October 6, 2020


MZUNGUKO  wa tano kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Bara ambao umeanza Oktoba 2 umekamilika Oktoba tano na timu zote zimecheza jumla ya mechi tano.

Kwa mwezi Septemba, wachezaji walionyesha ushindani mkubwa ndani ya uwanja na kushudia kila timu ikivuna kile ambacho wamekipanda.

Kwa mizunguko yote minne iliyochezwa ilikusanya jumla ya mabao 53 ambapo katika mabao hayo ni moja tu lilikuwa la kujifunga ambalo lilifungwa na Edson Katanga wa JKT wakati timu yake ikipoteza kwa kufungwa bao 1-0 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Spoti Xtra inakuletea kikosi bora ndani ya ligi kwa mwezi Septemba namna hii:-

 David Kissu wa Azam FC

Jukumu lake ameweza kulitimiza ndani ya Azam FC ambayo imecheza jumla ya mechi nne ambazo ni dakika 360.

Lango lake halijaruhusu kuokota bao ndani ya dakika 360. Hivyo amekuwa bora muda wote wa mwezi Septemba akiwapoteza makipa wengine ikiwa ni pamoja na Aishi Manula wa Simba mwenye ‘cleansheet’ 2 na Metacha Mnata wa Yanga mwenye ‘cleansheet’ 3. Alipoteza clean sheet yake raundi ya tano kwa kufungwa mabao mawili na timu ya Kagera Sugar.     


                   

Abdallah Kheri wa Azam FC

Nyuma ya ‘cleansheet’ 4 za David Kissu amesimama mwamba huyu Kheri ambaye ameaminika na Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba.

Alianza kikosi cha kwanza kwenye mechi zote nne ambazo Azam imecheza na haijaruhusu bao ndani ya dakika 90.

Matokeo yake yalikuwa ni:- Azam 1-0 Polisi Tanzania, Azam 2-0 Coastal Union, Mbeya City 0-1 Azam na Tanzania Prisons 0-1 Azam.

 

David Luhende wa Kagera Sugar

Nyota huyu wa Kagera Sugar anashikilia rekodi ya kucheza muda mrefu kuliko wote ndani ya Kagera Sugar msimu wa 2019/2020. Kwenye mechi 38 za Ligi Kuu Bara alitumia dakika 3,420 kwa kuwa alicheza mechi zote bila kuwa na ushkaji na benchi.

Ameanza tena makeke yake msimu wa 2020/2021 akiwa ametumia dakika 360 kwenye mechi nne za ligi. Ametoa pasi moja ya bao kwa Yusuph Mhilu wakati timu yake ikishinda mbele ya KMC Uwanja wa Kaitaba.


Pia kwenye mchezo dhidi ya Azam FC alifunga bao lake la pili mzunguko wa tano wakati timu yake ikipoteza kwa kufungwa mabao 4-2.


Dickson Job wa Mtibwa Sugar

Beki chipukizi ndani ya Mtibwa Sugar anaeaminika na Kocha Mkuu Zuberi Katwila. Balaa la washambuliaji wasumbufu Bongo kama John Bocco wa Simba na Michael Sarpong wa Yanga analitambua kwa kuwa alipambana nao.

Licha ya timu yake kufungwa jumla ya mabao mawili katika mechi nne bado kijana ni mpambanaji na anaonyesha kipaji alichopewa akiwa ndani ya uwanja.

 Kwa mwezi Oktoba tayari timu yake imefungwa bao moja.
Lamine Moro wa Yanga

Beki kisiki ndani ya Yanga atakupa mambo mawili kwa wakati mmoja. Jambo la kwanza atalinda lango lako na la pili, atafunga kuipa ushindi timu.

Ndani ya mwezi Septemba akiwa amecheza mechi tatu zenye dakika 270, timu yake haijafungwa na ameipachikia timu yake mabao mawili.


Clatous Chama  wa Simba

Akishindwa kufunga, atatengeneza pasi ya bao. Ikishindikana, atatibua mipango ya wapinzani wake.

Akiwa amecheza mechi nne na kutumia dakika 358, amefunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao kati ya kumi yaliyofungwa na timu yake ya Simba.

 
Luis Miqussone wa Simba

Kinara wa pasi ndani ya Ligi Kuu Bara akiwa mecheza mechi tatu na kuyeyusha dakika 270, ametoa jumla ya pasi nne zilizoleta mabao.

Uwezo mkubwa wakupiga mipira iliyokufa imejificha kwenye miguu yake, anafanya watu waamini kuwa mpira ni kazi nyepesi kila wanapomtazama nyota huyu.


Bigirimama Blaise wa Namungo FC

Mfungaji wa kwanza kufunga bao ndani ya Ligi Kuu msimu wa 2020/2021, aliwatungua Coastal Union Uwanja wa Majaliwa Septemba 6.

Kibindoni ana mabao mawili. Akiwa ametumia dakika 360, anauwezo mkubwa wa kucheka na nyavu akiwa uwanjani.Bao lake la pili aliwafunga Mbeya City na mechi zote timu yake ilishinda bao 1-0.

Mzamiru Yassin wa Simba

Wanamuita ‘Mapafu ya Mbwa’ akiwa ndani ya uwanja kutokana na uwezo wake wa kukaba na kuanzisha mashambulizi. Ni mzawa ambaye amekuwa bora kwenye vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora.

Amehusika kwenye mabao matatu ya Simba kati ya 10, akiwa amefunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao. Ni chaguo namba moja kwa kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck.


Meddie Kagere wa Simba

Mabao yake 47 aliyoyapata ndani ya Ligi Kuu Bara, yanamaanisha kuwa si mchezaji wa kubeza. Ana tuzo mbili kabatini za mfungaji bora, moja aliitwaa msimu wa 2018/2019 alivyotupia mabao 23 na ya pili, aliitwaa msimu wa 2019/2020 aivyotupia mabao 22.

Msimu huu akiwa amecheza mechi nne, amefunga mabao mawili yanayokamilisha jumla ya mabao 47 ndani ya ligi.


Prince Dube wa Azam FC

Mtambo wa mabao ndani ya Azam, akiwa amehusika kwenye mabao manne kati ya matano yaliyofungwa na timu yake. Amefunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao.

Ametumia jumla ya dakika 360. Ni chaguo la kwanza kwa Mromania, Aristica Cioaba ndani ya Azam FC. 


Tayari ameyeyusha dakika nyingine 90 kwenye mchezo wa raundi ya tano dhidi ya Kagera Sugar na alifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao. 

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic