana yake mengi ambayo yatakuwa mapya yataendelea kuonekana hayafai na inawezekana akawa tofauti na mwendo wa wale wanaoingia.


Kama Musonye ataona walioingia wanakuwa na mambo tofauti ambayo hayana faida kwake, hawezi kuyapa nafasi hasa kwa kuwa yeye ndiye mtendaji mkuu wa baraza hilo na anashughulikia mambo mengi zaidi ya watu wengine.


Nimekuwa nikishangazwa sana na mfumo wa Cecafa ambao unamruhusu mtu mmoja kuweka mizizi yake kwa muda mrefu.



Hii ni kama ilivyokuwa kwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na lile la kimataifa (Fifa) namna Issa Hayatou na timu yake na Sepp Blatter na kikosi chake walivyolazimika kubaki madarakani milele hadi walipoondolewa kwa nguvu kama majambazi.



Soka ni mchezo wa watu, mchezo wa wanajamii na wakati mwingine una nguvu hata baadhi ya serikali au marais wa nchi na ukumbuke nguvu yake ni watu. Hivyo katika uongozi wake, lazima watu wapewe nafasi ya kuleta mambo mapya kuendana na mabadiliko.


Alichokifanya Musonye kimetosha, apongezwe na hicho na baada ya hapo Cecafa ipate katibu mkuu mpya badala ya kuruhusu tuone marais miaka  mia moja, Musonye mmoja na mawazo yaleyale.


Inawezekana hata wadau wengi wa Cecafa wamekuwa wadau wa Musonye, hii maana yake wengi walio ndani ya Cecafa nao wanaishi kwa maslahi zaidi yanayowagusa badala ya mpira wenyewe.





1 COMMENTS:

  1. Umezungumza vizuri kabisa. Lakini mbona hata sisi tusio waandishi, tusio na ujuzi kufanya uchunguzi wa taarifa, ambao tunategemea taarifa toka kwenu mbona tunajua Musonye anaondoka? Mbona ni taarifa zilizo wazi kwamba alikuwwa anasubiri Challenge na Uchaguzi viishe ndipo aaichie ngazi? Ina maana hata hili dogo tu kweli blog ya heshima kama hii imeshindwa kuzifahamu?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic