June 27, 2020

KUMEKUWA na wimbo ambao unaimbwa na watu wengi hivi sasa wakati Ligi Kuu Bara na michuano mingine ikiendelea hapa nchini baada ya kusimama kwa muda mrefu.

Ligi Kuu Bara na michuano mingine hapa nchini ilisimama Machi 17, mwaka huu kutokana na uwepo wa janga la Corona ambalo limeitikisa dunia nzima.

Corona kuingia kwake imefanya mambo mengi kusimama ikiwemo michezo. Ligi mbalimbali duniani zilisimama na zingine kuahirishwa kabisa. Angalau hivi sasa mambo yamepoa na michezo imerejea kwa baadhi ya nchi.

Kurejea kwa michezo inamaanisha kwamba Corona kasi yake imepungua, lakini haijaisha kabisa, hivyo tahadhari bado zinatakiwa kuchukuliwa tena kwa kiwango cha juu sana.

Najua kwamba kila nchi inapambana kwa namna yake lakini kupungua kwa maambukizi ni ishara kwamba nchi yetu imechukua hatua stahiki zaidi katika kukabiliana na janga hili. Kuna nchi ambazo zilijifungia lakini maambukizi yamezidi kuongezeka kila kukicha.

Jumatano ya wiki hii baada ya mchezo kati ya Mbeya City dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe alisikika akitoa kauli za kulalamika juu ya ambacho kimetokea uwanjani hapo.

Mwakyembe alisifia uamuzi wa Mbeya City kuwa makini katika kufanya mchakato wa mashabiki kuingia uwanjani ambapo alisema utaratibu ulikuwa mzuri.

Anasema watu wengi walizingatia suala la kujikinga kwenye mageti, wakiwa wananawa mikono kwa maji tiririka na wengine wakiwa wana vitakasa mikono.

Lakini alieleza kuwa kilichotokea ndani ya uwanja ni wazi kilisikitisha kwa kuwa asilimia kubwa hakukuwa na tahadhari yoyote kwa wahusika.

Ameeleza kuwa hilo lilimsikitisha na kumfanya atafakari mara mbili juu ya uamuzi wa kuendelea kuwaruhusu mashabiki kuingia uwanjani kipindi hiki.

Katika hoja yangu ya msingi, ni kwamba michezo imerejea lakini haitoi tafsiri kwamba tunapaswa kujisahau na kuona kama Corona haipo.

Pamoja na kwamba Corona imepungua, lakini bado ipo, hivyo ni vizuri tusipoe katika kuchukua tahadhari zote zinazoelekezwa na Wizara ya Afya.

Mpaka sasa, maelekezo rasmi ni kwamba watu wanatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari. Ni hatari sana kujisahau katikati ya vita.

Na sasa mpira umerejea. Hapo napo, umakini unatakiwa kuzingatiwa na tahadhari iwe kubwa sana ili tuendelee kuona mpira, vinginevyo Serikali ikiamua kuweka ngumu ya kuzuia mashabiki basi mambo hayatanoga kama ambavyo wengi wetu tunataka iwe.

Mpira kurejea, haitoi tafsiri kwamba Corona haipo na kwamba watu wanaweza kwenda viwanjani bila kuchukua tahadhari.

Tunajua kwamba serikali imeruhusu mashabiki wachache kwenda uwanjani na wazingatie kujitenga, yaani kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.

Sasa kwa wale watakaokuwa wakipata nafasi ya kwenda viwanjani, hawatakiwi kujisahau na kuanza kukaribiana, badala yake wachukue tahadhari kubwa kwelikweli.

Wahusika wote, wanatakiwa wawe makini kuhakikisha soka linachezwa kwa usalama na kwa kuzingatia kanuni zote za kiafya katika kipindi hiki cha Corona.

Ile tabia ya mashabiki kukumbatiana baada ya bao kufungwa na kugongesheana mikono, hata kama tunajua kwamba ni ngumu kuzuia shangwe, basi kwa kuwa tupo katika kipindi cha Corona, tuhakikishe tunafanya shangwe zetu kwa tahadhari.

Tunajua mchezo wa soka unahusisha hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki, lakini isiwe kisingizo cha kutojali afya wakati huu mgumu tulionao.

Huu wimbo ambao unaimbwa kila siku, ifikie wakati muusikie vizuri na kuuelewa zaidi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic