DAVID Molinga, mshambuliaji namba moja ndani ya Yanga amesema kuwa alipata taarifa za kuachwa na timu yake ya Yanga kupitia mitandao kwa kuwa alizungumza na viongozi wake wakamwambia kuwa watamuongezea mkataba.
Yanga imeachana jumla na wachezaji wake 16 ambapo kwa sasa imeanza kusajili majembe mapya kwa ajili ya msimu wa 2020/21 unaoatarajiwa kuanza Septemba 6 na tayari wameshaanza mazoezi.
Akizungumza na Saleh Jembe, Molinga amesema kuwa baada ya Ligi Kuu Bara kuisha alikaa mezani na viongozi wa Yanga ambao walimuahidi kuwa watamuongezea mkataba kutokana na utendaji wake wa kazi jambo ambalo limekuwa tofauti.
"Ujue nilizungumza na Yanga, waliniambia kwamba wataniita ili tuongeze mkataba lakini ghafla nikiwa nyumbani nikaona jina langu lipo kwenye orodha ya wachezaji ambao wameachwa.
"Kiukweli nilishtuka lakini ndio maisha yetu ya mpira huwezi kuwa na chaguo, inatokea sio Bongo tu hata Ulaya kwenye timu kubwa wachezaji wanaachwa ila utofauti kwa hapa umekuja kwa namna ambavyo nimeachwa.
"Kikubwa kwa sasa maisha yanaendelea nitaangalia namna nitakavyofanya kwani mimi ni mchezaji na uwezo wangu unajulikana na upo wazi," amesema.
Ndani ya ligi, Yanga ikiwa imefunga mabao 45 amehusika kwenye mabao 12, akifunga mabao 11 na kutoa pasi ya bao moja mbele ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba wakati Yanga ikishinda bao 1-0.
0 COMMENTS:
Post a Comment