DIRISHA la
usajili kwa timu za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili
na Ligi Kuu Wanawake Tanzania Bara, limefunguliwa tangu Agosti Mosi, mwaka huu.
Tangu
kufunguliwa kwa dirisha hilo, kumekuwa na fujo nyingi za usajili kwa kila timu
kuona inaimarisha kikosi chake kwa msimu ujao wa 2020/2021.
Timu za Ligi
Kuu Bara ndizo zimeanza fujo hizo kwa kasi, Simba, Yanga na Azam ndizo zimekuwa
zikitajwa sana katika usajili tangu kufunguliwa kwa dirisha hilo kubwa ambalo
linatarajiwa kufungwa Agosti 31, mwaka huu.
Katika
usajili huo, tumekuwa tukisikia mengi ikiwemo kuzidiana kete katika kuchukua
wachezaji.
Kipindi hiki
cha usajili ni muda ambao timu zinatakiwa kuwa makini sana kwani ukikosea tu,
basi utateseka kipindi kijacho wakati ligi imeanza.
Mara kadhaa
tumeona timu zikifanya usajili wa wachezaji wengi kipindi cha usajili, lakini
wachezaji wale wanashindwa kuendana na mfumo wa timu, mwisho wa siku wanaachwa.
Kusajili ni
jambo moja na kusajili kwa malengo ni jambo la pili. Hivyo nawaasa fanyeni
usajili kwa malengo, siyo mnasajili kwa kushindana tu mwisho wa siku mnafeli.
Kila timu
inafahamu mapungufu yao kutokana na kile ambacho walikifanya msimu uliopita.
Hivyo basi sajilini kulingana na mapendekezo ya mabenchi yenu ya ufundi.
Itapendeza
kuona usajili unaofanyika ni kwa mujibu wa mabenchi ya ufundi na si kwa mujibu
wa viongozi kwani tumeona mara kadhaa wachezaji wakisajiliwa kwa matakwa ya
viongozi.
Kocha anatoa
mapendekezo yake, lakini viongozi nao wanakuwa na mapendekezo yao, mwisho wa
siku wale wachezaji wa viongozi wanashindwa kwenda na mfumo wa kocha, timu
inafeli.
Tunataka
kuona msimu ujao kila timu ikiwa na wachezaji ambao wana matumizi nao, siyo
kujaza tu wachezaji halafu hawatumiki, hiyo si sawa kabisa.
Kuwa na
lundo la wachezaji halafu huwatumii, hiyo inakuja kuleta shida huko mbele kwa
kuhitajika kuwalipa halafu klabu inaona kama inatupa fedha bure. Sajilini kwa
malengo na siyo kwa kukomoana.
Kwa namna
ambavyo msimu wa 2019/20 ulivyokuwa, sidhani kama kutakuwa na timu itafanya
usajili ili tu kuwakomoa wapinzani, bali ni kwa malengo.
Azam FC
baada ya kufeli msimu uliopita, imeona ijiimarishe zaidi kwa kusajili majembe
mapya, Yanga nao hivyohivyo, bila ya kuwasahau mabingwa Simba.
Usajili wa
timu zote sina shaka nao, lakini wasiwasi wangu ni kwamba, mnasajili kulingana
na kile ambacho makocha wanahitaji au ni matakwa yenu viongozi?
Kumbukeni
msimu unakuwa na mechi nyingi, kucheza mechi 34 ukiwa na wachezaji wa viwango
vya chini mwisho wa siku mnaambulia maumivu makubwa.
Si mmeziona
timu ambazo zimeshuka daraja, nyingi zimeponzwa na udhaifu wa vikosi vyao na
hata Azam na Yanga zimeshindwa kushindana na Simba kutokana na kuwa wadhaifu
kiviwango.
Yanga
ilisajili wachezaji takribani 20 wapya kwa msimu uliomalizika, cha kushangaza
pia ikawaacha wengi ambao walicheza nusu msimu tu. Kuanzia dirisha kubwa,
ilipofika dirisha dogo wakawaacha. Huu ni upotevu wa fedha bure.
Binafsi
nahitaji kuona kila timu ikisajili wale wachezaji ambao itawatumia. Kama
mmeruhusiwa timu kuwa na wachezaji 30, si lazima mjaze nafasi zote ilimradi tu,
wekeni malengo.
Unaweza kuwa
na wachezaji wako 25, lakini wote wana uwezo wa kucheza kwa kiwango kikubwa,
hapo mtafanikiwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment