October 9, 2020

 



NA SALEH ALLY

ILIKUWA faraja kubwa kwa mara nyingine kuona kuna kampuni inasimama na kuamua kuwashika mkono wapenda mpira wa kikapu nchini.


Benki ya CRDB imeamua kumwaga kitita cha Sh milioni 200 kwa ajili ya kudhamini Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Taifa yatakayofanyika mjini Dodoma.


Mashindano hayo yamepangwa kuanza Novemba 12 hadi 21 na kushirikisha mikoa yote zikiwemo Wilaya tano za Mkoa wa Dar es Salaam.


Nilimuona Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akiongoza shughuli hiyo ya uzinduzi na kimyakimya nikasema “CRDB wamefanaya jambo la msingi hasa.”


Hakika hili ni jambo la msingi hasa kwa kuwa CRDB wamedhamini michuano ambayo bila ya ubishi ilikuwa imepoteza kabisa mwelekeo.


Ilipoteza mwelekeo si kwamba hakuna wachezaji au makocha au waamuzi wa mchezo huo lakini hali imekuwa ngumu na hakuna wadhamini wanayoupa nguvu mchezo wa kikapu.

Mchezo wa kikapu kama ni takwimu, unaonyesha ni wa tatu kwa kuwa na mashabiki wengi hapa Tanzania, baada ya soka na ngumi. Maana yake ni mchezo wenye watu wengi sana wenye mapenzi nao. Lakini umekuwa ukishindwa kabisa kusimama kutokana na kukosa nguvu ya udhamini.


Wako watu wamekuwa wakipambana nao kuhakikisha unaendelea kuchechemea. Mmoja wao ni Michael Mwita ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF).


Bahati nzuri kwangu nafahamiana na Mwita tokea tukiwa tunasoma, wakati nikipambana katika timu ya shule ya mpira wa miguu, yeye na akina Deo Kwiyukwa walikuwa nyota wa mpira wa kikapu kuanzia shule wakati wa Umiseta lakini hata katika timu za mtaani.


Mwita amewika hata katika ngazi kubwa za Dar es Salaam na amekuwa akiendelea kuupigania mchezo huo, hii inaonyesha licha ya kuwa kiongozi tu lakini ana mapenzi nao ya dhati.


Kwangu bado naona mchezo huo ni sehemu ya afya na furaha lakini ni biashara inayoweza kutengeneza ajira na hasa kama itapata watu ambao wanaweza kuendelea kuusimamia vizuri zaidi katika ngazi za klabu.


Watu wanaupenda mchezo huo lakini hawapati nafasi ya kuuona ukichezwa kiushindani au katika ule mwonekano unaokuwa na mvuto na sasa CRDB wanaweza kuwa chanzo cha kuchagiza hili kurudi kwenye zile enzi za mchezo huo.


Muonekano unaochagiza, pia ni kuonekana kukiwa na ushindani, jezi nzuri, mipira bora, waamuzi wakichezesha kwa kiwango bora na wamependeza. Hali kama hizi huchangia kupatikana kwa hamasa ya kimichezo.


Lazima michuano hii ya taifa huko Dodoma itakuwa na mwonekano tofauti kwa ajili ya udhamini huu wa CRDB na lazima itaongeza mvuto na ikiwezekana deni linabaki kwa wadau wenyewe kwa maana ya wachezaji, waamuzi na makocha.


Kwamba lazima michezo hiyo iwe na kiwango kinachovutia, hali itakayowafanya wadhamini hao kuona walikuwa sahihi ili waone wanaweza kuendelea au hata kurudi hadi katika ngazi za klabu na kudhamini tena.


Lazima mjifunze kitu, kwamba wadhamini hawapatikani kwa ulaini, lazima mjue kuwa wadhamini wanahitaji jambo nao, hivyo ni lazima kuhakikisha mnawabakiza na hili linawahusu hata wachezaji pia.


Watakapoonyesha kiwango bora, watazidi kuongeza ushawishi wao kubaki lakini ikiwezekana kuwashawishi wengine kuingia na kudhamini mchezo huo.


Kuingia kwa CRDB kuwe chachu ya kuimarisha au kuboresha kila sehemu wadau wa mpira wa kikapu walikuwa wanaona ilikuwa inapwaya.


Kwa CRDB, bila ya kupindisha, wanapaswa kupewa shukurani kwa uamuzi wao huo katika kipindi hiki kwamba kweli wameijali michezo na hasa mpira wa kikapu, jambo ambalo wengi wameshindwa kulifanya ndio maana nikasema, kama walikuwa wamechelewa hivi maana tuliwasubiri sana.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic