SHAMRASHAMRA za tuzo za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2019/20 zilifanyika usiku wa Ijumaa Agosti 7 ambapo wachezaji, timu, makocha na viongozi mbalimbali waliibuka kidedea na kutwaa tuzo hizo kutokana na mchango mkubwa ambao waliutoa kwa kipindi chote cha msimu huu.
Tuzo hizo ambazo hazikuweza kufanyika mwaka jana kutokana na kutokuwepo kwa mdhamini wa ligi, zilirejea kwa kishindo ambapo kulikuwa na vipengele mbalimbali na zawadi kwa kila kipengele ikiwemo; tuzo na zawadi za fedha.
Miongoni mwa tuzo ambazo zilikuwa zikisubiriwa kwa hamu ni ile ya Kikosi Bora cha Msimu wa Ligi Kuu Bara ambacho huonyesha wanaume 11 waliofanya vizuri zaidi msimu huu.
Hivi ndivyo walivyofanya ndani ya msimu wa 2019/20 wachezaji walio kikosi cha kwanza:-
AISHI MANULA
Ametwaa tuzo ya Golikipa Bora wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tano mfululizo, ndiye chaguo la kwanza la kocha Sven Vandenbroeck ndani ya kikosi cha Simba, naye hajamwangusha kocha wake kwani kwa msimu huu pekee ameweza kusimama langoni kwenye michezo 17 bila kuruhusu nyavu zake kuguswa yaani ‘Clean sheets’.
NICHOLAS WADADA
Raia huyu wa Uganda alitwaa tuzo hiyo ya beki bora akiwashinda mabeki Bakari Mwamnyeto (Coastal Union) na David Luhende wa Kagera Sugar.
Wadada amehusika kwenye mabao tisa kati ya 52 yaliyofungwa na Azam msimu huu, amefunga bao moja na kuasisti nane.
DAVID LUHENDE
Huwezi kutaja mafanikio ya Kagera Sugar msimu huu na kuacha kuutaja mchango wa beki huyu wa kushoto, Luhende ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wametumika kwenye michezo yote 38 ya Ligi Kuu Bara msimu huu ambapo amefanikiwa kutoa asisti nne za mabao.
SERGIE WAWA
Raia wa Ivory Coast ambaye ameendelea kuthibitisha ule usemi wa Kiswahili usemao ‘Ukubwa Dawa’ mara kadhaa amekuwa kiongozi wa safu ya Ulinzi ya Simba huku pia msimu huu akifanikiwa kuasisti mara moja.
BAKARI MWAMNYETO
Nahodha wa zamani wa Coastal Union ambaye tayari amekamilisha usajili wake wa kujiunga na kikosi cha Wanajangwani, alikuwa na msimu bora sana ambapo ameiongoza safu ya ulinzi ya Coastal.
Ukiacha suala la kutimiza majukumu yake ya kuifanya safu ya ulinzi ya Coastal kuwa bora, Mwamnyeto pia ameisaidia safu ya ushambuliaji ya timu hiyo baada ya kuweka kambani bao moja.
ZAWADI MAUYA
Mkata umeme wa zamani wa klabu ya soka ya Kagera Sugar ambaye pia amekamilisha usajili wake wa miaka miwili kuitumikia Yanga msimu ujao, Mauya amepata nafasi ya kuingia kwenye kikosi bora cha msimu kwa kumshinda kiungo wa Simba, Jonas Mkude ambaye pia alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuingia kwenye kikosi hicho.
LUIS MIQUISSONE
Anatajwa kuwa ndiye mchezaji ghali zaidi kwenye Ligi Kuu Bara katika usajili ambao Simba iliufanya kipindi cha dirisha dogo la mwezi Januari ambapo Simba ilimsajili nyota huyu kutoka Klabu ya Mamelodi Sundowns inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.
Miquissone kwenye ligi kuu msimu huu ameifungia Simba mabao manne na kuasisti mara moja huku bao alilofunga dhidi ya klabu ya Alliance likiwa miongoni mwa mabao matatu bora msimu huu.
LUKAS KIKOTI
Ubora wa kikosi cha Namungo msimu huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na ubora aliokuwa nao Kikoti katika eneo la katikati ya uwanja, uwezo wake wa kuituliza timu na kupiga pasi zenye macho, unajidhihirisha kwenye furushi la takwimu bora alizozikusanya na hii ni baada ya kuhusika kwenye mabao 11 ya Namungo, amefunga mabao manne na kuasisti mengine saba.
MEDDIE KAGERE
Ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili mfululizo, tangu ajiunge na Simba msimu wa 2018/19 Kagere ameifungia Simba mabao 45 kwenye Ligi Kuu Bara pekee huku msimu huu pekee akihusika kwenye mabao 28, akiweka kambani mabao 22 na kuasisti mara sita.
CLATOUS CHAMA
Kwa maneno machache unaweza kusema huu ulikuwa mwaka wake kwani ukiacha suala la kutajwa kuwa kwenye kikosi cha timu bora ya msimu huu, Chama mpaka sasa amefanikiwa kukusanya tuzo nne kubwa, tuzo hizo ni; Mchezaji Bora wa Michuano ya FA, Mchezaji Bora wa SportPesa, Kiungo Bora wa Msimu na Mchezaji Bora wa Msimu.
Amefunga mabao mawili na kutoa pasi 10 za mabao.
JOHN BOCCO
Nahodha wa Simba anayeshikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kwa miaka zaidi ya kumi aliyocheza ligi kuu amefunga zaidi ya mabao 100, msimu huu kwa mara nyingine tena ameiongoza Simba kutwaa kombe la tatu mfululizo ambapo yeye pekee amechangia mabao 12 ya Simba akifunga mabao tisa na kuasisti mengine matatu.
duh hawakutoa hata mmoja hao mbumbumbu fc! pole sana hadi mwakani
ReplyDeletePana kosa hapo kidogo kwa kutomtaja Kapombe kwa kuwa Kati ya mabeki bora wa msimu na tumemuona jinsi anavolinda, kuupanda na pasi zake nyingi za assist
ReplyDeletePia ilibidi Katika tuzo, ingelikuwepo tunzo ya msemaji bora wa timu ambapo Manara alistahili
ReplyDeleteKwahiyo Morison si chochote au mpaka aichezee simba ndio watamuona? Ama kweli hii ndio Tqnzania yetu!!
ReplyDeleteWe kweli ni pumbu
ReplyDeleteHongera zao waliopata matunzoooooooo wasichoke waendelee kupambana
ReplyDelete