WAKIWA kwenye mchakato wa kumsaka Kocha Mkuu atakayerithi mikoba ya Zlatko Krmpotic ambaye amefungashiwa virago vyake Oktoba 3 akiwa amebakiza siku 14 kabla ya dabi dhidi ya Simba Uwanja wa Mkapa, uongozi wa Yanga umetaja sababu kubwa zinazompa nafasi Cedric Kaze kukinoa kikosi hicho.
Mkurugenzi wa Uwekezaji ndani ya Kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said amesema kuwa mchakato unaendelea kwa umakini kumsaka kocha mpya huku akiweka wazi sababu zitakazompa nafasi Kaze.
"Faida ya kuwa na Kaze ndani ya timu ni uwezo wake wa kujua lugha zaidi ya moja ambapo anajua lugha nne ikiwa ni Kiswahili, Kiingereza,Kifarana na Kihispania.
"Kwa kujua lugha nyingi ni mwanzo mzuri wa kuweza kurahisisha mawasiliano hivyo itakuwa rahisi kwa wachezaji wetu ambao wanajua lugha hizo kuweza kuongea naye na kufanya mazungumzo.
"Hatumleti Kaze kwa ajili ya mechi moja ambayo ni dhidi ya Simba pekee hapana kuna mechi nyingi za kucheza ambazo ni 33 ukiachana na dabi," amesema.
Kwa sasa Yanga ipo chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Juma Mwabusi ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ukaribu na Krmpotic raia wa Serbia.
Kaze alikuwa kwenye mpago wa kutua Yanga kubeba mikoba ya Luc Eymael ambaye alifutwa kazi kutokana na ishu ya ubaguzi wa rangi ila alishindwa kuibuka Bongo kwa kile alichoeleza ana matatizo ya kifamilia na alikuwa chaguo la kwanza kabla ya Yanga kuamua kumshusha Mserbia huyo Agosti 29.
0 COMMENTS:
Post a Comment