January 13, 2020



2020 ndo inaanza kumeguka nayo taratibu endapo mipango haitakuwa sawa unaweza kushtuka upo mwaka 2021 bila kutegemea iwapo neema ya Mungu itakuangazia.

Yote kwa yote napenda kukutakia kila la kheri ndugu msomaji kwa kuanza mwaka mpya 2020 na leo ikiwa umefungua ukurasa wa 13 ndani ya mwezi Januari ndivyo siku zinazidi kukatika.

Kwenye kalenda ya matukio kimichezo kuna mengi ambayo yanatarajiwa kufanyika ndani ya mwaka huu hii hapa  orodha ya baadhi ya yale matukio ambayo yatafanyika 2020 yatakuwa namna hii:-

Kombe la Mapinduzi

Azam FC walikuwa ni mabingwa watetezi wa Kombe hili ila walitolewa na Simba kwenye hatua ya nusu fainali kwa penalti 3-2 baada ya dakika tisini kutoshana nguvu ya bila kufungana.

Leo  Michuano hii ambayo ilianza  kutimua vumbi Januari, 6,2020 na inafika tamati leo Januari 13,2020 ambapo Mtibwa Sugar itamenyana na Simba.

Ilianza kwa  makundi mawili ambapo kundi A lililokuwa na  Yanga, Azam FC, Mlandege na Jamhuri  liliweka ngome Visiwani Unguja na zilitumia Uwanja wa Amaan.

Kundi B lilikuwa  Pemba lili jumuisha timu za Simba, Mtibwa, Chipukizi na Zimamoto  zilitumia Uwanja wa Gombani.

Ni moja ya tukio muhimu ndani ya mwaka mpya 2020, uwepo wa Simba na Yanga uliongeza presha kwa bingwa mtetezi Azam FC iliyo chini ya Arstica Cioaba ambapo alishuhudia timu hiyo ikipigwa chini hatua ya nusu fainali.


Michuano ya Afcon

Mwaka 2020 timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars itakuwa na kazi ya kutafuta tiketi ya kuwania kufuzu michuan ya Afcon inayotarajiwa kufanyika mwaka 2021 nchini Cameroon.

Mechi sita zinatarajiwa kuchezwa ili kupata timu itakayoshiriki michuano hiyo mikubwa Afrika, bingwa mtetezi ni Algeria ambaye alimfunga Senegal kwenye fainali ya michuano hiyo iliyofanyika 2019 nchini Misri.

Tayari Stars iliyo chini ya Etienne Ndayiragije imecheza mechi mbili ikiwa kundi J pamoja na Tunisa ambao wanaongoza kundi wakifuatiwa na Libya. Stars ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi zake tatu na nafasi ya nne ipo kwa Equatorial Guinea.

Mechi zake zitakuwa nammna hii:-31/08/2020, Tunisia v Tanzania , Tanzania v Tunisia 08/09/2020, 05/10/2020 Equatorial Guinea v Tanzania na 9/11/ 2020 Stars itamenyana na Libya, 31/08/2020.

Hapa Stars ikishinda na kufuzu michuano hii mikubwa itakuwa ni mara yake ya tatu kushiriki baada ya mwaka 2019 kuboronga ilipopata nafasi nchini Misri kwa kushindwa kuambulia pointi, kazi itakuwa kufuta makosa ya wakati uliopita.

Michuano ya Chan

Timu ya Taifa ya Tanzania imefanikiwa kufuzu michuano ya Chan ambayo inawahusisha wachezaji wa ndani. Michuano hii inatarajiwa kuanza Aprili 4-25 nchini Cameroon. Awali ilitarajiwa kufanyika mwezi Januari mpaka Februari ila ratiba zikabadilishwa.

Timu 16 zimekata tiketi ya kushiriki michuano hii ikiwa ni pamoja na Cameroon hawa ni waandaaji wa michuano hii nchi nyingine ni Congo, DR Congo, Rwanda, Uganda, Morocco, Tunisia, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Guinea, Mali, Burkina Faso, Niger na Togo.

Ligi Kuu Bara

Mwezi Mei, 24 inatarajiwa kufika ukingoni kwa timu zote kucheza raundi ya 38 Ligi Kuu Bara kwa mwaka 2019/20 ambapo bingwa mtetezi ni Simba aliyetwaa msimu uliopita baada ya kufikisha jumla ya pointi 93 kwenye jumla ya mechi 38 na Yanga ilimaliza ikiwa nafasi ya pili na pointi zake 86 Azam ya tatu na pointi 75 KMC ilimaliza ikiwa nafasi ya nne na pointi 55.

Kwa sasa ushindani umezidi kupamba moto ligi ikiwa bado ipo mzunguko wa kwanza, vita ya ubingwa imekuwa kwa timu tatu ambazo zilimaliza ligi msimu uliopita zikiwa nafasi ya juu ambazo ni Simba iliyo nafasi ya kwanza na pointi zake 34 huku Azam ikiwa nafasi ya pili na pointi zake 26 zote zimecheza mechi 13 na Yanga iliyomaliza nafasi ya tatu kwa sasa ipo nafasi ya 7 ikiwa na pointi 25 ila ina mechi mbili mkononi kuwa sawa na timu  zilizo nafasi ya juu.

Pia vita kubwa ya kushuka daraja ni kubwa kwa kuwa timu nne zitashuka jumla msimu huu na mbili zitacheza playoff na timu zile zitakazomaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Singida United, Ndanda FC, Mbeya City na KMC zimekuwa na mwendo wa kusuasua msimu huu zisipobadili gia mapema zigo la kushuka daraja litawahusu huku vita ya ubingwa ikizidi kupamba moto.

Kombe la Shirikisho

Kwa sasa ipo hatua ya 32 michuano hii inatarajiwa kuendelea kutimua vumbi mwaka huu 2020 na bingwa mpya atapatikana atakayetwaa kombe hili.

Kwa sasa Kombe lipo mikononi mwa Azam FC ilitwaa kombe hilo baada ya kuifunga Lipuli kwenye mchezo wa fainali.Bingwa wa michuano hii anapata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Huku pia mwaka 2020 ushindani unatarajiwa kuwa mkali baada ya vigogo Simba kuvuka kigingi cha kwanza cha hatua ya 32 bora ilichoshindwa kuvuka mwaka 2018 kwa kufungwa mabao 3-2 na Mashujaa FC  ya Kigoma , Uwanja wa Taifa.

Yanga nao wamo kwenye hatua ya 32 jambo ambalo litazidi kunogesha michuano hii ambayo inatarajiwa kuendelea mwezi Februari na kufika tamati kati ya mwezi Mwezi Aprili kati ya tarehe 24-26.

Uchaguzi Mkuu

Oktoba 25,2020 uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika ambapo familia za wanamichezo zitatupa kete zao kuwachagua wale wanaowahitaji. Upepo unaonekana kubadilika ambapo Josepph Haule,’Proffessor Jay’ Mbunge wa jimbo la Mikumi na Joseph Mbilinyi, ‘Sugu’ mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini hawa ni wasanii ambao wanapeperusha bendera pia kwenye siasa huenda wakarudi tena majimboni mwao kuomba ridhaa ya kuchaguliwa.
Ibrahim Mussa maarufu kama Roma ambaye yeye ni msanii pia anatajwa kuingia kwenye siasa na huenda mwaka huu 2020 akagombea ubunge baada ya kuimba nyimbo nyingi za harakati ikiwa ni pamoja na Mathematics, Zimbabwe na Mr President.

Mashindano ya Kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika

Kwa upande wa mpira wa kikapu, 2020 kutakuwa na mashindano ya kufuzu kwenda kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika itakayofanyika mwaka 2021. Michuano hii inatarajiwa kuanza kufanyika Januari 14-18 nchini Kenya ambapo timu ya Taifa ya Tanzania ya kikapu itashiriki mashindano haya.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic