BAADA ya msanii, Godfrey Tumaini ‘Dudu Baya’, kufungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kushiriki shughuli za sanaa kwa kutoa lugha zisizo na maadili, ameibuka na kusema yuko tayari kuliburuza baraza hilo mahakamani kama kweli limemfungia.
Dudu Baya alisema jana kuwa, bado hajapokea barua yoyote ya kufungiwa kutoka Basata na amesisitiza kuendelea kutumbuiza.
Basata juzi ilitangaza kumfutia usajili msanii huyo baada ya kutoitika wito wa kufika katika ofisi za baraza hilo kwa ajili ya kutoa maelezo ya kina kuhusiana na lugha zisizokuwa na maadili anazodaiwa kuzitoa kupitia video fupi aliyorusha kwenye mtandao wa kijamii.
Akiandika jana kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Dudu Baya alisema ataendelea kufanya shoo na shughuli zote za sanaa na atakapopata barua ya kufutiwa usajili ataungana na mwanasheria wake kujua ufumbuzi wa suala hilo.
“Nikipata barua nitakaa na mwanasheria wangu kujua kilichoandikwa ndiyo tutakwenda mahakamani, naamini serikali ya awamu ya tano ni ya haki nitashinda tu,” alisema.
Dudu Baya pia alitishia kuhama nchi na kwenda kufanya shughuli zake za muziki nchini Uganda endapo ataona longolongo zinazidi dhidi yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment