UONGOZI wa Mwadui FC ya Shinyanga
kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Ramadhan Kilao amesema timu yake imekuwa
ikiendelea na mazoezi ya wachezaji wake kujiweka fiti ili ligi itakaporejea
wote wawe kwenye kiwango bora kwa kuwa hawako vizuri katika msimamo wa Ligi Kuu
Bara msimu huu.
Kilao
amesema: "Wachezaji wetu kiukweli wamekuwa wakiendelea na mazoezi binafsi nyumbani, kocha wetu Khalied Adam aliweka utaratibu wa kila mchezaji kufanya
mazoezi binafsi.
“Lengo ikiwa ni wachezaji wetu
waendelee kuwa fiti na hilo tumelifanikisha, kwani karibia kila siku tunapata
ripoti ya kocha wetu kwa namna wanavyoendelea na mazoezi yao.
"Kocha wetu kwa sasa yuko likizo
na tumefanya hivyo kwa sababu hata kambini hatuna wachezaji, tumewapumzisha
kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.
“Pamoja na hivyo, huko aliko kwa
kushirikiana na benchi lake la ufundi tunapata taarifa zote na hata wachezaji
wanaougua tunatoa matibabu kwao ili waweze kuendelea kujifua."
Aidha, Kilao amesisitiza kuwa malengo
ya timu yake ni kumaliza ligi ikiwa miongoni mwa timu 10 bora katika msimamo wa
Ligi Kuu Bara.
“Ukiangalia namna tulivyoanza ligi
tulianza kwa kusuasua lakini kwa sasa tumeshagundua wapi tulikosea tunajipanga
ili tuweze kufanya vizuri na kutimiza malengo," alisema katibu huyo.
Mwadui FC ipo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 28.
Ilikuwa timu ya kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara kuitungua Simba kwenye mchezo wao uliochezwa Shinyanga kupitia kwa Gerald Mdamu.








0 COMMENTS:
Post a Comment