December 22, 2019


Leo Jumapili, kutakuwa na mechi ya wenyeji Tottenham Hotspur dhidi ya Chelsea. Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Tottenham kuanzia saa 1:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Ni mchezo wa Ligi Kuu England maarufu Premier, ambapo itawakutanisha watu wawili ambao mmoja ni mwalimu na mwingine mwanafunzi.

Jose Mourinho akiwa na kikosi chake cha Tottenham maarufu Spurs, anakwenda kukutana na Frank Lampard ambaye anainoa Chelsea.

Wawili hawa walikuwa pamoja kwenye kikosi cha Chelsea kwa vipindi viwili tofauti ambapo Mourinho alikuwa kocha na Lampard mchezaji wake tegemeo kwenye nafasi ya kiungo.

Lampard aliitumikia Chelsea kama mchezaji kuanzia mwaka 2001 hadi 2014, huku Mourinho akiinoa Chelsea kuanzia mwaka 2004 hadi 2007, kisha akarejea tena kikosini hapo na kuwa kocha mwaka 2013 hadi 2015.

Katika mchezo huu, kila mmoja atataka kuonyesha makali yake ukizingatia kwamba, Chelsea imetoka kufungwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Bournemouth, huku Spurs ikiinyuka Wolverhampton mabao 2-1.

Rekodi zinaonyesha kuwa, timu hizo zimekutana jumla mara 164. Chelsea imeshinda mechi 70, Spurs imeshinda 54 na sare 40.

Katika mechi tano timu kukutana kwao, Chelsea imeshinda mbili, Spurs imeshinda tatu. Hakuna sare.

Matokeo ya mechi hizo ni Chelsea 1-3 Tottenham, Tottenham 3-1 Chelsea, Tottenham 1-0 Chelsea, Chelsea 2-1 Tottenham na Chelsea 2-0 Tottenham.

Vikosi vyote vina majanga na vinatarajiwa kuwakosa wachezaji wao kadhaa kutokana na majeraha.

Spurs itawakosa Hugo Lloris, Erik Lamela, Michel Vorm, Ben Davies na Tanguy Ndombele.

Upande wa Chelsea, itawakosa Fikayo Tomori, Ruben Loftus- Cheek na Olivier Giroud.

Mourinho amekiangalia kikosi chake, kisha akakitazama kile cha Chelsea, akafungua mdogo wake na kusema anawahofia sana Chelsea.

“Kwa mara ya kwanza nimekuwa na uoga wa mechi kubwa. Chelsea wana kikosi kizuri chenye vijana wengi kama Willian na Kante.

“Frank ameanza vizuri kuinoa Chelsea lakini kwa bahati mbaya amepoteza mechi kubwa mara mbili dhidi ya Man United, wakafungwa nyumbani na Liverpool, lakini pia wakapoteza mbele ya Man City.

“Nikiwatazama, naona kabisa wana timu nzuri ambayo ni ya muda mrefu zaidi. Wanaweza kutupa shida.”

Katika msimamo wa Premier, timu zote zimecheza mechi 17, Chelsea iponafasi ya tatu ikiwa na alama 29, Spurs ina alama 26 katika nafasi ya tano.

Spurs ikishinda inaishusha Chelsea kwani licha ya kwamba zote zitakuwa na alama 29, lakini Spurs itakuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

LONDON, England

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic