October 9, 2020







Na Saleh Ally

UMEWAHI kusikia mashabiki wa Manchester United, Manchester City, Real Madrid, Barcelona, Juventus wamepigana kwa ajili ya rangi? Najua utanijibu hapana.


Hapa nazungumzia mashabiki wa timu kama hizo, za kariba ya aina hiyo na mashabiki hasa ambao ni asilia ya timu hizo kwa maana ya wale wanaotokea barani Ulaya.


Mashabiki hawa wanakuwa wanajua timu zao zinahitaji nini, wanaelewa maana ya wao kuwa mashabiki na wanajua kuwa furaha na faraja ndio jambo namba moja kwao.


Utambulisho wa timu, unajulikana na lazima shabiki aelewe kuwa rangi na nembo ni jambo ambalo linahusika katika utambulisho lakini bado hakuna klabu hata moja duniani ina uwezo wa kumiliki rangi zake peke yake.


Kwa rangi haiwezekani, hakuna mmiliki wa rangi lakini zinaweza kutumika katika mambo mengi sana, katika soka moja ni utambulisho.


Nembo inawezekana kila klabu kuwa na nembo yake ambayo inatambulika ikiwa na ujumbe ambao inafikisha kulingana na hali fulani.


Kama nembo kila klabu inaweza kumiliki yake, basi huu ndio utambulisho namba moja wa klabu ambao unapewa nafasi ya kwanza na unapaswa kuheshimiwa.


Msisitizo wangu hapa ni hivi, rangi za njano na kijani zinaitambulisha Yanga, nyekundu na nyeupe zinaitambulisha Simba na unaona, wakati Simba wanatengana na Yanga walichagua rangi tofauti ili watofautiane nao. Lakini tukubali rangi haziwezi kugeuka na kuwa kitu kinachotumika kujenga kutoelewana, kuchukiana hadi wakati mwingine kufikia kuwa uadui.


Tumeona mara nyingi mashabiki wa Yanga na Simba wakifikia hadi kupigana, kuchaniana nguo na jezi, kudhalilishana eti kisa rangi. Swali linakuja, nani hasa mmiliki wa hizo rangi?


Mfano tunaona mtu katika soka ni Simba (rangi nyeupe na nyekundu), katika siasa ni CCM (rangi njano na kijani). Sasa huyu anapaswa kuzichukia rangi hizi kwa sababu ipi?


Wakati mwingine katika soka, mtu anaishangilia Yanga (njano na kijani) lakini anaipenda Arsenal (nyekundu na nyeupe). Na utaona baadhi hadi wanayafinya mapenzi yao kwa madai hawawezi kuvaa jezi nyekundu ya Arsenal wakati Arsenal inaanza kuonekana kwa jezi hiyo nyekundu na nyeupe.


Kuna vitu vya kujifunza na tukaamua kuachana na ushamba wa rangi. Ushambu huu umewafanya mashabiki wengi kuumizana au kujengeana uadi. Pia tunaweza kupunguza heshima ya kupindukia katika rangi mbalimbali za klabu mnazozipenda na kufanya ni kitu cha kawaida kwa kuwa rangi inayotumika Yanga au Simba leo, kesho utaikuta inatumika katika kitu kingine kabisa ambacho huenda hakikuvutii hata kidogo.


Klabu zenu hazimiliki rangi hata moja, ila zinatumia rangi ambazo pia zinaweza kutumiwa na klabu nyingine au jambo jingine kwa kuwa ndio dunia ilivyo na hili haliwezi kubadilika.


Kuendelea kuumizana na kudhalilishana kisa eti huyu kavaa rangi fulani ni kuonyesha kutojitambua katika kiwango kilichopitiliza.


Watu wanaumizwa na ajabu watu wanafurahia, jambo hili si sahihi kwa maana ya uvunjifu wa kisheria na ukiukwaji wa haki za binadamu. Mambo haya yote mawili hayakubaliki katika mchezo wa soka kwa kuwa ni mchezo wa kistaarabu.


Anayekwenda mpirani na kutaka kuumiza wenzake, maana yake si mpenda soka wala mwanamichezo. Hawezi akawa na nia nzuri au njema na mchezo huo badala yake ni yale matakwa ya kupenda sifa zisizo na msingi lakini akiwa anavunja sheria za nchi na kukiuka haki za kibinadamu.

Nakukumbusha, usidhani unaweza kuwaonea watu kila siku. Kuendelea kufanya uovu ni kutengeneza chuki ambayo ni mbaya sana kwa kuwa ina katika mioyo ya unaowaonea, kuna siku wakisimama na kuamua kulipiza itakuwa shida. Hivyo, si sahihi kupiga au kuwadhalilisha watu kwa kisingizio cha rangi. Soka bado inabaki kuwa sehemu ya upendo na umoja.


Mpira una faida nyingi, moja kubwa ni kuwaunganisha watu hata waliokuwa wametengana hivyo, si sahihi hata kidogo suala la vurugu kupitia jazba za kutunga kwa visingizio vya rangi. Tubadilike.




6 COMMENTS:

  1. We mbona hujabadilika kuandika habari za kujitungia? Acha ujinga

    ReplyDelete
  2. Salehe shida siyo rangi ya jezi, Mimi mtoto wangu wa kwanza wa kiume akiwa mdogo Kakangu alimnunulia jezi ya Simba tangu hapo mtoto anapenda Simba na Nina mpenda japo Mimi napenda Yanga Sana.Hapa issue ni maadili hasa kwa Mashabiki,eg Yanga Inacheza na Mtibwa we mpenzi wa Simba ukivaa jezi ya Simba ukaenda Uwanjani ukakaa kimya Nani atakubughudhi.Lkn ukodi Costa utoke Dar uende Morogoro na jezi zako za Simba uanze kushangilia mwanzo mwisho na matusi juu wAtu wakuache?

    ReplyDelete
  3. Mimi rangi ya njano na kijani ccm na boleka,lkn the same rangi Yanga nafurahi na vilevile Red colour Simba kwangu kichefuchefu by Liverpool nyekundu na furahi sana Unasemaje hapo

    ReplyDelete
  4. Hawa mazazwa wanaotafuta kuleta fujo na kuwapiga wenzao kwa kisingizio cha kutotaka washangilie.Kila mtu ana haki ya kushangilia timu anayotaka.Hakuna mwenye haki ya kuchagulia watu timu za kushangilia.
    Wanaoleta fujo wanajulikana.Washamba tu.

    ReplyDelete
  5. Salehe acha kiwaogopa waambie tu Ukweli walichokifanya morogoro tungelipa dodoma je ingekuaje........

    ReplyDelete
  6. Kama Ni kushangilia si mkashangilie Mtibwa na Ruvu shooting

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic