WANASEMA
mfungwa hachagui gereza na ule msemo wa mkulima hachagui jembe, hii haina
tofauti na harakati za kijana wa Kitanga, Salim Jengo Mtango.
Mtango
mwenye umri wa miaka 25 lakini hajawahi kukata tamaa ya kimaisha kutokana na
kufanya kazi nyingi kabla ya kuingia katika mchezo wa ngumi za kulipwa licha ya
mengine kuendelea nayo hadi sasa.
Kirekodi
bondia huyo mwenyeji wa Makorora, amecheza jumla ya mapambano 16 akiwa
ameshinda 13 kati ya hayo nane kwa KO,
amepigwa mapambano matatu kati ya hayo moja kwa KO.
Achana na
rekodi zake na ule ufundi wake akiwa kwenye ulingo lakini tayari anashikillia
mikanda kadhaa ya ubingwa aliyofanikiwa
kuitwaa tangu alivyoanza mchezo wa ngumi.
Huenda akawa
pia hajulikani sana lakini kwa Tanga, Mtango anapendwa na kukubalika zaidi
kutokana na ukaribu wake pamoja na maisha yake ya kujichanganya katika kazi
mbalimbali licha ya ubondia wake.
Bondia huyo
ambaye anajiandaa na pambano lake la kimataifa dhidi ya Eduardo Mancito kutoka
Ufilipino ambalo linatarajia kupigwa Novemba 28, mwaka huu kwenye Ukumbi wa
Next Door uliopo Masaki jijini Dar chini ya udhamini wa Gazeti la Spoti Xtra,
+255 Global Radio, DSTV, Plus TV, Kebbys Hotel, Clouds Fm na kinywaji cha Smart
Gin.
Championi
ambalo lilipiga kambi katika jiji la Tanga na kuweza kumshuhudia bondia huyo
akijishughulisha na uuzaji wa Pweza nyakati na usiku pamoja na masuala ya uvuvi
ndani ya bahari ya Hindi licha ya kupanda ulingoni kupigana.
Wenyeji wa
Tanga wanaeleza kuwa kijana huyo hachagui kazi kwani pia alishawahi kuhusika
na uuzaji wa dagaa wa mchele maarufu zaidi kwa watu wa ukanda wa Pwani kama
Uwono katika soko la Makorora.
Mtango
mwenyewe anasema ameshafanya kazi nyingi kwa lengo la kutafuta pesa kwa ajili
ya kuendesha kazi zake.
“Nafanya
mambo mengi, bodaboda naendesha, shughuli ya kusajili laini nimefanya hata
hapa kwenye soko la Makorora nimeuza sana samaki wabichi huko nyuma.
“Sasa hivi
bado nauza Pweza, wapo vijana ambao wananisaidia kwa sababu ya ratiba yangu
kuwa ngumu hasa upande wa mazoezi.
“Ninachofanya
asubuhi huwa naenda mazoezini, kisha nikirudi naenda kukusanya Pweza,
nawaachia vijana wanaanda kwa ajili ya biashara jioni.
“Nikitoka
hapo nitaenda kwenye kijiwe cha kahawa kucheza drafti na kuongea, huwa naenda
kucheza mpira, namudu kucheza nafasi ya kipa, namba 11 na beki wa kushoto bila
ya shida.
“Baada ya mizunguko hiyo ndiyo narudi kwenye kuuza Pweza kwa lengo la kuwasaidia vijana majukumu yao na hiyo imekuwa kawaida kwa kuwa mimi ni mtu wa watu."
Baada ya maongezi hayo siku ya pili, bondia huyo alitupeleka katika eneo la ufukwe wa Sahare ambapo kuna bandari ndogo ya wavuvi na sehemu ambayo alikua akifanya shughuli zake za uvuvi. Championi liliweza kuhushuhudia namna alivyokua akifanya mambo mbalimbali akiwa baharini.
Nimeambiwa
wewe ni mvuvi?
“Hawajakudanganya
kweli mimi ni mvuvi, nafanya shughuli hizo japo sasa wazee hawataki niende kule
kwa sababu wanasema nimepata kazi yenye uafadhali.
“Lakini
kwenye kuvua nimevua na hadi leo navua, nakumbuka siku ya kwanza katika kuvua
tulienda sehemu mmoja inaitwa Deep Sea hapahapa, Tanga, tulivua lakini
tuliambulia 500 kila mmoja wetu kwa ajili ya chai kwa kuwa hali haikuwa nzuri.
Kitu
gani huwezi kusahau ndani ya bahari?
“Unajua mara
ya kwanza kwenye kuvua nilifika Kasera huko nikaomba lifti katika vyombo vya
wavuvi wengine hadi Kenya, huko nikavua sana sasa wakati tunarudi tulikutana na dhuruba kali kiasi mawimbi yalikuwa yanafunika jahazi, sisi wavuvi wote
tukaingia ndani ya jahazi kujificha juu akabakia nahodha peke yake.
“Kiukweli
ilikua ni Mungu maana nilikua nahisi
ndiyo mwisho wetu na tukio lingine lilikuwa ndani ya bahari, nahodha wachombo
alinitukana kisha akanipiga kibao kwa kuwa nilikosea kuvuta kamba ya nyavu, ukweli nilimrudishia kwa kumtandika
ngumi tatu kwa sababu hakutakiwa kunitukana.
“Lakini
baada ya hapo ikabidi niombe lifti kwenye chombo kingine kurudi nchi kavu na
hapo ndiyo nikaanza kuacha kwenda baharini lakini katika kuvua nipo sawa kabisa,”
anasema Mtango.
0 COMMENTS:
Post a Comment