August 7, 2020

 

KAZI imeanza sasa kwenye upande wa usajili ndani ya ardhi ya Bongo ambayo huwa haishiwi matukio hasa kinapofika kipindi cha usajili.

Nakumbuka kuna wakati fulani mchezaji mmoja ambaye alikuwa gumzo zama hizo alikuwa anatoka Mbao FC, Pius Busitwa aliripotiwa kwamba alishawishiwa na shetani kukubali kusaini kwenye timu mbili.

Kuna mambo huyapati sehemu nyingine zaidi ya ardhi ya Bongo hapa ndipo kulipo na burudani na furaha unapata kwa wakati mmoja sio mchezo.

Imerudi tena sasa baadaa ya Ligi Kuu Bara kukamilika na bingwa kujulikana ambaye ni Simba.

 

Mchezo wa kufungia pazia la msimu wa 2019/20 ulikuwa ni wa Kombe la Shirikisho ambao ulipigwa pale kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.

 

Bingwa ni Simba ambaye alishinda kwa mabao 2-1 mbele ya Namungo FC kwenye mchezo huo ambao ulikuwa na hekaheka nyingi.

 

Mabingwa wanastahili pongezi hata washindi wa pili pia Namungo nao wanastahili pongezi kwa kupambania kombe mwanzo mwisho.

Hatua ambayo wamefika siyo ya kubeza kwa kuwa wanaonyesha kuwa walikuwa na jambo lao tangu awali mpaka wameweza kufikia malengo ambayo walikuwa wamejiwekea katika kusaka ushindi.

Ni furaha kwao kufika fainali pia wana furaha kwa kuwa wana nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa lakini hawakuwa wanyonge niliona walipambana.

Kuna zile gonganagongana zilikuwa zinafanyika na pia kulikuwa kuna muunganiko mzuri wa wachezaji kuwa ni timu moja kwenye kusaka matokeo licha ya kwamba hawakuwa na wachezaji wake wengi muhimu ambao ni tegemezi.

Hilo achana nalo maana halisi ya timu kila mmoja anastahili kucheza kwa kuwa alisajiliwa ndani ya kikosi na anatimiza majukumu yake ni kitu cha msingi kwa kila mchezaji kukitambua.

Tayari suala la usajili limeanza na sarakasi zake zimeanza kuonekana kwani zipo timu ambazo zimeingia kwa miguu miwili kufanya usajili huku nyingine zikivuta kasi taratibu.

Hakuna muda wa kusubiri kwa sasa kwa kuwa muda wenyewe unazidi kumeguka yale masuala ya kuanza kuongeza spidi dakika za mwisho ni mbaya.

Viongozi wa timu wasisahaua kwamba kuna ishu ya kusajili wachezaji kwa mtandao unaitwa TTF Conect, hili haina ile tunaongeza siku saba ama mbili kwa ajili ya usajili hapana ni mwendo wa mtandao tu.

Ingawa hilo linawezekana lakini muhimu kufuata utaratibu ambao umewekwa wazi kwa kusajili kwa umakini na kwa wakati.

Agosti Mosi, dirisha lilifunguliwa na linatarajiwa kufungwa Agosti 31,sio muda mwingi iwapo kila mmoja atakuwa makini katika kutimiza majukumu yake kwa wakati na utakuwa mrefu kwa yule ambaye atashindwa kutimiza majukumu yake kwa wakati.

Maana yangu ni kwamba yule ambaye atatulia na kusajili vizuri kwa muda uliopo kwa sasa wakati ujao atakua hana presha ya kupata matokeo uwanjani kwa kuwa anaamini ana kikosi imara huku yule ambaye atafanya makosa kwa sasa wakati ujao atakuwa na presha muda wote kwa kuwa hatakuwa na uhakika wa kupata matokeo.

 

Matatizo ambayo yalikuwa yanalalamikiwa na makocha zama zile za ligi kuanzia Ligi Daraja la Kwanza, Daraja la Pili, Ligi Kuu Bara na ile ya Wanawake wakati wao ndio sasa kufanyiwa kazi.

Kocha alikuwa akisema kwamba anashindwa kupata matokeo kwa kuwa hakuna mshambuliaji imara basi hapa tatizo ni ushambuliaji watafutwe washambuliaji wazuri na wenye viwango sio ilimradi.

 

Mwalimu alisema wanapoteza mechi nyingi kwa kuwa washambuliaji wanafunga ila mabeki wanashindwa kulinda matokeo hapo sasa ni kuangalia tunahitaji mabeki wangapi na makosa ya kipa yapoje. Huu ni muda wa kutibu tatizo palepale lilipo ili kuliondoa kabisa.

 

Lilipo tatizo la timu ndipo unapotakiwa kuboresha ili msimu wa 2020/21 utakapoanza kila timu iwe inapata matokeo kawa namna ilivyojipanga na hicho ndicho tunatarajia kukiona kwa kila timu.

Ni vyema kwa kila klabu ikasajili wachezaji kulingana na matakwa ya timu na si kufanya mashindano yasiyo na misingi alafu mwisho wa siku wachezaji ambao walisajiliwa bila ya uhitaji wanakuja kuzigharimu timu kwenye ligi.

 

Wasajiliwe wachezaji watakaotoa ushindani na ni vyema wachezaji wote watakaosajiliwa katika timu husika haswa wale wa nje wawe wamefuatiliwa kwa kina mienendo yao na ubora wao ili mwisho wa siku wasisajiliwe wachezaji mizigo ambao watakuja kuleta changamoto katika timu jambo ambalo si sahihi.

 

Kuna baadhi ya timu katika msimu uliomalizika zimejikuta zikishuka daraja kutokana na kushindwa kuonyesha makali kutokana na kutokuwa na wachezaji wenye viwango.

 

Muda ni mfupi katika kipindi hiki hivyo ni vyema kila timu ikasajili kwa umakini na kuzingatia wakati kwa kupata wachezaji sahihi na si bora wachezaji kwani ligi bora ni ile yenye wachezaji wenye ushindani.

 

Kitu cha msingi kabla ya usajili ni muhimu kuwa na maskauti ambao watawafuatilia kwa umakini wachezaji ambao watajiunga na timu kwenye msimu wa usajili.

Hii itasaidia kupunguza sarakasi hizi ambazo huwa zinaibuka kwani kila mmoja kwa sasa na matamanio ya kuona anakuwa na mchezaji mzuri ila hajui atampata wapi.

Kuna umuhimu wa kuwachunguza wachezaji tabia zao za ndani na nje ya uwanja zitasaidia kila mchezaji ambaye atasajiliwa ndani ya timu kupambana kutimiza majukumu yake na kuachana na vitendo ambavyo sio vya kiungwana.

Mpira una kanuni zake ambazo zinapaswa zifuatwe na kila mmoja ambaye anaishi maisha ya mpira ikiwa ni pamoja na wachezaji na viongozi.

Hakuna mchezaji ambaye anaweza kupata jina bila kupita kwenye timu ambayo inamfungulia maisha yake ya kujulikana kwa mashabiki pamoja na timu nyingine ambazo zinahitaji saini yake.

Ili timu ipate mafanikio inahitaji kuwa na mchezaji makini na mwenye nidhamu nje na ndani ya uwanja jambo ambalo linahitaji umakini mkubwa na sio kukurupuka.

Uwezo wa kusajili hata kama unao wewe sajili lakini inabidi itazamwe unasajili mchezaji ili akafanye nini ndani ya timu ama ndo anakwenda kukaa benchi na kuchuja kiwango chake jumla.

Ikiwa hakuna tatizo ndani ya timu yako presha ya nini kuanza kufanya usajili mwisho wa siku utawaacha wachezaji wazuri unawachukua wachezaji ambao hata hawakupi matokeo wa kazi gani sasa hao?

Ligi imeisha na makosa ya kila timu yameonekana basi ni muda wa kujibu sasa makosa kwa kuziba mapengo  ambayo yamekuwa yakionekana.

Kila mchezaji anahitaji nafasi ya kucheza kwenye timu ambayo atasajiliwa jambo la msingi ni kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kuwavutia waya na kuwapa madili wasaini.

Zipo ambazo zimemaliza ligi na kushuka jumlajumla na nyingine zimepanda basi wakati wa maandalizi ni sasa bila kujali upo eneo gani.

Kwa kila timu ambayo imepata bahati ya kupanda inastahili pongezi na kuanza kujipanga upya kwa ajili ya msimu mpya na maisha yao yatakuwa ndani ya Ligi Kuu Bara na sio Ligi Daraja la Kwanza.

Mbao FC wabishi mpira umewafanya mmekuwa kweli wabishi lakini hakuna namna tunaamini kwamba mtapambana na mna nafasi ya kurejea ndani ya ligi kwa msimu mwingine tena.

Ihefu wana kutoka Mbeya karibuni ndani ya ligi mje kuonyesha kwamba hamkubahatisha kumaliza mkiwa nafasi ya pili na hamkubahatisha kupindua meza kwenye playoffs yenu mbele ya Trans Camp.

Ishu ya usajili inawahusu nanyi pia mnatakiwa kuwa makini na kufanya uchaguzi sahihi kwa kuwa mambo huku sio kama mlikotoka kuna mambo kidogo yapo tofauti huku ni mwendo wa jeshi tu.

Mmepishana na Mbao FC mkizubaa wakati ujao mtashangaa mnakutana nao mnawapisha tena ndiyo maisha ya mpira hayana mshindi wa jumla ni dakika 90 tu unashinda na maisha yanaendelea.

Kila la kheri na mnastahili pongezi kwani haikuwa kazi rahisi ndugu zangu kushinda mbele ya wabishi. Felix Miziro unastahili heshima na pongezi kwa jitihada ambazo umeonyesha.

 Wakati mwingine wengi wanapuuzia uwezo wako ila wewe ni bonge moja ya kocha licha ya ndoto yako na malengo makubwa ya timu kubaki ndani ya ligi kushindikana hukuwa na chaguo kila la kheri.

 


1 COMMENTS:

  1. Amina ila tumashangaa timu yenye CEO ndiyo inapeta vurugu na inaendeshwa kisasa tena ina Uwanja wa Mazoezi Whyyy??

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic