TANZANIA
ilisafiri na kombe kwenda nchini Afrika Kusini, hilo lilikuwa ni kombe la
ubingwa wa Baraza la Mashirikisho ya Michezo Kusini mwa Afrika (Cosafa) kwa
wachezaji chini ya miaka 20.
Safari hiyo
ilikuwa ni kwenda nchini Afrika Kusini inapofanyika michuano ya Cosafa na
Tanzania pekee wakiwa ni waalikwa kwa kuwa wako Ukanda wa Afrika Mashariki na wanapewa
heshima hiyo zaidi ya mara mbili sasa kutokana na ubora ambao timu za Tanzania
zimekuwa zikionyesha.
Wakati wa
kurudi nyumbani, Tanzania imerudi na kombe la ubingwa wa wachezaji chini ya
miaka 17. Hii maana yake, Tanzania walikwenda Afrika Kusini na kombe ambalo
walitakiwa kulikabidhisha na wamerejea na kombe.
Kwa kuwa
watu wengi hawafuatilii sana soka la wanawake, wanaweza wakawa wanapuuzia
lakini uhalisia ni kwamba Tanzania kwa zaidi ya miaka minne sasa, imekuwa
ikipata heshima kubwa kupitia dada na wadogo zetu.
Wamekuwa na
juhudi kubwa na kuna mabadiliko makubwa katika mechi za wanawake kuanzia hapa
nyumbani lakini pia katika michuano ya kimataifa.
Wanawake
wamekuwa washindani wakubwa na sasa wametengeneza heshima kubwa kwenye nchi
zote chini ya Ukanda wa Jangwa la Sahara na sasa kila anayeambiwa atakutana na
Tanzania, anajiuliza mara mbili.
Mara kadhaa,
tumeona hata timu za Afrika Kaskazini ambazo kwa soka la wanaume ndizo
zinaongoza barani Afrika, zimekuwa na hofu na Tanzania katika michuano
mbalimbali.
Tanzania
sasa inapaswa kuanza kuchuana na timu Afrika Magharibi ili kutafuta ukubwa
unaotambulika Afrika. Na nilifika Afrika Kusini na kushuhudia mechi zote za
Tanzania za michuano ya Cosafa, hakika lilikuwa ni jambo la kujivunia na
inaonyesha wazi kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limewekeza na limepania
kupata mafanikio makubwa kwa upande wa wanawake.
TFF wameona
namna ambavyo dada zetu wamekuwa wakijituma na kufanya vema. Wameona namna
ambavyo wamekuwa wakijitoa na kupambana na wao tokea wamechukua kutoka kwa
uongozi uliopita, wao wameongeza nguvu kubwa na matunzo ya juu ya timu za
wanawake.
Katika
michuano ya Cosafa, Tanzania ilienda na timu mbili katika michuano miwili
tofauti. Ile ya wakubwa na ile ya chini ya miaka 17.
Timu ya
wakubwa, Twiga Stars ilitolewa baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Zambia,
ikapoteza moja dhidi ya Botswana, zote matokeo yalikuwa bao 1-0. Lakini bado
timu ilionyesha kiwango bora kabisa, hata kama umetolewa unaona ubora
uliokuwepo ni ule wa kujivunia.
Kwa timu ya
chini ya miaka 17, yenyewe ilicheza mechi tano na kushinda nne. Ilianza kwa
kuichapa Comoro 4-1, ikakutana na Zambia na kupoteza kwa mabao 2-1. Mechi ya
tatu, ikawatandika wenyeji Afrika Kusini 6-1 kabla ya kuwashindilia Zimbabwe
kwa mabao 10-1.
Fainali na
Zambia, ikawa 1-1 kwa dakika 90, mwisho kwa mikwaju ya penalti Tanzania ikashinda
kwa 4-3. Ni jambo la kujivunia kutokana na ubora wa kiwango na matunzo sahihi
wanayopewa wanapokuwa kambini.
Lazima tukubali
kwamba hata kama ni jukumu lao lakini TFF wanaifanya kazi yao kwa weledi na
wanatoa uangalizi na matunzo sahihi kwa wachezaji wa timu za taifa.
Mfano, zaidi
ya madaktari watatu walisafiri na timu hizo mbili kuhakikisha kila kitu
kinakwenda kwa usahihi kuhusiana na masuala ya afya za wachezaji lakini
walipata kila kitu kwa weledi wa juu likiwemo suala la motisha.
Baada ya
kuwa wamepoteza mechi dhidi ya Zambia, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alitoa
ahadi ya takribani Sh 500,000 kwa kila mchezaji ili warejee katika kiwango.
Hakukuwa na kuwalaumu, badala yake walielezwa walichokosea, wakaaswa
kurekebisha na kupewa motisha.
Kwa watu wanaolala vizuri, wanakula vizuri, wanasafiri vizuri, chini ya uangalizi wa mameneja wazuri na madaktari bingwa na maarufu. Lazima walete matokeo mazuri na hii ndio kazi kubwa wanayofanya TFF ambao tunapaswa kuwapongeza na kuwaunga mkono na hili lianzie kwa mashabiki wanaoipenda nchini yao ya Tanzania, wapenda mpira lakini hata kwa makampuni na Serikali ya Tanzania.Hongereni TFF kwa kazi nzuri.
Hivi team mwalikwa anaruhusiwa kuondoka na kombe?au wanasheherekea nalo kisha wanaliacha na kuondoka na zawadi ikiwamo fedha?
ReplyDeleteHongereni TFF kwa kazi nzuri. Tumeondoka nalo sawa tumeliacha Zawadi ya Fedha hatuwezi kuacha hata kidogo. HONGERA KWA AKINA DADA, TFF na wadau wote wa Michezo pamoja na sisi mashabiki pongezi kwetu sana.
ReplyDelete