WAKATI mshambuliaji wa Aston Villa, Mtanzania, Mbwana Samatta kesho akitarajiwa kucheza dhidi ya Tottenham Hotspur inayofundishwa na Kocha Jose Mourinho, staa huyo amepewa mbinu maalum za kuifurahisha timu yake na kumkera Mourinho.
Samatta amejiunga na Aston Villa kwa mkataba wa miaka minne na nusu akitokea KRC Genk ya Ubelgiji ambapo kesho Jumapili atacheza mchezo wake wa pili katika Ligi Kuu ya England dhidi ya Spurs, mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Bournemouth ambapo alifunga bao moja wakati timu yake ikichapwa 2-1.
Baba mzazi wa staa huyo, mzee Ally Samatta alisema kwa sasa ndiyo wakati wa mtoto wake kuionyesha dunia kwamba Tanzania kuna wachezaji wengi kufuatia kupata nafasi ya kukutana na watu mashuhuri kwenye mchezo huo akiwa kwenye ligi ya England huku akimtaka ahakikishe timu yake inapata matokeo mazuri.
“Kwanza namu ombea ikitokea anacheza basi aweze kufanya vizuri kwa kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya hao Spurs lakini nitataka ajue kwamba ubora wake ndiyo fursa nyingine kwa wachezaji wetu wa hapa kwa kuwa atakuwa anafungua milango ya kuamini Tanzania soka lipo.
“Siku zote kabla ya mechi huwa tunawasiliana na huu niliokuambia wewe utakuwa ujumbe wangu kwake, ahakikishe anakuwa msaada kwenye timu lakini aweze kuitangaza nchi maana huko anakutana na watu wakubwa wengi, sasa ni muhimu awaambie kwa vitendo,” alisema mzee Samatta.
0 COMMENTS:
Post a Comment