September 26, 2020



MAPEMA jana Ijumaa, taarifa za mshambuliaji, na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta kujiunga na Fenerbahçe ya Uturuki, zilithibitishwa rasmi na klabu hiyo.

 

Samatta amejiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miaka minne akitokea Aston Villa ya England aliyoitumikia kwa takribani miezi nane tu baada ya kujiunga nayo Januari, mwaka huu akitokea KRC Genk ya Ubelgiji.

 

Kwenda kwake nchini Uturuki kucheza soka, inakuwa ni ukurasa mpya ameufungua, lakini ni katika mwendelezo wa mapambano yake kisoka.

 

Kama tunavyofahamu, safari ya Samatta kisoka haikuwa ya mkato, kuanzia Mbagala Market ambayo kwa sasa ni African Lyon, Simba, TP Mazembe, KRC Genk na Aston Villa, huko kote alionesha uwezo ingawa kuna changamoto alikumbana nazo.

 

Nikurudishe nyuma kidogo, kitendo cha Samatta kucheza Simba nusu msimu kisha kuchukuliwa na TP Mazembe ya DR Congo, ni wazi alionesha uwezo mkubwa kiasi cha matajiri hao kutoka DR Congo kumchukua.

 

Akiwa TP Mazembe, aliweka nembo yake pale, hata alipokuwa akiondoka mwaka 2016 kwenda KRC Genk, mashabiki hadi viongozi wa klabu hiyo hawakuwa tayari kuona akiondoka kirahisi kwani mara kadhaa alizuiwa na uongozi chini ya Moise Katumbi.

 

Samatta alifanya makubwa ndani ya TP Mazembe kiasi cha mwaka 2015 kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa Wanaocheza Ligi za Ndani. Pia aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mwaka huo.

 

Kuondoka kwake pale TP Mazembe, hakuacha deni, aliifanya kazi yake ipasavyo, ndiyo maana Wabelgiji waliona huyu mwamba anawafaa.

 

Alipoenda KRC Genk, huko nako aliuwasha moto. Wakati anaondoka Januari, mwaka huu na kutua Aston Villa, Wabelgiji walihuzunika sana kuona staa wao anaondoka.

 

Haikuwa rahisi kwake kuiweka alama huko kote anakopita, bali ni kwa juhudi na kutokata tamaa ndiyo kulikombeba zaidi nahodha huyo wa Taifa Stars.

 

Genk na Watanzania wana kumbukumbu nzuri sana ya Samatta kutokana na bao lake la kichwa pale Anfield dhidi ya Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2018.

 

Samatta ndani ya Aston Villa, alianza taratibu, bao lake moja ndani ya Premier na lingine katika Carabao Cup mbele ya Manchester City, lilionesha kweli ni mpambanaji. Kukosa nafasi kubwa ya kucheza, kukamfanya ashindwe kuonesha cheche zake.

 

Aston Villa ilipoponea chupuchupu kushuka daraja, imeona msimu huu ijiimarishe zaidi hasa kwenye nafasi ya ushambuliaji kwa kushusha vifaa viwili. Ollie Watkins na Bertrand Traore, hapo nafasi ya Samatta ikawa finyu, akachukua uamuzi wa kuondoka.

 

Kuondoka kwake England si kwamba ndiyo mwisho wa safari. Kama asemavyo mwenyewe kwamba HAINA KUFELI, basi naamini huko anapokwenda kwenye maisha mapya, hawezi kukubali kufeli.

 

Watanzania tuendelee kumuombea kijana wetu kwani kwa sasa ndiye anaipeperusha vema bendera ya Tanzania katika soka la kimataifa.

 

Wapo wengi ambao wanakwenda kucheza soka nje na kurudi Tanzania, lakini kwa Samatta, imekuwa tofauti.

 

Tangu mwaka 2011 alipoondoka Tanzania na kwenda DR Congo kucheza soka pale TP Mazembe, basi kurudi kwake ni kuja kuitumikia Taifa Stars au kipindi cha mapumziko tu.

 

Kila la heri Samatta katika maisha yako mapya, mapambano lazima yaendelee.

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic